Na DOTTO NKAJA-Mahakama, Geita
Aliyekuwa Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Geita,
Mhe. Kevin Mhina, tarehe 12 Juni 2026 alikabidhi
ofisi kwa Jaji Mfawidhi mpya, Mhe. Projestus Kahyoza, baada ya kuripoti katika
kituo chake kipya cha kazi.
Akizungumza wakati wa
hafla ya makabidhiano, Mhe. Mhina alisema kuwa taratibu zote za kikazi na
taarifa muhimu za ofisi zilishakabidhiwa kwa njia ya barua pepe za kikazi.
Aidha, alibainisha kuwa
anamwachia Jaji Kahyoza timu ya Watumishi
wenye ushirikiano mkubwa na wenye kujituma katika kuhakikisha majukumu ya
Mahakama yanatekelezwa kwa ufanisi.
“Nimekuachia Watumishi wenye ushirikiano mzuri sana
ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa kujituma na kuhakikisha huduma za utoaji haki
zinaendelea kutolewa kwa Wananchi
kwa wakati,” alisema Mhe. Mhina.
Kwa upande wake,
akizungumza wakati wa kumpokea Jaji Mfawidhi mpya, Mhe. Mwakapeje
alimhakikishia ushirikiano wa hali na mali kutoka kwa Watumishi wote wa Mahakama Geita.
Alieleza kuwa Watumishi wa Mahakama hiyo ni wenye maadili
mema na wako tayari kushirikiana ili kuhakikisha majukumu ya Mahakama
yanaendelea kutekelezwa kwa ufanisi.
Akizungumza baada ya
kupokea ofisi, Mhe. Kahyoza aliwashukuru Viongozi
na Watumishi wote wa Mahakama Geita kwa mapokezi mazuri
aliyoyapata. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuongeza
ufanisi katika utoaji wa haki kwa Wananchi.
“Naomba tuendelee
kushirikiana kwa dhati ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuimarisha
zaidi utoaji wa haki kwa wakati kwa kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na
mawasiliano (TEHAMA),” alisema Mhe. Kahyoza.
Naye Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu Geita,
Mhe. Fredrick Lukuna, alimpongeza Jaji Kahyoza kwa kuaminiwa na kuteuliwa
kuongoza Mahakama Geita.
Alimhakikishia kuwa Watumishi
wa Mahakama wataendelea kumpa ushirikiano unaohitajika ili kufanikisha majukumu
yake mapya.
Mhe. Lukuna pia alieleza
kuwa Mahakama Geita itaendelea
kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika shughuli za Mahakama kwa lengo la kuongeza
ufanisi na kuboresha huduma kwa Wananchi.
Katika kuonyesha furaha
ya ujio wake, Watumishi
wa Mahakama Kuu Geita waliandaa keki maalum kwa ajili ya kumkaribisha Jaji
Mfawidhi mpya katika kituo chake kipya cha kazi.
Makabidhiano hayo yanaashiria mwanzo wa hatua mpya ya uongozi katika Mahakama Geita, huku yakionesha dhamira ya kuendeleza ushirikiano, ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kuimarisha utoaji wa haki kwa Wananchi.
Watumishi wa Mahakama Kuu Geita wakimpokea Jaji Mfawidhi
mpya, Mhe.
Projestus Kahyoza.
Jaji Mfawidhi mpya, Mhe. Projestus Kahyoza
akisaini
kitabu baada ya kuripoti katika kituo chake kipya.
Aliyekuwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Geita, Mhe Kevin Mhina, akipeana mkono kama ishara ya makabidhiano na Jaji
Mfawidhi mpya, Mhe. Projestus Kahyoza.
Picha ya Majaji.
Keki iliyoandaliwa kumkaribisha
Jaji Mfawidhi,
Mhe. Projestus Kahyoza.
Watumishi wa Mahakama Kuu Geita wakiwa katika kikao kifupi
cha kumpokea Jaji Mfawidhi mpya.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni