JAJI MAHAKAMA YA RUFANI TANZANIA AUNGANA NA WATANZANIA WENGINE KWENYE MAADHIMISHO GENEVA
Na FASUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha
Jaji wa Mahakama ya
Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina, jana tarehe 9 Juni, 2026 aliungana
na Watanzania wengine wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Geneva, nchini Uswisi
kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Mtoto.
Maadhimisho hayo
yalifanyika katika Makao Makuu hayo ya Umoja wa Mataifa, huku , ujumbe huo wa
Tanzania uongozwa na Kamishna wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa, ambaye aliambatana na
Kamishna wa Kazi Zanzibar, Bw. Rashid Khamis Othman.
Walikuwepo pia Wakuu wa
Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano,
Wataalamu na Wawakilishi wa Waajiri (ATE) pamoja na Wawakilishi kutoka
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA).
Akizungumza wakati wa
hafla ya ufunguzi wa Maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kazi
Duniani (ILO), Bw. Gilbert Houngbo, alitoa wito kwa jamii ya Kimataifa na Wadau
wa Utatu kutekeleza kwa vitendo Mipango na Maazimio ya Mkutano wa Marrakesh
uliofanyika nchini Morocco, Februari 2026 kwa lengo la kupinga utumikishwaji wa
Mtoto.
Vilevile, alisisitiza juu
ya jitihada za makusudi zinazotakiwa kuchukuliwa na nchi wanachama wa Shirika la
Kazi Duniani (ILO), katika kukuza kazi za staha na utekelezaji wa sera ya elimu
bure.
Kwa upande wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu
Hassan, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, imeendelea
kudhihirisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya kazi na ajira.
Serikali imechukua hatua
madhubuti kutokomeza ajira za watoto nchini kwa kutekeleza Mradi wa pamoja kati
ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Brazil, kwa kushirikiana na ILO mradi
huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kuhusu utumikishwaji wa mtoto na
madhara yake.
Pia, kuhuishwa kwa
Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Utumikishwaji wa Mtoto 2024/25–2028/29,
unaolenga kuunganisha nguvu za wadau wote wa maendeleo, mashirika ya kiraia na
jamii kwa ujumla.
Kadhalika, Serikali
imeendelea kuimarisha mifumo ya Haki Kazini kupitia Mahakama Kuu, Divisheni ya
Kazi, na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA). Vyombo hivi vimekuwa vikitimiza
vyema wajibu wake wa kutafsiri sheria na kutoa haki, hususani ulinzi kwa mtoto;
na kuadhimisha Siku ya Kupinga Utumikishwaji wa Mtoto Kitaifa kila tarehe 12
Juni.
Wadau kutoka Tanzania
Bara na Zanzibar hushiriki na kupokea mikakati ya Serikali ya kukabiliana na
tatizo hili; pamoja na kutoa elimu kwa Umma kwa kuwa utumikishwaji wa mtoto ni
jukumu la jamii nzima.
Siku ya Kupinga Utumikishwaji wa Mtoto huadhimishwa kila mwaka tarehe 12 Juni na Shirika la Kazi Duniani (ILO) pamoja na nchi wanachama, kwa lengo la kuhamasisha nguvu ya pamoja baina ya Serikali, Vyama vya Waajiri, na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi katika kukuza ajira zenye staha na kutokomeza utumikishwaji wa watoto unaowanyima fursa za kijamii, hususan haki ya elimu.
Maadhimisho hayo kwa mwaka huu 2026 yaliongozwa na Kaulimbiu isemayo: “Red Card to Child Labour” ikimaanisha wito kwa wadau wote wa maendeleo kutoonesha uvumilivu wowote kwa vitendo vinavyochochea au kusababisha utumikishwaji wa mtoto katika sekta zote za kijamii na kiuchumi.
Jaji wa Mahakama ya
Rufani, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina (kushoto) Kamishna wa Kazi, kutoka
Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Bi. Suzan Mkangwa (kulia) na
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda (katikati) wakifuatilia hotuba ya
Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Bw. Gilbert Houngbo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya
Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Mtoto yaliyofanyika katika Ukumbi wa
Tempus, Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, tarehe 9 Juni, 2026, Geneva, Uswizi.
Jaji wa Mahakama ya
Rufani, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina (kushoto) Kamishna wa Kazi, kutoka
Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Bi. Suzan Mkangwa (kulia) na
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda (katikati) wakifuatilia hotuba ya
Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Bw. Gilbert Houngbo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya
Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Mtoto yaliyofanyika katika Ukumbi wa
Tempus, Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, tarehe 9 Juni, 2026, Geneva, Uswizi.
Mkurugenzi Mkuu wa ILO,
Bw. Gilbert Houngbo akihutubia wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya
Kupinga Utumikishwaji wa Mtoto yaliyofanyika katika Ukumbi wa Tempus, Makao
Makuu ya Umoja wa Mataifa, tarehe 9 Juni, 2026, Geneva, Uswizi.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni