Ijumaa, 12 Juni 2026

JAJI MKUU AWATAKA WADAU WA HAKI JINAI KUIMARISHA UMAKINI KATIKA UPELELEZI

 ·       Awataka pia wazingatie matakwa ya Kifungu cha 134 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai na Kanuni za Jaji Mkuu

·       Asisitiza Polisi kutoa dhamana kwa watuhumiwa kwa mujibu wa sheria

·       Amtaka kila mdau kusimama ipasavyo katika eneo lake kuboresha Haki Jinai

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amewataka Wadau wa Haki Jinai nchini kuendelea kuimarisha umakini katika upelelezi wa mashauri ya Jinai ya aina zote na uendeshaji wa mashauri ya jinai Mahakamani kwa kuzingatia Katiba na Sheria ipasavyo.

Mhe. Masaju aliyasema hayo jana tarehe 11 Juni, 2026 alipokuwa akifunga Mkutano wa Mahakama na Wadau kuhusu ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki mahakamani uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu uliopo Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mkuu amesema kuwa, “miongoni mwa Taasisi ambazo zinaongoza kufanya/kushiriki Mafunzo ya ndani na nje ya Nchi ni Taasisi zinazohusika na upelelezi, hivyo tunataka kuona matunda yake na matokeo yake kazini.”

Jaji Mkuu amesema, zoezi la upelelezi liendane na Kifungu cha 134 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai kinachotaka mashauri yafunguliwe Mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika isipokuwa kwa makosa ambayo ni makubwa na yale ambayo yanasikilizwa na Mahakama Kuu kama ilivyotajwa katika kifungu cha 134(4).

Aidha, amempongeza Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa kuweka Mwongozo ambao ni Sheria ambayo hata katika mashauri makubwa, upelelezi uwe umekamilika ndani ya siku 90 ili shauri lianze kusikilizwa.

“Yazingatieni hayo, lakini pia endeleeni kuzingatia na kanuni zilizotolewa na Jaji Mkuu kuhusu watuhumiwa kupata maelezo ya ushahidi dhidi yao, kabla ya kusomewa mashtaka kwa mara ya kwanza (Preliminary hearing) na kesi kuanza kusikilizwa ili kesi zinaposikilizwa wawe wanafamu ushahidi dhidi yao kama ilivyo kawaida katika Mahakama Kuu, hapo ndipo kutakuwa na usikilizwaji kikamilifu ile (fair trial) inayozungumzwa katika Katiba Ibara ya 13(6),” amesema Mhe. Masaju.

Sambamba na hilo, Jaji Mkuu amesema kuwa, kuna changamoto ya dhamana kwa upande wa Polisi ambapo amesema, “niwaombe Polisi, mmepewa mamlaka chini ya kifungu namba 65 mpaka 70 vya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai na bahati mbaya sisi tunawafamu ninyi Polisi peke yenu, lakini kuna Taasisi nyingine ambazo zinakamata watu zinaleta kwenye vituo vyenu. Vituo vyenu unakuta vimejaa, sasa sijui kama mna fedha za kutosha au ni vikubwa kiasi gani, hii yenyewe ni sababu ya msingi kwa makosa yale ambayo yanadhaminika kuwapa dhamana,” ameeleza Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amewashauri Polisi kutoa dhamana kwakuwa kifungu namba 65 mpaka 70 vya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai kimeeleza vizuri. “Wapeni dhamana itatupunguzia pia na hizi tuhuma nyingine zisizokuwa na sababu mtu anaweza akajidhamini au anaweza akadhaminiwa na mtu, mpeni dhamana, msipoweka utaratibu wa kuwa dhamana watajaa mahabusu na kusababisha magonjwa ya mlipuko hata wengine wanaweza wakafia Mahabusu ikawa shida, kwahiyo hakuna sababu ya kuogopa kuwapa dhamana kama umewakamata kwa usahihi kabisa wapeni dhamana,” amesisitiza Mhe. Masaju.

Ameongeza kuwa, Sheria inaelekeza kuhusu mtuhumiwa kutakiwa kufikishwa Mahakamani ndani ya saa 24 tangu alipokamatwa, hii itasaidia na kwa upande wa makosa ya uhujumu Uchumi wanatakiwa kufikishwa Mahakama ya Wilaya iliyo jirani na alipokamatwa ndani ya saa 48.

Kadhalika, amewataka kuzingatia masharti ya Kifungu cha 34 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai kinachowataka Mkuu wa Kituo cha Polisi kutoa taarifa ya kila Mtuhumiwa aliyekamatwa bila kibali cha Mahakama (Warrant of Arrest) na ambao wako ndani ya Vituo vya Polisi na wale waliopata dhamana. “Hili ni takwa la kisheria, zingatieni haya masharti, faida zake ni nyingi na tumezitafakari hapa wote, hapa hakutakuwa na cha Mswalia Mtume, zingatieni hayo masharti ili twende kwa sababu hata tusiposema hayo mengine ni vizuri tukayazingatia yote haya,” amesisitiza.

“Kwa upande wa Mahakama, wajibu wetu tuutekeleze ipasavyo bila kutumia madaraka yetu vibaya,” amesema Jaji Mkuu huku akiwaahidi Wadau hao kuwa, Mahakama itaendelea kuwa makini kwa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Ibara ya 107A(1)(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) kwa sababu ndio Wasimamizi wa Sheria hizo kwa sababu kuna changamoto katika eneo la upelelezi.

“Lakini wajibu wetu wa kuandaa vitabu vya Rufaa kwa Wafungwa wanaotoka Mahakama Kuu kuja Mahakama ya Rufani, tuviandae na kuvikamilisha hivi vitabu na kuwapatia wahusika ili waweze kukamilisha sababu zao za Rufaa, hivyo hivyo Mahakama tuwapatie wengine wanaotaka kukata rufaa labda kutoka Mahakama ya Wilaya au Hakimu Mkazi kuja Mahakama Kuu, wanaotaka nakala za hukumu, wanaotaka mwenendo wa mashauri tuwapatie mapema ipasavyo ili waweze kuandaa rufaa zao,” amesema Mhe. Masaju huku akisisitiza yote ambayo yamesemwa kuhusu Mahakama yatekelezwe na kila mdau wa mkutano huo atekeleze majukumu yake ipasavyo ili kushughulikia changamoto.

Jaji Mkuu amewataka Wadau hao wa Haki Jinai wakiwemo Magereza, Polisi, TLS na Wadau wengine kama kuna changamoto zozote zinazokwamisha upatikanaji haki wasisite kutoa taarifa Mahakama badala ya kusubiri siku ya vikao tu.

“Mahakama ina nafasi kubwa sana katika ustawi na maendeleo ya Taifa letu, bila na kuwa na amani na utengamano katika Taifa, maendeleo gani yatatoka katika Taifa hilo, watu hawatafanya siasi, watu hawatafanya shughuli zao za kiuchumi, hawatafanya shughuli zao za kijamii ikiwa ni pamoja na shughuli za siasa na kufunga ndoa na kushiriki katika matamasha, kwahiyo tuna dhamana kubwa katika hili ili Taifa hili lidumu kuwa la udugu kama ilivyokuwa zamani tunaitana ndugu. Amani na udugu ndivyo vinavyohimizwa katika Katiba kupitia Ibara ya 9, hivyo simamieni utekelezaji wa sheria kwa ufanisi ipasavyo,” amesema.

Aidha, Jaji Mkuu amesema kuwa, katika hotuba yake ya Siku ya Sheria nchini mwaka huu alieleza mambo ambayo Mahakama inafanya katika kuchangia ustawi na maendeleo ya Taifa. Amesema, “Kaulimbiu yetu ya Mahakama kwa mwaka huu 2026 ni; Mchango wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa.”

Ameeleza kuwa, Mahakama na wadau wake ni watu muhimu katika kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050 ambayo msingi wake mkuu ni Utawala, Amani, Usalama na Utulivu na vipaumbele vinne ambao ni Utawala Bora na Haki, Serikali za Mitaa Imara na zenye ufanisi, Utumishi wa Umma unaowajibika na Amani, Usalama na Utulivu ambapo kila mdau anahusika.

Amesema kuwa, pamoja na kwamba, Mahakama inatekeleza wajibu wake, inajikita kuangalia ni kwa namna gani Mhimili huo unachangia katika ustawi na maendeleo ya Taifa. “Sasa moja tunajua umuhimu wa Mahakama katika jamii, sasa katika kipindi hiki tangu tulivyokutana tarehe 02 Machi, 2026 mwaka huu Mahakama Kuu sita ambazo ni Njombe, Singida, Lindi, Simiyu, Songwe na Katavi zimezinduliwa na kufanya kazi na Mahakama za Mwanzo 15 nazo zimezinduliwa na kuanza kufanya kazi. Amesema kwa Tanzania Bara umebaki Mkoa mmoja pekee ambao hauna Masjala ya Mahakama Kuu ambao ni Pwani.

“Tumesogeza huduma zetu za Mahakama kwa watu ili haki ipatikane, kuwepo na amani na utulivu watu waweze kushiriki shughuli zao za kiuchumi, za kisiasa na kijamii kwa ufanisi ipasavyo. Kwa hiyo wenzetu mnaohusika na huduma za upelelezi mjue sasa kuna huduma za Mahakama Kuu katika hiyo Mikoa,” amesema Mhe. Masaju.

Ameongeza kuwa, Ibara ya 25(1) ya Katiba inasema; Kazi pekee ndio huzaa utajiri wa mali katika jamii, ndilo chimbuko la ustawi wa wananchi na kipimo cha Utu. Na kila mtu anao wajibu wa: - a) kushiriki kwa kujituma na kwa uaminifu katika kazi halali na ya uzalishaji mali na b) kutimiza nidhamu ya kazi na kujitahidi kufikia malengo ya uzalishaji mali ya binafsi na yale malengo ya pamoja yanayotakiwa au yaliyowekwa na sheria.

Kadhalika, Jaji Mkuu amewakumusha Wadau hao kuhusu mikakati waliyokubaliana ambayo ni endelevu, ambapo mkakati wa kwanza unasema, kila Taasisi ambayo ni Mdau wa Mnyororo wa Utendaji Haki Mahakamani iwajibike ipasavyo kwa kutekeleza jukumu lake kwa kuzingatia Katiba, Sheria na maadili ya utumishi yanayosimamia Taasisi ipasavyo.

Na Mkakati wa pili ni kwamba Wadau wote Waheshimu na kulinda hadhi ya Mahakama, aidha Mahakama kwa upande wake, isimamie sheria na kanuni zilizopo ikiwemo sheria inayohusu kosa la kuidharau Mahakama yaani ‘Contempt of Court’ ili kulinda hadhi na ukuu wake.

Amesema kuwa, Sharti hilo ni la Kikatiba na lipo kwenye Ibara ya 30 (1) na ya (2d) kulinda hadhi, heshima na uhuru wa Mahakama, si kama sisi tunataka kuheshimiwa tu hapa, hili ni takwa la Kikatiba.

Mkakati wa tatu ni; Mahakama na Wadau wa mnyororo wa haki waimarisha mahusiano miongoni mwao kwa lengo la kuchukua hatua haraka ili kutatua changamoto za utoaji haki zitakapojitokeza.

Mwingine ni, Mahakama na Wadau wote watambue nafasi ya kila mmoja, wadumishe heshima, nidhamu ya kazi na wazingatie sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza utendaji kazi wa majukumu ya kila mdau.

Taasisi ambayo ni mdau wa mnyororo wa haki, iimarishe ufuatiliaji mashauri na uwajibikaji kwa kutoa taarifa sahihi na za mara kwa mara kuhusu utekelezaji wa mikakati iliyowekwa na kutumia mifumo inayosomana ili kurahisisha mawasiliano.

Wadau wanaokiuka maadili wachukuliwe hatua ipasavyo kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamiwa na kila mdau husika.

“Mkakati wa saba, Mahakama iongeze na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali (Virtual Court) katika kuendesha mashauri yanayohusu watuhumiwa waliohamishiwa katika Magereza mbalimbali kutoka kwenye Wilaya zisizo na Magereza na ili upatikanaji wa haki uwe wa haraka na wa gharama nafuu.

Mkakati mwingine ni Vikao kuhusu ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa jukumu la utoaji haki mahakamani vifanyike angalau mara nne kwa mwaka ilikujadili changamoto na kufuatilia utekelezaji wa mikakati hiyo. Mkakati wa tisa ni kila Taasisi ambayo ni mdau wa mnyororo wa utoaji haki Mahakamani iweke utaratibu madhubuti wa ndani ya Taasisi utakaofanikisha utekelezaji wa mikakati hiyo.

Aidha, katika Mkutano huo uliofanyika jana uliongezeka mkakati mwingine mpya unaosema kwamba, migogoro yote inayopaswa kwa mujibu wa sheria kutatuliwa kwanza katika ngazi mbalimbali kwa njia ya kimadai au kiutawala ishughulikiwe na kukamilishwa katika hatua na ngazi zote husika badala ya kufunguliwa kama jinai moja kwa moja na hili ni sharti la kisheria.

Jaji Mkuu amesema kwamba, mikakati hiyo ikitekelezwa yatasaidia kuboresha mfumo wa haki jinai na haki itakuwa inapatikana mapema, kwa changamoto ambazo zinatatulika kwa urahisi.

“Huu mkakati wa mwisho pia ni wa kisheria, katika kifungu cha 4 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai ndipo kinapopatikana....., mikakati yote tuliyoiweka ni mikakati ya kisheria ipo kwenye sheria hakuna kitu hapa ambacho hakipo kwenye sheria na ndio maana tunaweka mikakati, kilichopo kwenye sheria lazima kinapaswa kitekelezwa, hatuwezi kuwekewa maazimio kwahiyo kwenye vikao vyetu sisi tumeshakataa maazimio huwezi kuazimia kutekeleza au kutotekeleza sheria, sheria ni lazima uitekeleze vinginevyo utaivunja na ukiivunja unawajibika. Kwahiyo tuna wajibu wa kutekeleza haya yote, tuna wajibu wa kutekeleza hii mikakati ambayo ni ya kisheria, vinginevyo tutawajibika,” ameeleza Mhe. Masaju.

Amesema, kwa mujibu wa Ibara ya 26 ya Katiba inayoweka Utawala wa Sheria, inasema kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii Katiba hii na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara 26(2) inasema kila mtu ana haki kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Sheria kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na Sheria za Nchi.

“Hata mikutano yetu hii, ni katika hatua tunazochukua kuhakikisha kwamba Katiba na Sheria za nchi zinatekelezwa ipasavyo na Ibara ya 25 inatutaka kila mmoja awajibike kwenye hili, na sisi wote tunafanya kazi sasa kwa nafasi mbalimbali, wengine ni Majaji, wengine ni Majaji Wakuu, wengine ni Wakurugenzi, wengine ni Maofisa wa Polisi, wengine Ofisi ya Magereza, wengine Ofisi ya PCCB, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, watumishi wote wa Taasisi zilizowakilishwa hapa tuna majibu tuonafanya kazi hizi,” amesema Jaji Mkuu.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza na Wadau wa Haki Jinai alipokuwa akifunga Mkutano wa Mahakama na Wadau kuhusu ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki mahakamani uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu uliopo Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma tarehe 11 Juni, 2026.


Wadau wa Mahakama wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju alipokuwa akifunga 
 Mkutano wa Mahakama na Wadau kuhusu ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki mahakamani uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu uliopo Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani na Mwenyekiti wa Mkutano wa Mahakama na Wadau kuhusu ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki mahakamani  akizungumza jambo wakati wa mkutano huo uliofanyika tarehe 11 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Baadhi ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania walioshiriki katika 
Mkutano wa Mahakama na Wadau kuhusu ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki mahakamani uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu uliopo Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni