Alhamisi, 11 Juni 2026

JAJI MKUU ASHAURI KUFANYIKA KWA MAREKEBISHO YA SHERIA ZA MAHAKAMA ZA MAHAKIMU

·       Asema Mahakama imetunga Kanuni kuruhusu matumizi ya Ushahidi wa kieletroniki katika Mahakama za Mwanzo

·       Ahimiza matumizi ya Usuluhishi wa migogoro kwa kufuata mila na desturi za Kitanzania

·       Awataka Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea kujiandaa vema kabla ya kuja Mahakamani

·       Azishauri Wizara za Kisekta kusimamia uboreshaji wa sheria zenye mapungufu ili kuwezesha ufanisi wa utoaji haki

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju ameishauri Serikali na hasa Wizara ya Katiba na Sheria inayohusika na Sheria za Mahakama za Mahakimu (The Magistrate’s Court Act) kufanya mabadiliko ili kuongeza mamlaka ya Mahakama za Mwanzo ya kifedha kwa mashauri yanayofunguliwa katika Mahakama hizo. 

Mhe. Masaju ametoa ushauri huo jana tarehe 10 Juni, 2026 alipokuwa akifunga Mkutano wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

“Tumezungumza hapa juu ya Uchumi wa Kidijitali (Digital Economy), siku hizi miamala mingi inafanyika kwa njia ya mtandao, mikataba inafungwa ya kielektroniki, kuna miamala ya kifedha inafanyika kwa njia ya mtandao na mambo ya aina hiyo, na sisi tunahimiza matumizi ya TEHAMA katika kufanikisha kitu hiki. Na ndio maana pia tumetunga kanuni hivi karibuni tarehe 04 Juni, 2026 za matumizi ya Ushahidi wa kielektroniki katika Mahakama za Mwanzo na ndio maana sasa tunaishauri Serikali na hasa Wizara ya Katiba na Sheria kufanya mabadiliko katika Sheria ya Mahakama za Mahakimu kuongeza mamlaka ya Mahakama za Mwanzo....,” amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amesema, kutokana na ukweli kwamba watu wengi wanatumia simu, imeleta msukumo wa kushauri kuwa matumizi makubwa ya Ushahidi wa kielektroniki. Amesema, “Katika kufanikisha suala hilo ndio maana Mahakama ya Tanzania inahimiza matumizi ya TEHAMA na hivi karibuni tarehe 04 Juni, 2026 tumetunga Kanuni za matumizi ya Ushahidi wa kielekitroniki katika Mahakama za Mwanzo ili kuziwezesha Mahakama hizo ambazo ziko nyingi ziweze kusikiliza mashauri mengi zaidi kuliko kwenda Mahakama ya Wilaya ambayo iko moja tu kila Wilaya.”

Kadhalika, Jaji Mkuu amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, katika jitihada za kutekeleza wajibu wa utoaji haki, kuna mambo mengine ambayo Mahakama inafanya yenyewe na yale ambayo wanaona hayawezi kutekelezwa na Mahakama pekee huwashirikisha wadau kwa njia mbalimbali ikiwemo kupitia vikao.

Aidha, Mhe. Masaju amewajulisha wajumbe wa Mkutano huo kuwa, tarehe 30 Machi, 2026 jumla ya Mahakama za Mwanzo mpya 15 zimefunguliwa na kupeleka huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi kwa kufunguliwa jumla ya Masjala ndogo sita za Mahakama Kuu katika Mikoa ya Singida, Lindi, Njombe, Songwe, Katavi na Simiyu.

“Jitihada hizi ukiziangalia sana zipo katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050, kwa ule msingi mkuu wa Dira na vile vipaumbele vyake vinne vyote vinahusu Utawala wa Sheria na kama Taifa ili tuweze kwenda lazima utawala wa sheria uzingatiwe kwa sababu kila kitu kinatawaliwa na kuongozwa na sheria,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Kadhalika, Mhe. Masaju amesema kuwa, katika kuendelea kuimarisha Utawala wa Sheria, Mahakama imefanya mafunzo kuhusu Sheria za Kiislamu ili Mahakama za Mwanzo ambazo zinahudumia asilimia 70 ya wananchi, Sheria inasema watatumia Sheria za Kimila na Sheria za Kiislamu.

“Na katika viapo vyetu pia (sisi Majaji na Mahakimu), tunaambiwa kuzingatia Katiba, Mila, Desturi na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Jaji Mkuu huku akisisitiza kuwa ni vyema kuzingatia mila na desturi za Tanzania katika utatuzi wa migogoro mbalimbali (ya madai, jinai au migogoro ya ndoa) badala ya kujikita katika mila za Kizungu.

Amesisitiza kuwa ni vyema kutumia na kuenzi mila na desturi za kitanzania kwa kuwa zina sifa ya watu kuishi bila kubaguana, kuzingatia usalama wa jamii, amani katika jamii, umoja wa kitaifa pamoja na kupunguza migogoro.

Mhe. Masaju ameikumbusha Mahakama ya Tanzania kutoa haki ipasavyo bila kufungwa na masharti ya kiufundi kupita kiasi yanayoweza kuzuia haki kutendeka.

“Majaji na Mahakimu niwaombe sana, muwe makini mnapoamua haki za watu kwa mujibu wa ushahidi. Ukishakuwa Jaji au Hakimu lazima uwe tayari kupokea malalamiko, Sisi wajibu wetu ni kutekeleza haki kwa mujibu wa Katiba na Sheria,” amesema Jaji Mkuu.

Aidha, Mhe. Masaju amesema akirejea Ibara ya 26(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inayosema; Kila mtu ana wajibu wa kuifuata na kuitii Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ameongeza kuwa, “Ibara 26(2) inasema kila mtu ana haki kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na Sheria za Nchi’, kwa hiyo tuzifuate sheria kwakuwa zimeweka utaratibu wa kutatua migogoro na huku mahakamani migogoro itapungua lakini gharama zitakuwa nafuu sana kwa wadau wanapoenda kule kutatua migogoro yao kwa kuanzia kule kule kuja Mahakamani moja kwa moja ndio maana tunahimiza hili jambo.”

Mhe. Masaju amesema kwamba, "linapozungumziwa suala la uchumi, unazungumzia matumizi ya ardhi, kwa sababu kwenye ardhi ndipo mazao yanalimwa ni biashara hiyo, kwenye ardhi kuna maji ni biashara, kwenye ardhi kuna madini, kuna petroli ni biashara, uchumi wote siku zote ni ardhi."

Ameeleza kuwa, mashauri ya migogoro ya ardhi yamewekewa utaratibu mzuri kwenye Sheria ya Ardhi (The Land Registration Act) ili kuwezesha migogoro kutatulika kwa ufanisi na kupunguza gharama 

Jaji Mkuu amekitaka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kusaidia kuwashauri Wadaawa badala ya kwenda Mahakamani waanze kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi na ikishindikana ndio waende Mahakamani kama rufaa, hatua hiyo itasaidia kutatua migogoro ya wananchi haraka zaidi.

Sambamba na hilo, Mhe. Masaju amewataka Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea kuja Mahakamani wakiwa wamejiandaa na kuweka sawa nyaraka za mashauri ili kuepukana na uahirishaji wa mashauri usio na sababu za msingi. Na vilevile, amewaonya Mawakili kutoka TLS kusimamia vema nafasi yao na majukumu yao ipasavyo, kuwa imara na kuwajibika ipasavyo kuishauri Serikali badala ya kuwa kama chama cha siasa.

Mhe. Masaju amesema kuwa, hivi karibuni Mahakama itarekebisha Kanuni ya 96(7) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani ambayo inatumiwa vibaya na Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea inafikia mwisho, "Tunafanya mabadiliko ya hizo kanuni, niwashauri kuzingatia umuhimu wa kuwasilisha Mahakamani kumbukumbu za rufaa zilizokamilika kwakuwa imekuwa ni kawaida sasa kuwasilisha mahakama kumbukumbu ambazo hazijatimia aidha kwa uzembe au kukusudia ili kuchelewa kesi.

Jaji Mkuu amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa, Mahakama imepokea pia ushauri wa kurekebisha Kanuni za (Remote proceedings) umepokelewa na watafanya mabadiliko. Ameongeza kwa kuwaomba wadau hao kuwasilisha maoni ya kanuni ambazo zimekaa vibaya au zina changamoto wasisite kusema au hata kwa maandishi ili zifanyiwe marekebisho na kuleta ufanisi.

Katika hatua nyingine, wajumbe wa mkutano huo wameshauri kuwa, zitungwe sheria zinazoziba mianya ya kisheria ya kukwepa kulipa kodi ili kuwezesha Serikali kupata mapato. “Huo ni ushauri mzuri, sisi kesi ikija mahakamani tutaamua kwa mujibu wa sheria zilizopo lakini ukweli ni kwamba kama kuna mianya hii inatengeneza migogoro inakuja huku mahakamani, sisi tunashauri kama sheria za namna hiyo zipo zirekebishwe zizibe mianya ili kuwezesha Serikali kupata mapato lakini itapunguza migogoro,” amesisitiza Mhe. Masaju.

Jaji Mkuu kuboresha sheria, kama zipo ziboreshwe mapema, zile Wizara za Kisekta zinazohusika zichukue hatua mapema na pia kuoanisha sheria zinazogongana ili kuboresha ufanisi wa utoaji haki Mahakamani. Amesema lisipofanyika hilo msingi mkuu wa Dira hautatekelezeka, uchumi hautakua na hata wakiteuliwa Majaji wengi, kiwango cha migogoro kama kinaendelea kuongeza bado shida itakuwa palepale.

Mhe. Masaju ametoa rai kwa watumishi wa Serikali kwa ujumla kujituma na kusimamia utawala wa sheria ipasavyo ili kupunguza migogoro kwakuwa migogoro mingine inakuja kutokana na kukiuka sheria.

"Njia mojawapo ya kupunguza hii migogoro ni watumishi wa Serikali wote tufanye na kutekeleza majukumu yetu kwa kuzingatia Katiba na Sheria za Nchi, ukishazingatia hivyo migogoro inatoka wapi? hakuna jambo katika nchi hii ambalo halisimamiwi na sheria, ukitaka kufunga ndoa kuna sheria, masuala ya ibada yana sheria, ukitaka kuwa Mganga wa Tiba za Asili kuna sheria, ukitaka kuandika habari kuna sheria, ukitaka kilimo, ufugaji uvuvi kuna sheria hakuna jambo la umma ambalo halisimamiwi na sheria. Sasa kama tunafanya kwa namna ya kukiuka sheria tunatengeneza migogoro," ameeleza Jaji Mkuu.

Kwa upande mwingine, Jaji Mkuu ametoa wito kwa Wadau hao kutenga muda wa kuhudhuria vikao hivyo muhimu ambavyo pamoja na mambo mengine vinalenga kuboresha ufanisi wa Mahakama na Sekta ya Sheria kwa ujumla.

“Wananchi wanatutegemea sisi katika ustawi na maendeleo ya Taifa letu, zile Taasisi ambazo zinalegalega tutawaacha nyuma,” amesisitiza Mhe. Masaju.

Katika kikao hicho cha Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji, wajumbe wameweka mkakati mpya unaosema kuwa, ushirikiano unaotolewa katika usikilizwaji wa mashauri ya ardhi, biashara, kodi, mabenki, ushindani wa kibiashara na uwekezaji utolewe pia katika utekelezaji (execution) wa hukumu.

Mikakati mingine iliyowekwa na Wajumbe hao wakati wa mikutano miwili iliyofanyika awali ni pamoja na Mahakama na wadau wa   mnyororo   wa   haki waimarishe mawasiliano na mahusiano miongoni mwao, kwa lengo la kuchukua hatua   za   haraka   pale changamoto   zinazoathiri upatikanaji haki mapema zinapojitokeza.

Mkakati mwingine ni Wadau wa mnyororo wa haki wapatiwe elimu kuhusu sheria, kanuni na taratibu zinazoratibu uendeshaji wa mashauri ya ardhi, biashara, ushindani wa kibiashara, kodi, mabenki na uwekezaji ili kupata uelewa wa pamoja.

Kila taasisi ambayo ni mdau wa mnyororo wa haki Mahakamani iwajibike ipasavyo kutekeleza jukumu lake kwa kuzingatia Katiba, sheria na maadili ya utumishi wa taasisi husika.

Mwingine ni Wadau wote   wa   Mahakama wenye   mashauri  mbele ya Mahakama wanapaswa kuhudhuria na kuyaendesha mashauri yaokikamilifu ili kuwezesha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo. Mahakama haitakuwa tayari kuahirisha shauri isipokuwa kama kutakuwa na sababu za msingi kufanya hivyo mingine mitano.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza na Wadau wa Haki Jinai jana tarehe 10 Juni, 2026 alipokuwa akifunga Mkutano wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria Mkutano wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Sehemu ya Wajumbe wa Mkutano huo wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (aliyesimama mbele) alipokuwa akifunga Mkutano wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.  

Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi akichangia jambo wakati wa Mkutano wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Franklin Rwezimula akichangia jambo wakati wa Mkutano wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.



 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni