- Awataka kuwa huru kutoa michango yenye kuboresha mnyororo wa Haki Jinai
- Asema ushirikiano wa wadau kwa Mahakama ni muhimu katika kufikia azma hiyo
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amewataka Wadau wa Haki Jinai nchini kuwa huru na wakweli katika kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali yanayoukabili mnyonyoro wa Haki Jinai.
Mhe. Masaju ameyasema hayo leo tarehe 11 Juni, 2026 alipokuwa akifungua Mkutano wa Mahakama na Wadau kuhusu ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki mahakamani uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu uliopo Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
"Kama changamoto zipo Mahakamani semeni, kama changamoto zipo ili mradi tuwe wakweli sio kusingiziana na tutasema hapa kwa kuheshimiana hatujaja kusutana, tumekuja kushauriana ni wapi kuna tatizo turekebishe na ni wapi tunafanya vizuri kwa hiyo vikao hivi ni vya muhimu," amesema Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu amewaeleza Wadau hao kuwa, wao ni watu muhimu katika kusukuma mbele na kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki Mahakamani.
Mhe. Masaju amesema kuwa, Mahakama itaendeleza utaratibu wa kufanya vikao hivyo na wadau, ambapo amesema jana tarehe 10 Juni, 2026 kulikuwa na mkutano na wadau wa Haki Madai.
"Leo tunafanya mkutano na Wadau wa Haki Jinai, sasa kama mnavyofahamu sisi utaratibu huu tutauendeleza, kumekuwa na tatizo kubwa hata katika mfumo wa haki jinai na jinsi tunavyofanya kazi katika Taifa hili, ndio maana Rais aliunda Tume, moja ya Tume za kwanza kabisa alizoziunda ilikuwa ni Tume ya Haki Jinai iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman ikiwa imesheheni na wajumbe wengine wengi maarufu mpaka Inspekta Jenerali wa Polisi, walikuwepo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwepo na watu wengine maarufu," ameeleza Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju amesema kwamba, uundwaji wa Tume hiyo uliashiria kwamba bado kuna changamoto kubwa katika utekelezaji wa haki jinai katika Taifa. "Na ile Tume ilikuja na mapendekezo na mimi nilivyoteuliwa na Mhe. Rais kuwa Jaji Mkuu siku ananiapisha tarehe 15 Juni, 2025 alinielekeza pamoja na mengineyo kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai, sasa yale sisi hatuwezi kuyatekeleza peke yetu, lazima tuyatekeleze kwa kushirikiana na Wadau wa Mahakama waliopo kwenye mnyororo wa haki jinai,'" amesisitiza.
Kadhalika, Jaji Mkuu ameeleza kuwa, "Mahakamani huwa hatukai peke yetu huwa tunakuwepo sisi Mahakama na watu wenye mashauri Mahakamani, watu wenye mashauri mahakamani wanaweza kuwa ni watu binafsi na Taasisi binafsi, miongoni mwao lakini pia wanaweza kuwa baina ya Taasisi za Serikali na watu na mashirika binafsi."
Kupitia ukweli huo, amesema ndipo unaona nafasi ya kwa mfano Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wakiwakilisha Taasisi za Serikali kwenye mashauri mbalimbali ama wao wenyewe kama Washtaki na Wadai au Washtakiwa na Wadaiwa na ziko na Taasisi nyingine nyingi.
"Kwahiyo ndio maana tunakuwa na utaratibu huu wa kuwashirikisheni ninyi katika shughuli za Mahakama si kwa maana kwamba kwenye masuala ya ushirikishaji wa mashauri, tunashirikisha kwenye hizi shughuli kwa maana kujadili kwa pamoja changamoto zinazotukabili katika utoaji haki na ndio maana tumeanzisha hicho kitu kinachoitwa Haki Jinai," amesema Mhe. Masaju.
Mhe. Masaju ametoa kuwa, uwepo wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wanawakilisha watu wanaoshtakiwa Mahakamani wenye makosa ya jinai lakini na hata wao wenyewe wanapoamua kushtaki mahakamani (private prosecution), lakini Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Katiba na Sheria ambaye naye amehudhuria kikao hicho ni muhimu ili Wizara hiyo ijue ni kitu gani kinaendelea ndani ya Mahakama ili wanaporatibu masuala ya kisera wajue hali ya Mahakama kwa maana ya mafanikio na changamoto zinazoukabili Mhimili huo.
Aidha, Jaji Mkuu amesema, hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiwaapisha Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani, pamoja na mambo mengine alisema Haki ndio Msingi wa Amani.
"Na jana (tarehe 10 Juni, 2026) nilisema haki ni nini, nilisema haki ni uamuzi unaofanywa na Mahakama huru kwa kuzingatia Katiba na Sheria za Nchi hii kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa Mahakamani, hiyo ndio haki. Kwahiyo niwaalike wote kwa dhati tushiriki katika mkutano huu, hapa leo hatuko Mahakamani tupo katika mkutano kwahiyo tuwe wazi, tushauriane," amesisitiza Mhe.
Katika Mkutano huo Mahakama na Wadau wametoa taarifa ya utekelezaji wa mikakati waliojiwekea katika vikao viwili vilivyofanyika nyuma. Kupitia taarifa hizo, kila mdau ataeleza amefanya nini na kubaini maeneo waliyofanikiwa na walipokwama na kuweka mikakati zaidi ya kujikwamua ili kwenda pamoja.
Sehemu ya Viongozi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania waliohudhuria katika Mkutano wa Mkutano wa Mahakama na Wadau kuhusu ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki mahakamani uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu uliopo Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 11 Juni, 2026.
(Picha na MARY GWERA, Mahakama)















Hakuna maoni:
Chapisha Maoni