Na. ELIUD ANDREW KIWANGA – Mahakama, Songwe
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Pascal Malata aongoza hafla ya uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Msangano iliyopo Kata ya Msangano Wilaya ya Momba Mkoa wa Songwe na kufanyika katika viunga vya Mahakama ya Mwanzo Msangano
Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mfawidhi Mahakama
Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Pascal Malata aliishukuru
Serikali ya awamu ya sita kwa kuwezesha ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Msangano,
Aidha, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuiwezesha
Mahakama ya Tanzania na kuhakikisha inakuwa na miundombinu ya kisasa. Vilevile aliishukuru
Mahakama ya Tanzania chini ya Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Geoge M.
Masaju kwa kuendelea kubuni miradi mbalimbali ya uboreshaji wa Miundombinu ya
Mahakama.
Mhe. Malata alisema kuwa, ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo
Msangano ni ishara ya Serikali ya awamu ya sita kuwathamini na kuwajali wananchi wa Msangano na maeneo jirani
kwa kuwasogezea huduma ya upatikanaji wa haki na kuwa tofauti zozote za
kisiasa, kijamii, kiuchumi, kiitikadi zisiwe sababu ya kuharibu miundombinu ya
Mahakama ya Mwanzo Msangano.
“Hivyo wananchi wote kwa pamoja wanao wajibu wa
kulinda na kutunza miundombinu ya Mahakama hiyo kwasababu ni mali ya umma na
imejengwa kwa kodi za wananchi wenyewe. Wananchi wa Msangano wamepata bahati
kujengewa Jengo la kisasa la Mahakama mapema ikilinganishwa na maeneo mengine.
Nawaasa wananchi wa Msangano kuishi wa amani na upendo ili kuepuka migogoro
kwani migogoro hurudisha nyuma maendeleo ya jamii,” alisisitiza Jaji Mfawidhi
Malata.
Mhe. Malata aliwashukuru wanachi wote wa Msangano na maeneo jirani kwa kuwa walipa kodi wazuri na kufika katika hafla ya uzinduzi katika viunga vya Mahakama ya Mwanzo Msangano na pia aliushukuru uongozi wa Wilaya ya Momba kwa kuupokea mradi, kuusimamia na kuulinda mpaka ulipokamilika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Momba Mhe. Elius
Daniel Mwandobo alianza kwa kuwaomba wananchi kuepuka tabia ya kujichukulia
sheria mkononi kwani kwa kufanya hivo ni kinyume na sheria na pia alimshukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuendelea kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya Mahakama maeneo mbalimbali nchini.
Mhe. Daniel Mwandobo aliipongeza Mahakama ya Tanzania
kwa kuendelea kutumia mifumo ya kidigitali kwani kwa kufanya hivyo kumepunguza
gharama, muda wa ufatiliaji na pia imeimarisha mifumo ya utoaji wa haki.
Vile vile aliwaasa wananchi wasiiogope Mahakama bali
wailinde na kuitunza na pia siyo mashauri yote yanapaswa kwenda mahakamani bali
watumie pia njia za usuluhishi kutatua baadhi ya migogoro miongoni mwao. Aidha,
aliipongeza Serikali na Mahakama ya Tanzania kwa kuanza kwa mchakato wa ujenzi
wa Mahakama ya Wilaya ya Momba inayotarajiwa kujengwa katika mji mdogo wa
Chapwa.
Naye, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Momba Bw. Kataba
Sukuru aliishukuru Serikali ya awamu ya sita na Mahakama ya Tanzania kwa
kuwezesha ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Msangano.
Bw. Sakuru aliahidi kuendelea kushirikiana na uongozi
wa Wilaya ya Momba na Mahakama ya Tanzania ili kuhakikisha huduma za msingi
ikiwemo huduma ya Haki inapatikana kwa wananchi wa Kata ya Msangano pamoja na wa Wilaya ya Momba kwa ujumla.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na sehemu ya viongozi wa ngazi ya Wilaya wakiwemo Mkuu wa Wilaya ya Momba Mhe. Elius Daniel Mwandobo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma Bw. Salumu Kyambi, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba Bw. Paul Sheyo, Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Momba Mhe. Raymond Kaswaga, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Momba Bw. Sukuru Kataba pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe Mhe. Francis Kishenyi.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Ndogo
ya Songwe Mhe. Gabriel Pascal Malata akihotubia wakati wa uzinduzi wa Mahakama
ya Mwanzo Msangano.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Malata (wa pili kulia) akiwa katika hafla ya uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Msangano, (wa kwanza kulia) ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Songwe Mhe. Francis Kishenyi, (wa tatu kulia) ni Mkuu wa Wilaya ya Momba Mhe. Elius Daniel Mwandobo, (wanne kulia) ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Tunduma Bw. Salumu Kyambi na Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Momba Bw. Paul Sheyo wakifuatilia hafla hiyo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Malata (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Momba Mhe. Elius Daniel Mwandobo katika zoezi la kukata utepe.
Sehemu ya wageni waalikwa waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa
Mahakama ya Mwanzo Msangano.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Pascal Malata (katikati) wakiwa kwenye picha ya pamoja ya viongozi wa Mahakama Mkoa wa Songwe pamoja na Viongozi mbalimbali wa ngazi ya Wilaya ya Momba nje ya jengo la Mahakama ya Mwanzo Msangano.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Momba Bw. Sukuru Kataba akitoa
neno akiwa katika hafla ya uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Msangano.
Mkuu wa Wilaya ya Momba Mhe. Elius Daniel Mwandobo
akitoa neno katika hafla ya uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Msangano.
Mkuu wa Wilaya ya Momba Mhe. Elius Daniel Mwandobo akipanda mti wa kivuli katika
viunga vya Mahakama ya Mwanzo Msangano.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni