Jumatatu, 15 Juni 2026

SUMBAWANGA YAMPONGEZA KISASILA SAGUDA KWA UTEUZI WA UNAIBU MSAJILI

Na. SHARIFU MOKIWA – Mahakama, Sumbawanga

Watumishi na Viongozi wa Mahakama wampongeza Mhe. Kisasila Saguda kwa kuteuliwa kwake kuwa Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, katka hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Sumbawanga.

katika hafla hiyo maalumu ya kumpongeza Mhe. Saguda iliwakutanisha Watumishi na Viongozi mbalimbali wa Mahakama ili kumpongeza aliyekuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Sumbawanga kufuatia kuteuliwa kwake kuwa Naibu Msajili wa Mahakama ya Tanzania.

Hafla hiyo ilifunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Sumbawanga, Mhe. Frederick Kapela Manyanda na ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama pamoja na watumishi kutoka Idara mbalimbali. Miongoni mwa viongozi walioshiriki ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Sumbawanga, Mhe. Thadeo  Mwenempazi, Mtendaji  wa  Mahakama  Kuu Masjala Ndogo ya  Sumbawanga,  Bw. Machumu  Essaba,  Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala ndogo  ya Sumbawanga  Mhe, Pamela Mazengo  pamoja na watumishi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Saguda alitoa shukrani zake kwa uongozi wa Mahakama kwa imani waliyoionesha kwake kupitia uteuzi huo, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano, upendo na uwajibikaji katika utendaji wa kazi.

“Ushirikiano, upendo na kazi vinakwenda pamoja, hivyo tusiviache nyuma. Napenda kushukuru uongozi wa Mahakama kwa namna ambavyo wameniona nafaa kuchukua nafasi hii ya Naibu Msajili wa Mahakama ya Tanzania na ninaahidi kuwa nitahakikisha nachapa kazi kuonyesha kwamba uteuzi walioufanya hawakukosea,” alisema Mhe. Saguda

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Sumbawanga, Mhe. Mwenempazi, alimtakia kila la heri Mhe. Saguda katika majukumu yake mapya, akieleza kuwa mafanikio aliyoyapata yametokana na utendaji wake mzuri wa kazi na mahusiano mema na wenzake.

“Tunakutakia kheri katika yote utakayoyatenda katika nafasi yako. Lakini yote uliyokuwa unatufanyia sisi hapa, popote utakapoenda usisahau kuyafanya hivyo, kwani baraka zako zimekuja kwa sababu ya hayo mazuri uliyoyafanya,” alisema Mhe. Mwenempazi.

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Sumbawanga, Mhe. Manyanda, alitumia fursa hiyo kueleza kanuni muhimu zinazopaswa kuongoza maisha na utendaji wa Afisa wa Mahakama ili kufikia mafanikio katika kazi.

“Kuna kanuni sita ambazo Afisa wa Mahakama akiziishi lazima atafanikiwa; uhuru wa kufanya jambo lolote bila kuingiliwa na bila uoga, kutokuwa na upendeleo, uadilifu ambao ndiyo msingi wa majukumu yetu, mwenekano, usawa pamoja na weledi. Hivyo sote tuzingatie kanuni hizi. Lakini pia namtakia kheri, naamini anaweza, alistahili, anastahili na ataweza. Mwenyezi Mungu aendelee kumuinua zaidi na zaidi,” alisema Jaji Manyanda.

Katika kuonesha kuthamini mchango wake katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga, Mhe. Saguda alipokea Kitabu maalum cha kumbukumbu za utendaji kazi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga kutoka kwa Jaji Mfawidhi Mhe. Manyanda. Kitabu hicho kinajumuisha historia ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo pamoja na picha na majina ya watumishi wake, ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu na ukumbusho wa ushirikiano na mchango wake.

Kwa ujumla, hafla hiyo ilikuwa ishara ya kuthamini utumishi uliotukuka, kujenga moyo wa kufanya kazi kwa bidii na kuhamasisha watumishi wengine kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kujituma kwa manufaa ya taasisi na wananchi wanaohudumiwa na Mahakama.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Sumbawanga, Mhe Frederick Manyanda (aliyesimama) akitoa Nasaha fupi wakati wa hafla ya kumpongeza Mhe, Kisasila Saguda wakati wa pongezi hizo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mteule Mhe. Kisasila Saguda aliyekuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Sumbawanga   akitoa Shukrani baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Msajili wa Mahakama ya Tanzania.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Thadeo Mwenempazi akimpongeza na kumtakia kheri Mhe. Kisasila Saguda baada ya Uteuzi huo wa kuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Pamela Mazengo (aliyesimama) akitoa neno wakati wa afla hiyo, kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga  Machumu Essaba na kushoto ni Mhe Kisasila Saguda aliyeteuliwa kuwa Naibu Msajili wa Mahakama ya Tanzania.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Frederick Kapela Manyanda [kushoto] akimpatia kitabu Mhe. Kisasila Saguda [Kulia] kikiwa na picha na majina ya watumishi wake, ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama waliohudhulia katika hafla hiyo maalum ya kumpongeza Mhe. Saguda kwa Uteuzi huo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni