Na DOTTO NKAJA, Mahakama - Geita
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu, Masjala Ndogo ya Geita, Mhe. Projestus Kahyoza, Julai 28, 2026, amekutana
na kufanya mazungumzo na Mawakili wa Serikali na wa kujitegemea mkoani Geita katika
kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mafunzo wa Mahakama Kuu Geita kwa lengo
la kujengeana uwezo na kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa haki.
Akifungua kikao hicho,
Mhe. Kahyoza aliwashukuru mawakili kwa kuitikia wito na kueleza kuwa mkutano huo
ulilenga kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama na wadau wa sheria,
kujadiliana masuala yanayohusu utoaji wa haki, kubadilishana uzoefu kuhusu
matumizi ya mifumo ya Mahakama pamoja na kufahamiana, kwa kuwa yeye ni mgeni
katika Masjala Ndogo ya Geita.
Alisema uwepo wa wadau
wengi wa sheria mkoani Geita ni fursa muhimu ya kuendeleza utoaji wa haki kwa
ufanisi na kuongeza kuwa Mahakama ya Geita imeendelea kuwa mstari wa mbele
katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha
utoaji wa huduma za Mahakama.
Mhe. Kahyoza alisisitiza
umuhimu wa mifumo mbalimbali ya TEHAMA kusomana na kufanya kazi kwa pamoja ili
kuongeza ufanisi na kuboresha huduma kwa watumiaji. Aidha, aliwahimiza mawakili
kuanza kutumia Kiapo cha Ushahidi (Witness Statement), hususan katika mashauri
ya madai, akieleza kuwa utaratibu huo unasaidia kuharakisha usikilizaji na
utoaji wa maamuzi ya mashauri.
Pia aliwataka mawakili
kuendelea kutoa taarifa na mapendekezo wanapokutana na changamoto katika
matumizi ya mifumo ya Mahakama ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati.
Kwa upande wake na kwa
niaba ya mawakili, Wakili Marina Mashimba aliipongeza Mahakama ya Geita kwa maboresho
ya mifumo ya kidijiti ambayo imepunguza gharama na muda wa uwasilishaji wa
mashauri. Alipendekeza pia kuimarishwa kwa ushirikiano wa mifumo ya Mahakama na
taasisi nyingine za utoaji wa haki, ikiwemo Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA)
pamoja na Mabaraza ya Ardhi.
Aidha, aliomba mafunzo ya
mara kwa mara kwa mawakili ili kuwaongezea uwezo wa kitaaluma na kuwawezesha
kupata alama za maendeleo endelevu ya taaluma kupitia chama chao cha kitaaluma.
Naye, Wakili George
Alfred aliipongeza Mahakama kwa maboresho ya huduma, huku akiainisha baadhi ya
changamoto zinazojitokeza katika matumizi ya mfumo wa kielektroniki. Alieleza
kuwa, baadhi ya kampuni hazionekani wakati wa usajili wa mashauri, baadhi ya
vijiji havipo kwenye mfumo, na wakati mwingine mfumo humtambua wakili
anayesajili shauri kama mlalamikaji badala ya mwakilishi wa mlalamikaji.
Alisisitiza umuhimu wa kuwawezesha mawakili kutumia kikamilifu mifumo ya
kielektroniki ili kupunguza matumizi ya karatasi na kuongeza ufanisi.
Akijibu hoja hizo, Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Geita, Mhe. Fredrick
Lukuna, alisema changamoto zote zilizowasilishwa zimepokelewa na zitafanyiwa
kazi. Alieleza kuwa, changamoto zinazohusu mashauri ya mirathi, nyaraka
kutokuonekana kwenye mfumo pamoja na usajili wa kampuni zitawasilishwa kwa
wajenzi wa mfumo ili zipatiwe ufumbuzi.
Akihitimisha kikao hicho,
Mhe. Kahyoza aliwashukuru mawakili kwa ushiriki wao na maoni yao yaliyolenga
kuboresha huduma za Mahakama. Aliwahimiza kuendelea kutoa taarifa kuhusu
changamoto wanazokutana nazo, kuimarisha ushirikiano na Mahakama, pamoja na
kutumia huduma za usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao ili kuongeza
ufanisi katika utoaji wa haki.
Aidha, aliwakumbusha
mawakili umuhimu wa kufanya mazoezi na kushiriki michezo mbalimbali ili
kuimarisha afya ya mwili na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya
kila siku.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Geita, Mhe. Projestus Kahyoza (katikati mbele) akiwakaribisha
Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Kujitegemea katika kikao kazi hicho cha
kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji.
Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Geita, Mhe. Fredrick Lukuna akijibu maswali na
hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Mawakili katika kikao kazi hicho.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Geita Bi. Masalu Kisasila aliyesimama akitoa shukurani kwa ushirikiano mzuri katika uendeshaji wa shughuli za kiutawala baina ya Mawakili na Uongozi wa Mahakama.
.png)

.png)
.png)

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni