Ijumaa, 26 Juni 2026

JAJI MTULYA AONGOZA KIKAO CHA KUSUKUMA MASHAURI YA JINAI

Na. MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania, Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya, ameongoza kikao cha usimamizi wa mwenendo wa mashauri ya jinai (Case Flow Management) kilichofanyika tarehe 25 Juni 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Mbeya kwa lengo la kujadili mwenendo wa mashauri ya jinai na hali ya upatikanaji wa haki jinai.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Mussa Pomo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Judith Lyimo, Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mhe. Zawadi Laizer, Mahakimu pamoja na wadau mbalimbali wa haki jinai.

Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni mustakabali wa mashauri ya jinai ya mlundikano na yanayotarajiwa kuingia kwenye mstari wa mlundikano ifikapo Disemba, 2026, ambapo mikakati iliwekwa ili kuhakikisha kuwa mashauri hayo yanamalizika hadi ifikapo Novemba 2026.

Aidha, kikao hicho pia kilipitia kwa pamoja utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita, ikiwemo uteketezaji wa vielelezo vya madawa ya kulevya ambao ulitekelezwa tangu mwezi Mei, 2026 ikiwa ni katika mikakati ya kupunguza mlundikano wa vielelezo mahakamani.

Vilevile, Mhe. Mtulya aliielekeza Ofisi ya Mwendesha Mashtaka (NPS) kupitia majalada ya mashauri 26 yanayotarajiwa kuwa ya mlundikano ifikapo mwezi Disemba, 2026 ili kuandaa vikao maalum vitakavyosaidia kuharakisha usikilizwaji wa mashauri hayo.

Naye, Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer alisisitiza ushirikiano wa taasisi zote za haki jinai katika kutekeleza majukumu yao kwa wakati.

Kwa upande wake, Naibu Msajili Mahakama Kuu masjala ndogo ya Mbeya Mhe. Judith Lyimo aliiomba taasisi ya Magereza kuwasaidia wafungwa kusajili mashauri yao kwa wakati.

Nao, Magereza walipendekeza wafungwa walio tayari kukiri makosa yao wasikilizwe mapema ili kurahisisha mwenendo wa mashauri, huku Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashitaka (NPS) wakiahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa katika kikao hicho.

Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za wadau wa haki jinai Masjala Ndogo ya Mbeya za kuimarisha usimamizi wa mashauri na kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati mapema ipasavyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akizungumza katika kikao hicho, kulia ni Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer na kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Mussa Pomo.

Sehemu ya washiriki wa kikao hicho wakimfuatilia kwa makini Mwenyekiti wa kikao hicho Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya Mhe. Fahamu Mtulya (hayupo pichani).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (wa pili kulia), Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Mussa Pomo (wa pili kushoto), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Judith Lyimo (wa kwanza kushoto) na Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mhe. Zawadi Laizer (wa kwanza kulia) wakiwa wanaendesha kikao cha kusukuma mashauri ya jinai.

Sehemu ya washiriki wa kikao hicho wakimfuatilia kwa makini Mwenyekiti wa kikao hicho Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya Mhe. Fahamu Mtulya (hayupo pichani).

Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer akiwasilisha taarifa katika kikao hicho, kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya.


Mmoja wa washiriki wa kikao cha kusukuma mashauri ya jinai akichangia jambo katika kikao hicho.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni