- Asema ushirikiano huo una manufaa makubwa kwa Mahakama na kuleta ustawi na maendeleo ya Taifa
- Asema Mahakama haitamvumilia yeyote anayekwamisha upatikanaji haki mapema ipasavyo
- Awataka wadau wa haki madai kuwa huru kuwasilisha changamoto zilizopo ili zitatuliwe na kuwezesha haki kupatikana bila vikwazo
Na
MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amewashukuru wadau
wa Mahakama nchini kwa uwepo wao na ushirikiano wanaotoa kwa Mhimili huo na kukiri
kuwa, umeleta mafanikio makubwa ambayo moja ya manufaa yake ni kuchangia kuleta
ustawi na maendeleo ya Taifa.
Mhe.
Masaju ameyasema hayo leo tarehe 10 Juni, 2026 alipokuwa akifungua Mkutano wa
Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya
Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi na Ushindani wa Kibiashara uliofanyika kwenye
ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
“Tangu
tumeanza vikao hivi vimekuwa na mafanikio makubwa sana, kuwepo kwenu (wadau)
sisi ndio mafanikio ya kusonga mbele. Kaulimbiu ya Mahakama ya mwaka 2026 ni; Mchango
wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa, na hatuwezi kufanya sisi
wenyewe kama hatushirikiani na Taasisi za Umma na Serikali kwa ujumla wetu kama
tulivyo hapa, historia inaonyesha kadri tunavyoshirikiana ndivyo
tunavyofanikiwa,” amesema Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju amesema kuwa, Kaulimbiu hiyo ya Mahakama kwa mwaka huu inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo msingi wake mkuu ni Utawala, Amani, Usalama na Utulivu na vipaumbele vinne ambavyo ni Utawala Bora na Haki, Serikali za Mitaa imara na zenye ufanisi, Utumishi wa Umma unaowajibika na cha nne ni Amani, Usalama na Utulivu.
Amebainisha kuwa, kupitia Dira hiyo ni dhahiri kuwa, Mahakama na Sekta ya Sheria kwa ujumla wana kazi kubwa katika kuleta ustawi na maendeleo ya Taifa.
Jaji Mkuu amewaelewa Wadau hao kuwa wanapotenga muda wao kuja katika vikao na
kushirikiana na Mahakama, ni faraja kubwa kwa Mhimili huo na pia wanawasaidia
wote kwa pamoja kushiriki kuchangia katika ustawi na maendeleo ya Taifa.
Katika
Mkutano huo uliosheheni taarifa mbalimbali za utekelezaji wa mikakati kutoka Mahakama
pamoja na Wadau, Jaji Mkuu aliwasihi wajumbe wa kikao hicho kuwa wakweli na
wawazi kueleza changamoto mbalimbali hata kama zipo Mahakamani ili kupata
ufumbuzi wa changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa majukumu.
Ameongeza
kuwa, lengo la kuzijua changamoto hizo na kuzitafutia ufumbuzi ni kuhakikisha
kuwa, haki inapatikana kwa wananchi mapema ipasavyo kwa mashauri ambayo yapo
mahakamani lakini kuepuka migogoro zaidi.
“Mimi
ningependa Serikali isiwe chanzo cha kutengeza migogoro na mpaka kuwa
inashtakiwa Mahakamani, lakini ningependa pia wananchi wasiwe chanzo cha migogoro,
migogoro inakwamisha maendeleo, inakwamisha na mambo mengine ya ustawi wa Taifa
letu. Kwahiyo niwatakeni wote kwa ujumla wetu tushiriki mkutano huu,” amesema
Mhe. Masaju.
Aidha,
Jaji Mkuu ametoa rai kwa watumishi wa Serikali kwa ujumla kufanya kazi kwa kusimamia
Katiba ya Nchi na misingi iliyowekwa kwa mujibu wa sheria.
Mhe. Masaju amesema kuwa, Mahakama
ya Tanzania haitawavumilia na itawawajibisha watu wanaopuuza uhuru, heshima, mamlaka na hadhi ya Mahakama.
Katika
Mkutano huo wa tatu kufanyika umeongozwa chini ya Mwenyekiti Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani umehudhuriwa na
Wadau mbalimbali wakiwemo baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Wakili
Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Tume ya Taifa ya Mipango.
Wengine ni Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mahakama Kuu-Divisheni ya Biashara, Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Baraza la Ushindani, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na wengine.

















Hakuna maoni:
Chapisha Maoni