Jumatano, 15 Julai 2026

JAJI MFAWIDHI MANYARA AFANYA ZIARA YA UKAGUZI WA MAHAKAMA

Na. CHRISTOPHER MSAGATI- Mahakama, Manyara

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi amefanya ziara ya Ukaguzi katika Mahakama zilizopo Wilayani Mbulu na Hanang’ na kuwasisitiza watumishi kufanya kazi kwa uadilifu, ueledi na uwajibikaji ili kuhakikisha malengo ya Mahakama yanatimia ipasavyo.

Hii ni ziara ya kwanza ya ukaguzi kwa Mhe. Dkt. Mambi tangu ahamie Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara kama Jaji Mfawidhi akitokea Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Tabora ambapo pia alikuwa Jaji Mfawidhi.

Akizungumza na watumishi katika Mahakama ya Wilaya ya Mbulu, Mhe. Dkt. Mambi aliwaasa watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na nidhamu wanapokuwa ofisini na hata wanapokuwa nje ya Ofisi.

“sisi watumishi wa Mahakama tunapaswa kuishi kwa nidhamu kuanzia ofisini na hata tunapokuwa nje ya Ofisi zetu, tunatarajiwa kuwa vioo vya jamii kwa wadaawa wetu na watu wote tunaowahudumia. Kwa misingi hii, maadili na nidhamu lazima vitutawale popote tutakapokuwa”, alisema Mhe. Dkt. Mambi.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na Mahakimu wa vituo vilivyokaguliwa, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Charles Mnzava aliwasisitiza Mahakimu kuhakikisha kuwa wanahuisha taarifa za mashauri yao kwenye mfumo kila siku bila kukosa na kuhakikisha kuwa wanatoa nakala za Hukumu ipasavyo.

“Katika kipindi hiki cha matumizi makubwa ya TEHAMA, hatutarajii kuona kuwa tuna madeni ya kuhuisha mashauri katika mfumo rasmi uliowekwa hivyo ninawasihi mlichukulie suala hili kwa uzito wa hali ya juu. Vilevile hatutarajii tukifika katika magereza yetu tukutane na mfungwa ambaye analalamika kukosa nakala ya hukumu katika zama hizi”, alisema Mhe. Mnzava.

Kwa upande wa Wilaya ya Mbulu, Mahakama zilizokaguliwa ni Mahakama ya Wilaya Mbulu, Mahakama za Mwanzo Daudi, Dongobesh, Haydom na Gereza lililopo wilayani Mbulu.

Kwa upande wa Wilaya ya Hanang, Mahakama ambazo zilikaguliwa ni Mahakama ya Wilaya ya Hanang, Mahakama za Mwanzo Katesh, Bassotu na Endasak pamoja na mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Hanang ambao unaendelea kwa sasa.

Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Mambi alifanikiwa kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbulu na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mhe. Michael Semindu pamoja na kamati ya Wilaya ya Ulinzi na usalama, ambapo Mkuu wa Wilaya huyo aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama hususan kusaidia upatikanaji wa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama na upatikanaji wa hati za viwanja hivyo.

Aidha, Mhe. Dkt. Mambi alitumia pia ziara hiyo kutambulisha viongozi wapya wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara ambao ni yeye mwenyewe pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Charles Mnzava ambaye awali alikuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara.

Pia katika ziara hiyo, viongozi wengine walioambatana nao ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu anayehudumu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara Mhe. Mariam Lusewa pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Bi. Nyanzobe Hemedi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (aliyesimama) akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbulu (hawapo pichani) katika ziara ya Ukaguzi iliyofanyika wilayani hapo, kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Charles Mnzava na kulia ni Naibu Msajili anayehudumu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara Mhe Mariam Lusewa.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (wa kwanza kulia) akifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, aliyekaa mbele ni Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mhe. Michael Semindu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (wa tatu kushoto) akiendelea na zoezi la ukaguzi katika Mradi wa Ujenzi katika Mahakama ya Wilaya ya Hanang.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi akisalimiana na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Hanang mara baada ya kufika kituoni hapo kwa ajili ya Ukaguzi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi akiongoza zoezi la ukaguzi katika Mahakama ya Mwanzo Bassotu wilayani Hanang.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Haydom iliyopo Wilayani Mbulu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (wanne kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara pamoja na viongozi waandamizi wa Gereza la Wilaya ya Mbulu mara baaada ya kufanya Ukaguzi Gerezani hapo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (wa tatu kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Hanang.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe. Charles Mnzava (aliyesimama) akichangia neno wakati walipo mtemebelea Ofisini Mkuu wa Wilaya ya Mbulu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (aliyesimama katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Dongobesh wilayani Mbulu.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni