Ijumaa, 31 Julai 2026

JAJI KIONGOZI AONGOZA WAOMBOLEZAJI IBADA YA MAZISHI YA KUMUAGA JAJI MSTAAFU SAMBO

Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani amewaongoza mamia ya waombolezaji katika ibada ya kumuaga na kumsindikiza katika nyumba yake ya milele Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Marehemu Mhe. Kakusulo Mwakipome Mbutolwe Sambo aliyefariki Dunia mnamo 26 Julai, 2026 jijini Dar es Salaam.

Ibada hiyo ya kumuaga Marehemu Jaji Sambo ili kumpumzisha kwenye nyumba yake ya milele imefanyika leo tarehe 31 Julai, 2026 nyumbani kwa marehemu kitongoji cha Masebe wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya.

Akitoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa, majirani na marafiki Mhe. Dkt. Siyani amesema kuwa, maisha ya marehemu Jaji Sambo ni maisha ya mfano kwa aliowaacha kwani aliyaishi maisha yake kama sehemu ya maandalizi ya maisha ambayo sasa ameyaanza.

Jaji Kiongozi amesema kwa wale wanaomjua marehemu Jaji Sambo alikuwa mtu muadilifu mwenye hekima na imani ya Mwenyezi Mungu, na ndiyo maana Majaji na watu kutoka sehemu mbalimbali wakiwemo aliofanya nao kazi na alioshirikiana nao katika shughuli mbalimbali za kijamii wamesafiri kuja kumuaga na kumpumzisha katika nyumba yake ya milele, hali hiyo inaonesha jinsi gani aliweza kuishi na watu vizuri.

Aidha, Mhe. Dkt. Siyani amesema kuwa, kwa upande wa Mahakama na tasnia ya Sheria kwa ujumla, Mhe. Sambo alichangia kwa kiasi kikubwa katika kutafsiri sheria kupitia maamuzi mbalimbali ambayo yataendelea kuwepo hata baada ya kuwa yeye amepumzika.

Aliongeza kuwa, maamuzi ambayo aliyatoa yameleta mchango ambao umewasaidia wengi kufahamu haki na namna ambavyo wanaweza kuziendea mahakamani. Mhe Sambo alikuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza taaluma za wengine.

Mhe. Dkt.Siyani alirejea salamu za rambirambi kutoka kwa mmoja wa wahadhiri wa chuo kikuu cha Dar Es Salaam na kueleza namna ambavyo alimsaidia mhadhiri huyo kukamilisha tafiti yake. Jambo hilo linaonesha namna ambavyo alifundisha wengi na wengi wataendelea kumkumbuka.

Aidha, Mhe. Dkt. Siyani amesema kwamba, pamoja na hadhi yake ya Ujaji, Mhe. Sambo aliendelea kushikilia imani yake kwa Mungu na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii wakati wa utumishi wake na hata baada ya kustaafu utumishi alijishughulisha na kilimo na ufugaji akiwa Sumbawanga na hata mkoani Arusha.

“Madaraka tunayopewa ni makoti na majoho, Maisha yetu rasmi yapo katika Jamii inayotuzunguka hivyo hatupaswi kujitenga nayo,” alisema Jaji Kiongozi, akisisitiza juu ya mafunzo yapatikanayo katika maisha ya Marehemu Jaji Kakusulo Sambo.

“Nimepata funzo kupitia maisha ya Jaji Sambo hakuwabagua watu waliomzunguka, alikuwa anafikika na watu wote, alikwa tayari kupokea ushauri kutoka kwa mtu yoyote hata walioko chini yake na aliwaunganisha watu akiwa hai lakini leo pia katika kumuaga ametuunganisha pamoja watu wa imani tofauti,” amesisitiza Mhe. Dkt. Siyani.

Jaji Kiongozi alihitimisha kwa kusema kuwa, wanapata faraja wakiyakumbuka maneno ya Mungu yasemayo, “Heri wafu wafao katika Bwana maana watapata kupumzika la milele,”

Kwa upande wake, Mchungaji Michael Bureta aliyeongoza Misa takatifu ya Ibada ya maziko ya Marehemu Jaji Sambo alisema, “Ndugu yetu amelala katika kristo na ni njia mbayo kila mmoja wetu atapita. Tuiombee familia ili iangalie jambo hili katika imani na waendelee kumkumbuka kwa imani na sala wakati wote.”

Mchungaji Bureta aliongeza kuwa, Marehemu alikuwa na mchango mkubwa sana katika Kanisa alinunua vifaa mbalimbali vya Kanisa, kuwezesha safari za kikanisa ndani na nje ya nchi na alikuwa Mfadhili wa Kwaya ya Kanisa hadi kuteuliwa mnamo mwaka 2023 kuwa Mwenyekiti wa kwaya ya “Nuru Angaza” kanisani kwake alipokuwa mkoani Arusha.

Naye, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mashtaka Mkoa wa Mbeya alisema kuwa, msiba wa kuondokewa na Jaji Mstaafu, Marehemu Mhe. Sambo umeacha pengo kubwa kwa watu ambao mpaka sasa walikuwa wanategemea huduma kutoka kwake.

Marehemu Jaji Kakusulo Mwakipome Mbutolwe Sambo ameacha mjane mmoja, Watoto watano na Wajukuu 11 “BWANA ALITOA, BWANA AMETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE” AMEN.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akiaga mwili wa marehemu Jaji Mstaafu Kakusulo Mwakipome Mbutolwe Sambo mara baada ya Ibada Takatifu ya mazishi iliyofanyika nyumbani kwa marehemu kitongoji cha Masebe wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya, leo tarehe 31 Julai, 2026.

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Ferdinand Leons Katipwa Wambali akiaga mwili wa marehemu Jaji Mstaafu Kakusulo Mwakipome Mbutolwe Sambo.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (katikati), akiwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Ferdinand Leons Katipwa Wambali (wapili kushoto), na Majaji wengine wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa kwenye mazishi ya marehemu Jaji Sambo. Walioketi mbele (wa kwanza kushoto) ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Iringa Mhe. Dustun Beda Ndunguru, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Angaza Mwipopo (wa pili kulia) na (wa kwanza kulia) ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Thadeo Marco Mwenempazi.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akihutubia waombolezaji katika mazishi hayo.

Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Masjala Kuu Makao Makuu ya Mahakama Mhe. Chiganga Mashauri Tengwa akifanya utambulisho wa Viongozi walioshiriki katika mazishi hayo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Rungwe Mhe. Jackson Banobi akitoa salamu za rambirambi za Mahakama ya Wilaya Rungwe na kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Rungwe.

Sehemu ya Viongozi wa Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Rungwe wakiwa katika mazishi hayo

Sehemu ya Watoto wa Marehemu wakiongozwa na Bw. Gwakisa Kakusulo Sambo (aliyeshika kipaza sauti) akisoma wasifu wa Marehemu Jaji Mstaafu Sambo.

Kwaya ya Angaza nuru ikitumbuiza katika mazishi hayo, kwaya ambayo Marehemu Jaji Sambo alikuwa Mwenyekiti wake.


Mwili wa Marehemu Jaji Mstaafu Sambo ukipumzishwa katika Nyumba yake ya milele.

Sehemu ya mamia ya waombolezaji katika mazishi hayo.


Sehemu ya mamia ya waombolezaji katika mazishi hayo

Sehemu ya mamia ya waombolezaji katika mazishi hayo.

Majaji wakiwa wamebeba Jeneza lenye mwili wa marehemu Jaji Mstaafu Kakusulo Mwakipome Mbutolwe Sambo wakati wa shughuli ya mazishi.

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Ferdinand Leons Katipwa Wambali akisaini Kitabu cha waombolezaji nyumbani kwa marehemu Jaji Mstaafu Kakusulo Mwakipome Mbutolwe Sambo.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akisaini Kitabu cha waombolezaji nyumbani kwa marehemu Jaji Mstaafu Kakusulo Mwakipome Mbutolwe Sambo 

Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania walioshiriki msiba huo wakiaga Mwili wa Marehemu Jaji Mstaafu Kakusulo Mwakipome Mbutolwe Sambo mara baada ya Ibada Takatifu ya mazishi iliyofanyika nyumbani kwa marehemu kitongoji cha Masebe wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni