Na MUSSA MWINJUMA -Mahakama Kuu Tanga
Jaji Mfawidhi zamani wa
Mahakama Kuu Masjala Ndogo Tanga, Mhe. Katarina Mteule, jana tarehe 9 Juni, 2026,
aliagwa na Watumishi wa Mahakama na Wadau baada ya kupata uhamisho kwenda
Mtwara kuendelea na wadhifa huo.
Hafla hiyo fupi
ilifanyika ndani ya ukumbi wa wazi wa Mahakama Kuu Tanga. Mhe Mteule amehudumu
Tanga kwa muda wa miaka mitatu. Nafasi yake imechukuliwa na Jaji Mfawidhi mpya,
Mhe. Abdallah Gonzi.
Wakati wa hafla hiyo,
Jaji wa Mahakama Kuu Tanga, Mhe. Messe Chaba alisoma risala ya kumuaga Jaji
Mteule kwa niaba ya watumishi wote na kumshukuru
kwa mchango wake mkubwa katika utoaji haki.
“Tunakushukuru kwa kuimarisha kasi ya usikilizaji
wa mashauri pamoja na matumizi ya TEHAMA na kuweka msukumo mkubwa kwenye haki
jinai na madai, uwepo wa Wadau kama Polisi, TAKUKURU, Uhamiaji, Magereza na
wengine katika hafla hii inaonesha mahusiano bora na madhubuti yaliyopo baina
yetu,” alisema Mhe. Chaba.
Akimkaribisha Jaji Gonz,i
Mhe. Chaba alisema, “Tunakukaribisha sio kama mgeni bali, kama sehemu ya timu
ya Mahakama Tanga na tunasonga mbele, tunaamini uzoefu, maarifa na utaalamu
wako katika masuala ya sheria utaleta tija.”
Aliwaasa Watumishi kuwa
na nidhamu, bidii na mshikamano wa kweli katika utendaji kazi ili kufikia
malengo ambayo Taasisi inayatarajia.
Kwa upande wake, Mhe. Mteule
alimpongeza Jaji Gonzi kwa uteuzi na kuwashukuru Watumishi na Wadau kwa
ushirikiano waliompatia katika kipindi chote alichohudumu kama Jaji Mfawidhi.
“Mlinivumilia pale
nilipokosea na kunishauri pale ilipohitajika, kwakweli namshukuru Mungu kwa
kila jambo. Wakati mwingine kukaa sehemu moja kwa muda mrefu inaweza kusababisha
kukosa ubunifu, hivyo kwangu jambo hili ni jema kwakua nakwenda kupata
changamoto mpya,” alisema.
“Mhe. Gonzi, nakukabidhi Wadau
hawa, ushirikiano wao na Mahakama ni dhabiti na imara kwelikweli, nakosa neno
la kusema juu yao, ni matumaini yangu ushirikiano huu utaimarika zaidi,”
alisisitza Jaji Mteule.
Naye Mhe. Gonzi,
akizungumza kwenye hafla hiyo, alisisitiza juu ya utendaji kazi kwa kufuata
misingi na taratibu za kazi. Alikemea vikali masuala ya uzembe na kutowajibika
kazini.
“Mahakama Kuu Tanga ni
sehemu ya Mahakama Kuu ya Tanzania, sasa haiwezekani wengine wanakimbia, sisi
tunatembea, maana yake tutakuwa tunadumaza juhudi za wenzetu kwa kuwashika
shati. Binafsi siwezi kuvumilia uzembe, lazima tufanye kazi kwa bidii ili
tusonge mbele kwa pamoja, ” alisema Jaji Gonzi.
Alisisitiza pia juu ya kuzingatiwa kwa haki na maslahi ya Watumishi na uwajibikaji wa kila mtu katika eneo lake la kazi.
Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu, Mhe. Hudi Majid Hudi akiongoza hafla ya kumuaga Jaji Katarina Mteule anayehamia
Mahakama Kuu Mtwara.
Jaji Abdallah Gonzi (kushoto),
Jaji Katarina Mteule na kulia ni Jaji Messe
Chaba wakiwa katika hafla ya kumuaga Jaji Katarina Mteule anayehamia
Mahakama Kuu Mtwara.
Jaji Mese Chaba akisoma
risala ya kumuaga Jaji Katarina Mteule kwa niaba ya Watumishi.
Jaji Katarina Mteule akiwaaga
Watumishi katika hafla ya kumuaga.
Jaji Abdallah Gonzi akitoa
neno la shukrani katika hafla hiyo.
Jaji Messe Chaba
akikabidhi zawadi kwa Jaji Katarina Mteule kwa niaba ya Watumishi. Anayeangalia
ni Jaji Gonzi.
Watumishi na Wadau
mbalimbali waliohudhuria katika hafla hiyo.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni