Alhamisi, 9 Julai 2026

JOPO LA MAHAKAMA YA RUFANI MBEYA LAFANYA TATHMINI YA USIKILIZAJI WA RUFAA ZA MADAI

Na. MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Mahakama ya Rufani ya Tanzania imefanya kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za usikilizaji wa mashauri ya Rufaa za madai katika Masjala Ndogo ya Mbeya, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhitimisha rasmi kikao cha Mahakama hiyo kilichoanza Juni 18, 2026 na kinachotarajiwa kumalizika Julai 17, 2026.

Kikao hicho kiliongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Winfrida Korosso, na kuhudhuriwa na Waheshimiwa Majaji wa Rufani walioambatana naye katika kikao hicho ambao ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe, Dkt. Mary Levira, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe Agnes Mgeyekwa, na Viongozi wengine wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya.

Kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya waliohudhuria ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya, Jaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Said Kalunde, Jaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Mussa Pomo.

Wengine ni Naibu Msajili Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Bernard Mpepo, Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer, Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bi. Sarah Lossi na wadau wengine wa haki madai.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kikao hicho, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Agatha Chugulu alisema kuwa, kati ya mashauri 48 yaliyopangwa kusikilizwa, mashauri 32 sawa na asilimia 67 yameshasikilizwa. Kati ya hayo, mashauri 23 yameshapatiwa maamuzi, huku mashauri tisa (09) yakisubiri kutolewa maamuzi kwa mujibu wa taratibu za Mahakama.

Aidha, alieleza kuwa, mashauri 16 yaliahirishwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo wito wa Mahakama kutowafikia baadhi ya wadaawa kwa wakati kwa mujibu wa matakwa ya sheria, mapungufu katika maandalizi ya kumbukumbu za rufaa pamoja na kutokuwapo kwa baadhi ya nyaraka muhimu, hali iliyolazimu wahusika kuongezewa muda wa kufanya masahihisho.

Katika tathmini hiyo, ilibainika kuwa baadhi ya mawakili hawakutumia ipasavyo mamlaka ya Ofisi ya Msajili na Naibu Wasajili wa Mahakama ya Rufani kutatua changamoto za mashauri yao kabla ya tarehe za usikilizaji. Vilevile, baadhi yao hawakufanya maandalizi ya kutosha mapema, jambo lililosababisha kasoro ambazo zingeweza kubainika mapema au kujitokeza wakati wa usikilizaji na hivyo kuchelewesha utoaji wa haki kwa wakati.

Aidha, pamoja na changamoto hizo, kikao kilieleza kuridhishwa na mafanikio yaliyopatikana, ikiwemo kusikilizwa kwa mashauri 32 kati ya 48 yaliyopangwa pamoja na ushirikiano mzuri uliooneshwa na Mawakili wa Serikali na wa kujitegemea waliohudhuria kwenye vikao hivyo kwa wakati. Mafanikio hayo yameendelea kuimarisha juhudi za Mahakama ya Rufani ya Tanzania za kuongeza ufanisi katika usikilizaji wa mashauri na kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati mapema ipasavyo.

Jopo la Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Rufani wakiwa kwenye kikao cha tathmini ya uendeshaji wa mashauri ya madai 48 yaliyendeshewa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, katikati ni Mwenyekiti wa Jopo hilo Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Winifrida Beatrice Korosso, kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Agnes Zephania Mgeyekwa na kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Mary Calorine Levira.

Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Said Kalunde (katikati) akizungumza jambo katika kikao hicho, kulia ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya, na kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Mussa Pomo.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Mhe. Agatha Chugulu (aliyesimama) akiwasilisha taarifa katika kikao hicho, kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Bernard Mpepo

Sehemu ya Wadau walioshiriki katika kikao hicho cha tathmini ya uendeshaji mashauri ya rufaa za Madai Masjala Ndogo Mbeya  

Sehemu ya Wadau walioshiriki katika kikao hicho cha tathmini ya uendeshaji mashauri ya rufaa za Madai Masjala Ndogo Mbeya.

Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer (kushoto), na kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Mbeya, Mhe. Tedy Mlimba waikifuatilia kikao hicho.


Mmoja wa wadau katika kikao hicho akitoa neno la shukrani kwa Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani lililoendesha kikao chake Mbeya.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)






  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni