Alhamisi, 16 Julai 2026

ZIARA YA MAHAKAMA LINDI YAANGAZIA MAFANIKIO YA KITUO JUMUISHI CHA UTOAJI HAKI

  •  Timu ya Habari, Elimu na Mawasiliano yajionea matokeo ya Mradi wa Awamu ya Pili wa Maboresho ya Mahakama
  • Uwepo wa Mahakama Kuu Lindi watajwa kufurahiwa na Wananchi wa Mkoa huo
  • Wapunguza aza ya wananchi kusafiri umbali mrefu kusaka huduma za Mahakama Kuu

Na HALIMA MNETE, Mahakama- Lindi

Timu ya Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania imefanya ziara katika Mkoa wa Lindi tarehe 15 Julai, 2026 kwa kutembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (Integrated Justice Centre – IJC), kwa lengo la kujionea mafanikio ya utekelezaji wa Mradi wa Awamu ya Pili wa Maboresho ya Mahakama ya Tanzania katika kuimarisha utoaji wa huduma za haki kwa wananchi.

Katika ziara hiyo, timu ilipata fursa ya kufanya mahojiano na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Lindi, Mhe. Sylvester Kainda, Mtendaji wa Mahakama Kuu Lindi, Bi. Quip Mbeyela pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mhe. Elia Mrema ambao kwa pamoja walieleza mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Lindi na namna ilivyoleta mageuzi makubwa katika upatikanaji wa huduma za kimahakama.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Kainda alisema, kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Lindi imekuwa hatua muhimu katika kusogeza huduma za haki karibu na wananchi na kupunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa Mkoa huo kwa muda mrefu.

"Kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Lindi ni hatua kubwa katika kuboresha upatikanaji wa haki. Wananchi waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kwenda Mtwara sasa wanapata huduma karibu na maeneo yao. Hii imepunguza muda wa usikilizaji wa mashauri, gharama kwa wananchi na kuongeza imani yao kwa Mahakama," alisema.

Kwa upande wake, Bi.Quip Mbeyela alisema mradi huo umeleta manufaa makubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi na Wilaya zake kwa kuwa umeondoa aza ya safari ndefu zilizokuwa zikifanyika kufuata huduma za Mahakama Kuu.

"Wananchi wameupokea mradi huu kwa furaha kubwa, zamani walitumia muda mwingi na fedha nyingi kusafiri kwenda Mtwara kutafuta haki. Leo hii huduma zinapatikana hapa Lindi, jambo ambalo limewawezesha kuendelea na shughuli zao za kijamii na kiuchumi bila usumbufu mkubwa," alisema Mtendaji huyo.

Naye Naibu Msajili, Mhe. Mrema, alisema uwepo wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Lindi umeongeza ufanisi katika utendaji wa Mahakama kupitia matumizi ya mifumo ya TEHAMA na uendeshaji wa huduma kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia.

"Mradi huu umeimarisha uendeshaji wa mashauri kwa kuwezesha matumizi ya nyaraka za kidijitali na utekelezaji wa utaratibu wa kufanya kazi bila matumizi ya karatasi (paperless). Hali hii imeongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, imeharakisha uchakataji wa mashauri na kupunguza gharama za uendeshaji," alisema Mhe. Mrema.

Taarifa zilizowasilishwa wakati wa ziara hiyo zinaonesha kuwa kabla ya kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Lindi kupitia Tangazo la Serikali Na. 76 la mwaka 2026, wananchi kutoka Wilaya za Kilwa, Liwale, Nachingwea na Ruangwa walilazimika kusafiri zaidi ya kilomita 300 kwenda Mtwara kufuata huduma za Mahakama Kuu. Hali hiyo ilisababisha matumizi makubwa ya muda na fedha, huku ikiathiri shughuli zao za uzalishaji.

Hata hivyo, kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Lindi kumeondoa changamoto hiyo kwa kusogeza huduma karibu na wananchi, hatua iliyochangia kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri, kupunguza gharama za kutafuta haki na kuimarisha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo.

Aidha, Watumishi wa Mahakama hiyo wameeleza kuwa, matumizi ya mifumo ya kidijitali na uendeshaji wa ofisi bila karatasi yameongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kupunguza gharama za uendeshaji na kuimarisha usimamizi wa mashauri.

Ziara hiyo imeiwezesha Timu ya Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano kujionea kwa karibu matokeo ya utekelezaji wa Mradi wa Awamu ya Pili wa Maboresho ya Mahakama, unaoendelea kuimarisha miundombinu ya kimahakama na kusogeza huduma za haki karibu zaidi na wananchi.

Mafanikio hayo yanaendelea kudhihirisha dhamira ya Mahakama ya Tanzania ya kutoa huduma bora za haki mapema ipasavyo, kwa ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya Uadilifu, Weledi na Uwajibikaji.


Jengo la Kituo Jumishi cha Utoaji Haki (IJC) Lindi, likiwa ni moja kati ya majengo ya Mahakama yaliyojengwa ikiwa ni utelelezaji wa Mradi wa Awamu ya Pili wa Maboresho ya Mahakama ya Tanzania.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Lindi, Mhe. Sylvester Kainda.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Lindi, Mhe. Elia Mrema.


Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Lindi, Bi. Quip Mbeyela.

Mahojiano yakiendelea.

Picha ya pamoja, wa tatu kulia ni 
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Lindi, Mhe. Elia Mrema, wa tatu kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Lindi, Bi. Quip Mbeyela, wa pili kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano (HIECU), Bw. Gerard Chami na sehemu ya Maofisa Habari wa Mahakama.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni