Ijumaa, 26 Juni 2026

JAJI MTULYA AKUTANA NA KUFANYA KIKAO NA MADALALI, WASAMBAZA NYARAKA

Na. MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya, jana tarehe 25 Juni, 2026 amefanya kikao na Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya, kwa lengo la kukumbushana majukumu yao ya kila siku, kubaini changamoto zinazowakabili na kujadili mapendekezo ya namna ya kuboresha utendaji kazi ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wananchi kwa wakati mapema ipasavyo.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhe. Mtulya aliwataka Madalali kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao huku wakizingatia kikamilifu taratibu, sheria na kanuni zinazoongoza kazi zao.

Mhe. Mtulya alisisitiza kuwa, utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia misingi ya taaluma na maadili utasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za Mahakama.

Aidha, Mhe. Mtulya alieleza kwamba, ni muhimu kwa kila mdau kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa mipaka ya mamlaka aliyopewa, akibainisha kuwa Mawakili wanapaswa kuheshimu majukumu ya Madalali na kuepuka kuingilia utekelezaji wa kazi zinazowahusu Madalali na wasambaza nyaraka za Mahakama ili kuimarisha uwajibikaji na ufanisi katika mfumo wa utoaji haki.

Kwa upande wake, Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Judith Lyimo aliwashauri Madalali kufanya vikao vya ndani kwa lengo la kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao na kuziwasilisha rasmi katika Ofisi ya Naibu Msajili ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati na kwa utaratibu unaostahili.

Nao, Madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama, walieleza kuwa moja ya changamoto kubwa wanazokutana nazo ni uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi pamoja na viongozi wa Serikali za Mitaa kuhusu nafasi, umuhimu na majukumu ya Madalali wa Mahakama. walisema kuwa, hali hiyo wakati mwingine husababisha ugumu katika utekelezaji wa majukumu yao na kuchelewesha baadhi ya hatua za utekelezaji wa amri za Mahakama.

Akijibu hoja hiyo, Mhe. Mtulya alisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wadau mbalimbali katika vikao vijavyo, ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ili kusaidia kutoa elimu kwa viongozi wa Serikali za Mitaa, Halmashauri na Manispaa kuhusu nafasi na umuhimu wa Madalali katika kusaidia Mahakama kutekeleza majukumu yake ya utoaji haki kwa wananchi.

Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za Mahakama za kuendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wake muhimu, kuboresha mazingira ya utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za haki kwa wananchi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe, Fahamu Mtulya (kushoto) akiongoza kikao cha Madalali Mbeya, kulia ni Naibu Msajili Mahakama kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Judith Timoth Lyimo.

Sehemu ya washiriki katika kikao hicho wakimfuatilia kwa makini Mwenyekiti wa kikao hicho Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe, Fahamu Mtulya Mhe. Fahamu Mtulya (hayupo pichani)

Sehemu ya washiriki katika kikao hicho wakimfuatilia kwa makini Mwenyekiti wa kikao hicho Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe, Fahamu Mtulya Mhe. Fahamu Mtulya (hayupo pichani)

Mmoja wa Madalali wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mbeya akichangia jambo katika kikao hicho.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni