Jumanne, 16 Juni 2026

MAHAKAMA SUMBAWANGA YAFANYA ZIARA YA UKAGUZI WA MAGEREZA

Na. SHARIFU MOKIWA – Mahakama, Sumbawanga

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Frederick Kapela Manyanda amefanya ziara ya kutembelea Gereza la Mahabusu Sumbawanga na Gereza la Mollo la Kilimo kwa ajili ya kusikiliza changamoto mbalimbali za wafungwa na Mahabusu wa magereza hayo, ikiwa ni zaira ya ukaguzi wa kawaida katika kipindi cha Juni, 2026.

Akiwasilisha taarifa fupi ya Gereza Kuu la Mahabusu Sumbawanga jana tarehe 15 Juni, 2026 Mkuu wa Gereza Mahabusu Sumbawanga Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Ally M. Abdallah  alieleza hali za wafungwa na mahabusu waliopo gerezani hapo.  

Mhe. Manyanda alipata fursa ya kukutana na Wafungwa na Mahabusu ambao waliwasilisha changamoto zao kwa viongozi mbalimbali wa Mahakama na wadau wengine wa haki jinai alioambatana nao,

Akijibu hoja mbalimbali Mhe. Manyara alielekeza kuharakishwa kwa hatua za upelelezi wa mashauri mbalimbali yanayohusisha Watoto ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati mapema ipasavyo na wahusika wanapata huduma stahiki kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Mhe. Mnyanda, alielekeza kubainishwa kwa changamoto zinazo kwamisha mwenendo wa mashauri ya jinai na kuzitaka kamati za haki jinai kushirikiana kwa karibu katika kuzitatua pamoja na kusukuma mbele mashauri yaliyopo ili kupunguza mlundikano wa mashauri.

Katika risala yao wafungwa na mahabusu katika Gereza la Mahabusu Sumbawanga waliweza kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili gerezani hapo mbele ya Mhe. Manyanda. Aidha, Mhe. Manyanda aliahidi kuzishughulikia changamoto zote zilizowasilishwa katika risala zao na zile ambazo zipo nje ya uwezo kuziwasilisha katika mamlaka husika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Mahabusu Sumbawanga ACP Ally M. Abdallah alitoa shukurani zake kwa ujio wa ziara hiyo, kwa kuwa umekuwa na tija kubwa kwao kwa kutoa fursa kadhaa ikiwemo matendo ya huruma na kushughulikia suala la kupunguza mlundikano wa mahabusu gerezani hapo.

Katika ziara hiyo Mhe. Manyanda aliambatana na Viongozi mbalimbali wa Mahakama akiwemo Mtendaji Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Sumbawanga  Bw. Machumu Essaba, Msaidizi wa Sheria, Mkuu wa upelelezi Mkoa, Kaimu Hakimu Mkazi Mkoa, Hakimu Mfawidhi wa Wilaya, Afisa Ustawi  Mkoa, Mkuu wa Mashtaka Mkoa, Mwakilishi wa Kamanda Takukuru Mkoa, Ofisi ya Upelelezi Mkoa, Afisa Huduma na Uangalizi, Afisa Uhamiaji Mkoa, Mkuu wa Magereza Mkoa na wadau wengine wa Haki jinai.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Frederick Kapela Mnyanda (katikati) akiwa pamoja na wadau wengingine wa haki jinai wakiwa katika gereza la kilimo Mollo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Sumbawanga Mhe. Frederick Kapela Manyanda (kushoto) akipokea risala kutoka kwa Afisa wa Jeshi la Magereza.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Sumbawanga Mhe. Frederick Kapela Manyanda (mbele ya picha kulia) akiwasili katika ukaguzi wa Gereza la Mahabusu Sumbawanga. 

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)

  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni