Alhamisi, 9 Julai 2026

JAJI MKUU MASAJU AWAPOKEA, AWAKUBALI MAWAKILI WAPYA 655

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, leo tarehe 09 Julai, 2026 amewapokea na kuwakubali waombaji 655, wakiwemo wanaume 329 na wanawake 326, kuwa Mawakili wa Kujitegemea.

Sherehe hiyo imefanyika katika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma na kuhudhuriwa na  Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, Majaji wa Mahakama Kuu, Viongozi wa Mahakama, wakiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Chiganga Tengwa, Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sundi Fimbo na Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama.

Walikuwepo pia Viongozi wengine, akiwemo Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Baraka Leonard, jopo la Wataalam wa Sheria likiongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka, Viongozi wa Baraza la Elimu ya Sheria na Wananchi kwa ujumla.

Hii ni Sherehe ya 74 ya kuwapokea Mawakili tangu kuanzishwa kwake mwaka 1986. Kupokelewa na kukubaliwa kwa waombaji hao 655, kunafanya idadi ya Mawakili walioandikishwa kufikia 14,875.

Miongoni mwa Mawakili hao wapya, 634 wamefaulu masomo yao Shule ya Sheria kwa Vitendo Tanzania, sita wamefaulu mtihani wa uwani (Bar Exam) na 15 wamepata msamaha chini ya kifungu cha 16 (2) cha Sheria ya Mawakili [Sura ya 341 Toleo la Mwaka 2023].

Akiwapokea na kuwakubali waombaji hao, Jaji Mkuu amesema, “Kwa mamlaka niliyopewa katika kifungu cha 16 (4) cha Sheria ya Mawakili [Sura ya 341 Toleo la Mwaka 2023], ninatamka kwamba wale wote ambao majina yao yamesomwa hapa wamekubaliwa kuwa Mawakili na wameorodheshwa rasmi kwenye orodha ya Mawakili kuanzia leo tarehe 09 Julai, 2026."

Baada ya kukubaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania aliwatunuku vyeti vya uwakili na kusema, “Kwa mamlaka niliyopewa katika kifungu cha 16 (4) cha Sheria ya Mawakili [Sura ya 341 Toleo la Mwaka 2023], ninawatunuku vyeti vya uwakili wa kujitegemea, Mawakili wote waliopokelewa na kukubaliwa leo hii kama walivyoorodheshwa katika kitabu cha Mawakili.”

Tukio hilo liliibua shangwe na fifijo kutoka kwa ndugu wa waombaji hao waliokuwa wamefurika kwenye viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania. Muda mchache baadaye, Mawakili hao walikula kiapo cha uadilifu mbele ya Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, akitoa tamko maalum la kuwapokea na kuwakubali Mawakili wa Kujitegemea 655 wapya leo tarehe 9 Julai, 2026 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dar es Salaam.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, ikipokea heshima kutoka kwa Mawakili wapya (picha chini) baada ya kuwapokea na kuwakubali kuwa Mawakili wa Kujitegemea.
 
Sehemu ya Mawakili wa Kujitegemea wapya 655 (juu na chini) ikitoa heshima kwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, baada ya kupokelewa na kukubaliwa kuwa Mawakili.


Sehemu ya Mawakili wa Kujitegemea wapya 655 wakila kiapo cha maadili (juu na chini) mbele ya Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa (hayupo kwenye picha).


Sehemu ya Mawakili wa Kujitegemea wapya (juu na chini) wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri wakati wa sherehe hiyo.


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, akitoa utambulisho wa Viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe hiyo.

Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, akiwatambulisha waombaji kwa majina kabla ya kupokelewa na kukubaliwa kuwa Mawakili wa Kujitegemea na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju.

Jopo linaloongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (kulia) likiwa kwenye sherehe za kuwapokea na kuwakubali Mawakili wa Kujitegemea wapya 655.

Viongozi wa Baraza la Elimu ya Sheria wakiwa kwenye sherehe hiyo.

Wananchi wakiwa kwenye sherehe hiyo.

Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu waliohudhuria sherehe hiyo.
 
Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati waliokaa juu na chini) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Mawakili wa Kujitegemea wapya 655.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni