Na DOTTO NKAJA – Mahakama, Geita
Viongozi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Katavi, wakiongozwa na Jaji
Mfawidhi, Mhe. Godfrey Isaya, tarehe 9 Juni 2026 walitembelea Masjala Ndogo Geita kwa
lengo la kubadilishana uzoefu katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA).
Viongozi
hao walipokelewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Masjala Ndogo Geita, Mhe. Kevin Mhina, ambaye alimshukuru Mhe. Isaya kwa kuona umuhimu wa kuambatana na Watumishi wa Mahakama hiyo katika
ziara ya mafunzo.
Alisema kuwa Mahakama Geita hufarijika na
kupata hamasa kubwa inapopokea wageni kutoka maeneo mbalimbali, kwani hali hiyo
huchochea ubunifu unaosaidia kurahisisha utoaji wa haki kwa wakati na kwa
gharama nafuu.
Mhe. Mhina alieleza kuwa
ili Taasisi yoyote ifanikiwe kufikia
malengo yake, ni muhimu kuzingatia mambo mawili makuu, ambayo ni kujitoa kwa dhati katika
kutekeleza majukumu ya kazi, na kuwa
na usimamizi madhubuti, ufuatiliaji endelevu pamoja na utoaji wa motisha kwa
watumishi.
Alisisitiza umuhimu wa
mafunzo ya ndani na nje ya Taasisi
kwa lengo la kuongeza uwezo na ufanisi wa watumishi.
Kwa upande wake, Mhe. Isaya
alisema kuwa mafanikio yanayoonekana Geita
yametokana na namna Watumishi
walivyoithamini kazi yao na kujituma katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aliongeza kuwa Mhe. Mhina
ni Kiongozi mwenye uwezo mkubwa wa
kupanga, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za
Mahakama.
“Nawaomba Watumishi wa Mhakama Katavi tujifunze kila
jambo tuliloliona hapa Geita na kuangalia namna Watumishi
wa Geita walivyoamua kufanya kazi kwa kutambua kuwa kazi yao ni wito wa
kuhudumia Mwananchi,”
alisema Mhe. Isaya.
Naye Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu Katavi,
Bi. Silivia Lushasi, aliwashukuru Viongozi na Watumishi wa Geita kwa maandalizi
mazuri ya mafunzo hayo pamoja na uwasilishaji wa mada mbalimbali zilizokuwa na
manufaa makubwa kwa washiriki.
“Kwa kweli nimejionea
jinsi wawasilishaji wa mada walivyo na uelewa mkubwa katika maeneo yao ya kazi.
Hali hiyo imetufanya tukose hata maswali ya kuuliza kwa sababu kila jambo
limeelezwa kwa uwazi na kwa ufasaha mkubwa,” alisema. Aidha, aliahidi kuwa watakwenda
kutekeleza mafunzo hayo mara watakaporejea katika vituo vyao vya kazi.
Katika mafunzo hayo, mada
mbalimbali ziliwasilishwa na wakuu wa vitengo tofauti. Miongoni mwao alikuwa
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Geita, Mhe. Fredrick Lukuna, ambaye aliwasilisha
mada kuhusu matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (E-Case
Management System) na kueleza namna mfumo huo unavyosaidia kukabiliana na
changamoto za usimamizi na ufuatiliaji wa kesi katika ngazi zote za Mahakama.
Pia, Hakimu Mkazi wa
Mahakama ya Wilaya ya Geita, Mhe. Devotha Kasebele, kwa niaba ya Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Mujuni Muchunguzi, aliwasilisha mada
iliyosisitiza kuwa mafanikio ya matumizi ya TEHAMA yanategemea ushirikiano
mzuri kati ya Viongozi
na Watumishi.
Kwa upande mwingine,
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu, Mhe. Ally Mgomba, alieleza
jinsi Mahakama za Mwanzo Geita zilivyofanikiwa kuondokana na matumizi makubwa
ya karatasi kwa kubuni mfumo maalum wa kidijitali unaorahisisha utendaji wa
kazi katika Mahakama.
Mada nyingine
iliwasilishwa na Mtendaji wa Mahakama, Bi. Masalu Kisasila, ambaye alifafanua
matumizi ya TEHAMA katika uendeshaji wa shughuli za kiutawala.
Naye Afisa Mtunza
Kumbukumbu, Bi. Anitha Mwanilunga, alieleza namna dirisha la KIOSK
linavyowasaidia wateja wasio na Mawakili
na wasiojua kusoma kusajili na kufuatilia mashauri yao kwa urahisi.
Aidha, Afisa TEHAMA, Bw.
Dotto Nkaja, aliwasilisha mada kuhusu mfumo wa kuhifadhi taarifa za Mahakama za
Mwanzo, akieleza jinsi mfumo huo unavyosaidia kuondoa changamoto za kuitisha
majalada kutoka Mahakama za chini pindi
yanapohitajika katika Mahakama za juu.
Ziara hiyo imekuwa fursa
muhimu ya kujifunza na kubadilishana uzoefu, huku ikionesha dhamira ya Mahakama
ya Tanzania katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA kwa lengo la kuboresha utoaji
wa haki nchini.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni