Na DOTTO NKAJA – Mahakama, Geita
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Masjala Ndogo Geita, Mhe. Kevin Mhina, tarehe 11 Juni, 2026, alizindua Jengo la Mahakama ya Mwanzo
Masumbwe baada ya ujenzi wake
kukamilika, hatua inayotarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma
za haki kwa Wananchi
wa Wilaya ya Mbogwe na maeneo jirani.
Uzinduzi
huo ulipokelewa kwa shangwe na Wananchi
wa Masumbwe kutokana na kusogezwa karibu kwa huduma za Mahakama ambazo kwa muda mrefu
zilikuwa zikitolewa katika jengo la Ofisi ya Tarafa.
Hafla
hiyo ilihudhuriwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Shinyanga, Mhe. John
Kahyoza, Jaji wa Mahakama Kuu Geita, Mhe. Griffin Mwakapeje, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya, Watumishi wa Mahakama, Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mbogwe, Viongozi
wa Taasisi mbalimbali pamoja na Wananchi.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Jaji Mhina alimshukuru Jaji Kahyoza kwa kushiriki uzinduzi
huo na kueleza kuwa ushiriki wake unaakisi historia ya usimamizi wa shughuli za
Mahakama katika eneo hilo, ambalo hapo
awali lilikuwa chini ya Wilaya ya Kahama kabla ya kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Geita.
Alisema
kuwa Mahakama ya Mwanzo Masumbwe
ilianzishwa mwaka 1998 wakati eneo hilo likiwa chini ya Wilaya ya Kahama, Mkoa
wa Shinyanga, na imeendelea kutoa huduma za haki licha ya kukosa jengo rasmi
kwa kipindi kirefu.
“Kwa
miaka mingi, Mahakimu
na Watumishi wa Mahakama walifanya kazi
katika mazingira yasiyokuwa rasmi, huku Wananchi
wakipata huduma katika maeneo yenye changamoto za miundombinu. Hata hivyo, hali
hiyo haikuwazuia kutekeleza wajibu wao wa msingi wa kusimamia haki,” alisema
Jaji Mhina.
Alisisitiza kuwa uwekezaji katika
miundombinu ya Mahakama
ni msingi wa kuimarisha amani, utulivu na maendeleo ya Taifa, akieleza kuwa haki ndiyo nguzo
muhimu ya maendeleo ya jamii.
Aidha,
alieleza kuwa ujenzi wa jengo hilo uliwezeshwa kwa kiasi kikubwa na uzalendo wa
aliyekuwa Diwani wa Kata ya Masumbwe, Mhe.
Shimo
Kasheto, ambaye alitoa eneo la ekari mbili kwa ajili ya mradi huo. Pia
aliwapongeza Evarist Gervas na wadau wengine waliochangia hatua za awali za
ujenzi.
Kwa
mujibu wa Jaji Mhina, juhudi za kukamilisha ujenzi ziliongezeka baada ya
kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Geita mwaka 2023, ambapo uongozi wa Mahakama ulianza kutenga sehemu ya
fedha za uendeshaji wa ofisi kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.
Katika
hafla hiyo, pia ulizinduliwa mfumo wa kidijitali wa kuhifadhi taarifa na
majalada ya Mahakama za Mwanzo unaojulikana kama GEITA Repository Database,
ambao sasa umeanza kutumika katika Mahakama zote za Mwanzo zilizopo Kanda ya
Geita.
Jaji
Mhina alisema mfumo huo ulifanyiwa majaribio katika Mahakama ya Mwanzo
Nyankumbu na kuthibitishwa kuwa tayari kwa matumizi rasmi. Alifafanua kuwa
mfumo huo utasaidia kuhifadhi taarifa za mashauri, kuzuia upotevu wa majalada
na kupunguza ucheleweshaji wa mashauri unaotokana na kusubiri kumbukumbu za
mahakama.
Kwa
upande wake, Jaji Kahyoza aliushukuru uongozi wa Mahakama Kuu Geita pamoja na Wananchi wa Masumbwe kwa ushirikiano
uliowezesha kukamilika kwa mradi huo.
Aliahidi
kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Viongozi,
Watumishi wa Mahakama na Wananchi ili kuboresha huduma za Mahakama na kutatua changamoto
zilizopo katika Mahakama za Mwanzo.
Naye
mMakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe
alisema Serikali imefanikisha ujenzi wa
barabara inayofika katika Mahakama
hiyo na kuahidi kusimamia utekelezaji wa mradi wa umeme katika mwaka wa fedha
2026/2027 ili eneo la Mahakama
pamoja na makazi ya jirani yaweze kupata huduma ya umeme.
Alieleza
kuwa upatikanaji wa umeme utarahisisha utoaji wa huduma za Mahakama na kuchochea maendeleo ya Wananchi wa eneo hilo.
Wananchi
waliohudhuria hafla hiyo walieleza kuridhishwa na ubora wa jengo hilo la kisasa
na kuomba Serikali pamoja na Mahakama kuendelea kujenga majengo ya Mahakama yenye gharama nafuu katika
maeneo ya vijijini na maeneo yenye changamoto za miundombinu ili kusogeza
huduma za haki karibu zaidi na Wananchi.
Uzinduzi wa Jengo la Mahakama ya Mwanzo Masumbwe unaonekana kuwa hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa haki, kuboresha mazingira ya kazi kwa Watumishi wa Mahakama na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za ki,ahakama katika Mkoa wa Geita.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, Mhe Kevin Mhina, akikata utepe.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Masjala Ndogo Geita,
Mhe. Kevin Mhina, pamoja
na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Shinyanga, Mhe. John Kahyoza, wakifungua Jiwe la Msingi.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Masjala Ndogo Geita, Mhe. Kevin Mhina, akiutangazia Umma juu ya kuanza
kutumika kwa jengo la Mahakama ya Mwanzo Masumbwe.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Masjala Ndogo Shinyanga,
Mhe.
John Kahyoza, akitoa
shukurani kwa uongozi Mahakama Kuu Geita
na Wananchi wa Masumbwe kwa kushirikiana
kikamilisha mradi
huo.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Geita, Mhe. Fredrick Lukuna, akiwakaribisha wageni katika hafla hiyo.
Wananchi wa Masumbwe wakiongonzwa na
ugeni katika zoezi la kukagua mradi wa jengo hilo.
Picha
ya pamoja katika Jengo la Mahakama ya
Mwanzo Masumbwe, wakatikati ni Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu
Geita, Mhe. Kevin Mhina, wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa MahaKama
Kuu Shinyanga, Mhe. John Kahyoza, wa pili
kulia ni Jaji wa Mahakama kuu
Geita, Mhe. Griffin Mwakapeje.
Picha
ya pamoja katika jengo la Mahakama ya Mwanzo Masumbwe
ngoma ya jadi na wageni katika hafla
hiyo.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni