Jumatano, 8 Julai 2026

JAJI MKUU ASHIRIKI KWENYE MAZISHI YA MTUMISHI WA MAHAKAMA YA WILAYA KALIUA

Na. MWANDISHI WETU - Mahakama, Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Masaju leo tarehe 8 Julai, 2026 ameungana na familia, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na watumishi wa Mahakama kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Mtumishi wa Mahakama ya Wilaya Kaliua, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kaliua, Mhe. Anna Elia Chilongola aliyefariki dunia tarehe 3 Julai, 2026.

Ibada na shughuli za mazishi zimefanyika katika Mtaa wa Chang'ombe Dispensari, jijini Dodoma nyumbani kwa marehemu, ambapo viongozi mbalimbali wa Mahakama kutoka Makao Makuu ya Mahakama, Masjala Ndogo za Dodoma na Tabora wakiwemo Majaji wa Rufani na Mahakama Kuu, Wasajili, Naibu Wasajili, Mahakimu, watumishi wa Mahakama pamoja na viongozi kutoka Taasisi mbalimbali zinazofanya kazi na Mahakama katika ngazi mbalimbali walihudhuria kushiriki katika kumuaga marehemu Anna.

Jaji Mkuu alifika katika eneo la mazishi na kushiriki kutoa heshima za mwisho kwa marehemu pamoja na kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na watumishi wa Mahakama waliofiwa na mwenzao, kabla ya kuondoka kuendelea na majukumu mengine ya kitaifa yaliyokuwa amejipangia.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dodoma Joachim Tiganga akitoa salaam za pole kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania amesema kuwa, marehemu alikuwa muadilifu, mwenye weledi, mchapa kazi hondari na hata alipokea salamu kutoka kwa Jaji Kiongozi akielezea umahiri wake katika kuchapa kazi enzi za uhai wake.

“Ni kweli usiopingika kwamba Mahakama ya Tanzania imempoteza mlezi wa Mahakimu wachanga waongia kazini kwani kwa sehemu kubwa Mahakama ilimtumia pia kama mlezi wa watumishi wengine katika kazi za kila siku za utoaji haki,” amesema Jaji Tiganga.

Mahakama ya Tanzania inatoa pole kwa familia ya Marehemu, Ndugu, Jamaa, Marafiki na wafanyakazi wote wa Mahakama ili azidi kuombewa na kupata pumziko la milele.

Wakizungumza wakati wa shughuli hizo, viongozi mbalimbali walimkumbuka Mhe. Anna Elia Chilongola kuwa mtumishi aliyekuwa mwadilifu, mchapakazi na mwenye kujituma katika utekelezaji wa majukumu yake, pia alikuwa Mchamungu huku wakieleza kuwa mchango wake katika utumishi wa Mahakama utaendelea kukumbukwa.

Mahakama ya Tanzania inaendelea kutoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na watumishi wote walioguswa na msiba huu, ikiomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.

Jeneza lililobeba mwili wa Marehemu aliyekuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kaliua, Mhe. Anna Elia Chilongola aliyefariki dunia tarehe 3 Julai, 2026.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Masaju (katikati) leo tarehe 8 Julai, 2026 ameungana na familia, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na watumishi wa Mahakama kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Mtumishi wa Mahakama ya Wilaya Kaliua, wengine ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dodoma Joachim Tiganga (kulia) na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Tabora Mhe. Martha Mpaze kulia akiteta jambo na Jaji Mkuu wa Tanzania.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Masaju akisaini Kitabu cha waombolezaji mara baada ya kuwasili kwenye msiba wa aliyekuwa Mtumishi wa Mahakama ya Wilaya Kaliua Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kaliua, Mhe. Anna Elia Chilongola

Sehemu ya Naibu wasajili na Mahakimu Wakazi Mfawidhi wa Mahakama za Wilaya walioshiriki katika msiba huo.
Sehemu ya wananchi, Ndugu, Jamaa na Marafiki walioshiriki Msiba huo
Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya wakiwa wamebeba Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kaliua, Mhe. Anna Elia Chilongola aliyefariki dunia tarehe 3 Julai, 2026.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dodoma Joachim Tiganga akiweka shada la Maua kwenye kaburi la marehemu Anna Elia Chilongola.


Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Masaju (mwenye tai nyekundu) akiwasili msibani nyumbani kwa marehemu Anna Elia Chilongola.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Masaju (mwenye tai nyekundu) akiwasalimu waombolezaji kwenye msibani nyumbani kwa marehemu Anna Elia Chilongola.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Masaju (mwenye tai nyekundu) akimpa pole Mume wa marehemu alipowasili kwenye msibani nyumbani kwa marehemu Anna Elia Chilongola.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni