Na. MUKSINI NAKUVAMBA- Mahakama, Mbeya
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Joachim Charles Tiganga,
amezindua rasmi Mpango wa Malezi ya Kitaaluma kwa Mahakimu (Mentorship Program)
hivi karibuni. Mpango huo unalenga kuimarisha utendaji kazi wa Mahakimu na
kuongeza imani ya wananchi kwa Mahakama pamoja na huduma zinazotolewa
mahakamani.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi huo, Mhe. Tiganga alisema kuwa, mpango huo umeanzishwa kwa lengo la
kuwajengea Mahakimu uwezo zaidi wa kiutendaji kupitia ushauri, mwongozo na
malezi kutoka kwa viongozi na watendaji wenye uzoefu mkubwa katika tasnia ya
sheria na utoaji wa haki.
“Ukimpata mtu wa
kukwambia madhaifu yako, huyo anakujenga. Utafakari ushauri huo na kuufanyia
kazi akisisitiza umuhimu wa kupokea ushauri kwa lengo la kujiboresha kitaaluma
na kiutendaji,” alisema Mhe. Tiganga.
Aidha, Mhe. Tiganga
aliongeza kuwa Mahakama inatarajia mpango huo kuzalisha viongozi bora wenye
uwezo wa kuongoza, kukua binafsi na kuwainua wengine katika taaluma yao.
“Tunatarajia kuwa, baada
ya kumalizika kwa programu hii, tutakuwa na viongozi wazuri wanaotambua vyema
dhana ya uongozi, kukua na kukuza wengine kitaaluma na kiutendaji,” alisisitiza
Mhe. Tiganga.
Kwa upande wao, baadhi ya
Mahakimu walioshiriki katika uzinduzi wa Mpango huo wamepongeza hatua hiyo,
wakieleza kuwa mpango huo utakuwa chachu ya kuboresha utendaji kazi wao na
kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kimahakama.
“Tumelipokea jambo hili
kwa mikono miwili na tunaamini kuwa litatunufaisha sana sisi Mahakimu na
kuboresha utendaji kazi wetu. Tunatarajia kujifunza zaidi na kufikia viwango
vya juu zaidi vya utendaji kazi katika vituo vyetu vya kazi,” alisema Hakimu
Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Paul Ntumo.
Uzinduzi huo, ulihusisha
Mahakimu kutoka maeneo mbalimbali, ambapo sehemu yao walishiriki kupitia mfumo
wa mkutano mtandao (video conference), jambo lililowezesha ushiriki mpana wa
watumishi wa Mahakama ndani ya Masjala Ndogo ya Mbeya.
Mpango wa Malezi ya
Kitaaluma kwa Mahakimu unatarajiwa kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha uwezo
wa watumishi wa Mahakama, kuongeza ubora wa utoaji wa haki na kuendeleza
dhamira ya Mahakama ya Tanzania ya kutoa huduma bora kwa wananchi kwa wakati na
kwa ufanisi.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga (Katikati) akiongoza uzinduzi huo, kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Angaza Mwipopo, na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Mussa Pomo (kulia).
Sehemu ya
Mahakimu walioshiriki katika kikao cha uzinduzi huo.
Sehemu ya
Mahakimu walioshiriki katika uzinduzi huo kwa njia ya Mtandao (Video conference).
Naibu Msajili
Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Judith Lyimo (wa kwanza kushoto),
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mhe. Zawadi Laizer
(katikati), Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Mbeya, Mhe. Tedy Mlimba
(kulia) wakifuatilia kwa karibu kikao cha uzinduzi wa program ya Malezi
kitaaluma.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni