Na EVA LESHANGE, Mahakama-Singida
Jaji
Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Singida, Mhe. Ayoub Mwenda amewasisitiza
Wajumbe wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Singida kuzingatia
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ikiwa ni jitihada za
kupunguza matumizi ya karatasi.
Akifungua
mkutano wa Chama hicho hivi karibuni uliofanyika kwenye ukumbi wa
Mikutano wa Mahakama Kuu Singida, Mhe. Mwenda alisema, “nasisitiza kuendelea
kutumia TEHAMA kwenye shughuli zetu za kila siku ikiwemo kusikiliza mashauri, maandalizi
ya nakala za hukumu, mienendo ya kesi na shughuli nyingine.”
Vilevile,
aliwaeleza wajumbe kuwa, jumla ya watumishi 25 wa kada mbalimbali kutoka
Mahakama Kuu hadi Mahakama za Mwanzo Singida, walikwenda Mahakama Kuu Masjala
Ndogo ya Geita kujifunza kuhusu matumizi ya TEHAMA katika shughuli mbalimbali
za kimahakama na kwamba, zoezi hilo ni endelevu na linaenda sambamba na ununuzi
wa vifaa vyenye uwezo kwa kushirikiana na Menejimenti.
Amesema,
hatua hiyo ni katika kuhakikisha matumizi ya karatasi yanapungua kwa kiasi
kikubwa ili kuendana na kasi ya teknolojia.
Aidha,
katika kikao hicho aliwasisitiza wajumbe hao wa TMJA kufanya kazi kwa
ushirikiano na watumishi wa kada nyingine ili kufikia malengo ya Taasisi.
Kadhalika,
Jaji Mfawidhi huyo amewasisitiza Mahakimu wafawidhi wa Wilaya kusimamia
watumishi walio chini yao ili kuendelea kuwa na nidhamu nzuri kazini na hata
nje ya mazingira ya kazi.
Akihitimisha mkutano huo, Mhe. Mwenda amewasisitiza Mahakimu kuviishi viapo vyao vya kazi na kuwajibika ipasavyo kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni na taratibu na kuendelea kusimamia maelekezo yote yanayotolewa na viongozi pasipo kuogopa kukosolewa kwani kiongozi mzuri ni yule ambaye anakubali kukosolewa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Singida, Mhe. Ayoub Mwenda (aliyesimama) akizungumza na wajumbe (hawapo katika picha) katika ufunguzi wa Mkutano wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Singida. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Singida, Mhe. Nenelwa Mwihambi na kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida, Mhe. Evodia Kyaruzi.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni