·
Zaibuka na Vikombe Vinne
katika Mashindano ya Mei Mosi 2026
Na. JAMES BUSANYA & HALIMA MNETE – Mahakama, Dodoma
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel,
amewapongeza watumishi wa Mahakama walioshiriki kuiwakilisha Taasisi hiyo
katika Mashindano ya Michezo ya Mei Mosi mwaka 2026.
“Nawaagiza ama kutoa maelekezo kwa viongozi wa Mahakama
katika ngazi mbalimbali kuhakikisha wanawapa watumishi muda wa kufanya mazoezi
ili kuendeleza vipaji vyao, kuimarisha afya na kuongeza ushindani wa timu za
Mahakama,” amesema Mtendaji Mkuu.
Prof. Ole Gabriel ametoa maagizo leo tarehe 10 Juni, 2026,
katika hafla ya kupokea rasmi vikombe vinne vya ushindi vilivyotwaliwa na timu
za Mahakama ambazo ni timu ya Karata, Timu ya kamba wanawake, timu ya Baiskeli
na timu ya mchezo wa bao kwenye mashindano ya Mei Mosi mwaka 2026 yaliyoshirikisha
timu 51 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali.
Mashindano hayo yalianza tarehe 13 Aprili, 2026 mkoani
Njombe na kufunguliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Ajira
na Mahusiano, Mhe. Rahma Kisuo na kufungwa rasmi Mei 1, 2026 na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kupokea vikombe na zawadi
za mashindano, Prof. Ole Gabriel amesema anawasilisha salamu za pongezi kutoka
kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju, na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani kwa wanamichezo wote
waliowakilisha Mahakama kwa mafanikio.
“Hayo ni matokeo ya kujituma, nidhamu na mshikamano mkubwa
miongoni mwa wanatimu. Mmeitangaza vyema Mahakama na kutuletea heshima kubwa,”
amesisitiza Mtendaji Mkuu.
Katika mashindano hayo, timu ya wanawake ya Mahakama
ilifanya vizuri kwa kuibuka mshindi wa kwanza katika mchezo wa karata, mshindi
wa pili katika mbio za baiskeli, na kushika nafasi ya tatu katika michezo ya
kamba na bao. Mafanikio hayo yaliifanya Mahakama kuwa miongoni mwa taasisi
zilizofanya vizuri katika mashindano hayo ya kitaifa ya wafanyakazi.
Akitolea ufafanuzi wa taarifa ya Katibu wa Timu ya Michezo
ya Mahakama iliyobainisha changamoto za ukosefu wa muda wa mazoezi na uhaba wa vifaa
vya michezo, Mtendaji Mkuu aliiagiza Idara ya Utawala na Usimamizi wa
Rasilimali Watu (DARHM) kushughulikia changamoto hizo.
“Viongozi wa utawala wanapaswa kuhakikisha wanatoa
ushirikiano unaohitajika kwa wanamichezo wetu. Suala la vifaa vya michezo
litazingatiwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027,” aliongeza Prof. Ole
Gabriel.
Aidha, Prof. Gabriel alieleza kufurahishwa na ushiriki wa
Mahakimu katika timu hiyo, akisisitiza kuwa michezo haina mipaka ya kada wala
cheo. Mahakama ina watumishi takribani 7,000. Hiyo ni hazina kubwa ya vipaji
ambayo vinaweza kutuwezesha kujenga timu imara zitakazoshindana na timu kubwa
nchini kama Simba na Yanga katika miaka ijayo. Mtendaji Mkuu huyo alisisitiza
umuhimu wa nidhamu kwa wanamichezo, akibainisha kuwa wao ni mabalozi wa taasisi
wanayoitumikia na mfano kwa jamii.
Akitoa mfano wa uzoefu wake binafsi, alisema aliwahi kuwa
mchezaji bora wa mpira wa wavu mwaka 1992, jambo linalompa uelewa wa kina
kuhusu mchango wa michezo katika maendeleo ya mtu binafsi na taasisi.
“Michezo huimarisha afya ya mwili na akili, hujenga
mahusiano ya kijamii na ustawi wa kiroho, na huongeza mshikamano mahali pa kazi
kwa kuwaondoa watumishi katika mipaka ya vyeo na kada wanapokuwa uwanjani. Aliongeza
kuwa Serikali hii chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuhimiza
ushiriki wa michezo kama sehemu muhimu ya maendeleo ya afya na ustawi wa
wananchi,” amebainisha Prof. Ole Gabriel.
Vilevile, Prof. Ole Gabriel aliwashukuru viongozi na
wasaidizi wake akiwemo Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu
pamoja na Mkurugenzi wa Mipango na Uratibu, kwa mchango wao wa kusaidia timu. Uongozi
utaendelea kutoa ushirikiano na msaada unaohitajika ili kuimarisha maendeleo ya
michezo. Akawahimiza watumishi kuifanya michezo kuwa sehemu ya maisha yao ya
kila siku na si kwa ajili ya mashindano pekee.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa makabidhiano rasmi ya vikombe
vya ushindi na pongezi kwa wanamichezo walioiwakilisha Mahakama kwa mafanikio
katika Mashindano ya Mei Mosi ya mwaka 2026.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza wakati wa kuwapongeza watumishi wa Mahakama walioshiriki kuiwakilisha Taasisi katika Mashindano ya Michezo ya Mei Mosi mwaka 2026 yaliyofanyika mkoani Njombe leo tarehe 10 Juni, 2026 katika ukumbi wa mikutano ndani ya Jengo la Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni