Ijumaa, 26 Juni 2026

WADAU WA HAKI JINAI KIGOMA WAKUTANA KUJADILI MWENENDO WA MASHAURI YA JINAI

  • Wafanya Tathmini ya mwenendo wa Mashauri ya Jinai

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, leo tarehe 26 Juni, 2026 imefanya Kikao cha Kusukuma Mashauri ya Jinai kilichoongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa kikilenga kutathmini na kuimarisha usimamizi na ufanisi wa utoaji haki kwa wananchi mapema ipasavyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mbelwa amebainisha kuwa, kikao  hicho kinajikita katika mikakati ya kuhakikisha mashauri ya jinai kwa ngazi ya Mahakama Kuu yanasikilizwa haraka ili kuepuka mashauri ya mlundikano huku zikiendelea juhudi za kuhimiza wadau kila mmoja kutimiza wajibu wake katika mnyororo wa haki jinai ili kuisaidia Mahakama kutekeleza jukumu lake la msingi haraka iwezekanavyo.

“Tunafahamu zipo changamoto ndogo za kujadili hasa katika eneo la stakabadhi za wafungwa kupelekwa Mahakama husika, nakala za hukumu na mienendo kutofika kwa wafungwa, mahabusu, inapotolewa na Mahakama husika, Mahakama hatupaswi kudaiwa nyaraka hizo kwani zinatolewa kwa wakati, ni rai yetu ninyi Wadau kuhakikisha mnatenda wajibu wenu mapema ili kuondoa hoja mbalimbali,” amesema Naibu Msajili huyo

Aidha, ametoa rai kwa wadau wote wa haki jinai kutoa kipaumbele zaidi katika mashauri ya watoto na yale ya ukatili wa kijinsia, ili kutoa haki kwa walengwa bila kuchelewa, kuleta nafuu kwa wahanga wa mashauri hayo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Tawi la Kigoma, Bw. Eliutha Kivyiro, amesema idadi ya Mawakili mkoani Kigoma haitoshi ukilinganisha na uhitaji wa wananchi katika uwakilishi wa Wakili Mahakama zote Kigoma, ameendelea kubainisha kuwa uhitaji wa Mawakili ni mkubwa ukilinganisha na idadi ya mashauri yaliyopo mkoani humo.

Wakili huyo ameliomba jukwaa hilo la haki jinai Mkoa wa Kigoma kusaidia ongezeko la Mawakili ili kutoa huduma ya sheria na uwakilishi mzuri wa wananchi Mahakamani kwa wakati, hatua hiyo itaiwezesha Mahakama kumaliza mashauri mapema ipasavyo, kwani zipo Wilaya tatu za Uvinza, Kakonko na Buhigwe ambazo hazina Mawakili. 

“Katika kuboresha mnyororo wa haki ni rai yetu Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) mkoani Kigoma tunao upungufu mkubwa ambao unaweza kuleta changamoto kwa Mawakili na Mahakama katika mnyororo wa haki katika upangaji wa mashauri katika ngazi zote za Mahakama, hivyo ni vema jukwaa hili kufahamu na kuona ambavyo tunaweza kutatua changamoto hii, ili wananchi wetu wa Kigoma wapate haki mapema ipasavyo,” amesema Bw. Kivyiro.

Kikao hicho cha Wadau wa Haki Jinai Kigoma kilihudhuriwa na wajumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Magereza, Polisi, Ofisi ya Upelelezi Mkoa, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Ustawi wa Jamii, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Idara ya Marekebisho ya Tabia, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa na Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Kigoma.

Sehemu ya Wajumbe wa Kikao cha Wadau wa Kusukumu Mashauri ya Haki Jinai Kigoma wakifuatilia kwa makini maelekezo ya Mwenyekiti wa kikao hicho (hayupo katika picha) leo tarehe 26 Juni, 2026.

 Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo  ya Kigoma,  Mhe. Fadhili Mbelwa akitoa maelekezo kadhaa kwa wajumbe  wakati wa Kikao cha Wajumbe wa Kusukuma Mashauri ya Jinai kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Kigoma.

 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo akifuatilia kwa makini moja ya taarifa iliyokuwa ikitolewa na mmoja  kati ya Wajumbe wa kikao hicho.

Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Wakili Michael Sallo akitoa  taarifa ya ofisi hiyo katika Kikao cha Wadau wa Mashauri ya Jinai Mahakama Kuu Kigoma.

 Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Kanda ya Kigoma, Bw. Eliutha Kivyiro akitoa taarifa ya chama hicho katika kikao cha Wadau wa Kusukuma Mashauri ya Jinai Mahakama Kigoma.


(Habari imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni