Na MARY GWERA & HABIBA MBARUKU, Mahakama - Dodoma
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amewataka
Mawakili wapya wa Kujitegemea kutenda haki huku wakiyazingatia, kuyaheshimu,
kuyajali na kuyapa kipaumbele makundi yenye mahitaji maalum wakiwemo Wajane, Watoto, Wajawazito, Wazee na Watu wenye
ulemavu.
Mhe. Masaju ameyasema hayo leo tarehe 09 Julai, 2026 alipokuwa akitoa
hotuba yake katika Hafla ya 74 ya Kuwakubali na Kuwapokea Mawakili wapya 655
iliyofanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini
Dodoma.
Akizungumza na Mawakili hao Jaji Mkuu amewasisitiza kuendelea kutekeleza
majukumu yao huku wakimtanguliza Mungu kama ambavyo wote wamekiri uwepo wa
Mungu kupitia viapo vyao.
Ameeleza kuwa, Mawakili wana mchango mkubwa katika kuisaidia Mahakama
kufanya maamuzi yanayozingatia haki kutokana na uhalisia wa matukio bila
upendeleo huku wakitenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti ya
kiufundi na kutekeleza jukumu la kusimamia upatikanaji haki kwa ufanisi, jambo
litakaloiwezesha Mahakama kuifikia azma ya kutoa haki mapema ipasavyo.
“Moja nikiwakumbusha sisi wenzetu huku mahakamani umuhimu wa kutenda haki
bila kufungwa na masharti ya kiufundi kupita kiasi. Sasa sisi mahakamani,
Mahakimu na Majaji hatukai peke yetu. Tunasaidiwa na ninyi Mawakili mlioko
kwenye utumishi wa umma na Mawakili mnaojitegemea. Ninazungumza na ninyi
kuwataka mtusaidie,” amesisitiza Mhe. Masaju.
Aidha, Jaji Mkuu ameeleza kuwa, Serikali imetunga sheria inayowawezesha
Mawakili kutoa msaada wa kisheria kwa Watanzania wasio na Mawakili na wale
wasio na uwezo wa kumudu gharama za Mawakili hivyo ni jukumu la Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS) kutekeleza jukumu hilo, huku akiwasihi kutekeleza
jukumu hilo kwa ufanisi ipasavyo na si kwa unyonge kwa kuwa dhamira yao ni
njema kuwasaidia watu masikini…...” Na mnavyotekeleza hilo jukumu litekelezeni kwa
ufanisi ipasavyo na wala sio kwa unyonge. Kwa sababu dhamira yenu ni njema
mmejiwekea hiyo ninyi wenyewe.”
Akizungumzia kuhusu uhuru wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), kama
ilivyoanzishwa na Ibara ya 59B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Jaji Mkuu ameeleza kuwa, hiyo ndio ofisi iliyopewa mamlaka ya kufungua,
kuendesha na kusimamia mashauri yote, na kwamba inapokuwa ikitekeleza jukumu
hilo ikiongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka, Katiba imeelekeza katika Ibara ya
59B(4) kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka atakuwa huru, hataingiliwa na mtu yeyote au
na mamlaka yeyote isipokuwa itazingatia mambo matatu, moja nia ya kutenda haki,
kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki na maslahi ya umma.
Akisisitiza kwa kusema “ishini mambo hayo yote kwa namna ambayo tunataka watu
wapate haki.”
Ameongeza kuwa, zipo kanuni zilizotungwa na Mahakama mahsusi kwa ajili ya
makundi ya watu maalum katika jamii ambazo zilitangazwa katika gazeti la
Serikali namba 110 mwaka 2019 kanuni zinazowahusu watu wa makundi maalum ambao
ni Wajane, Watoto, Wajawazito,Wazee na Watu wenye ulemavu ambao wanatambulika
kutokana na tamaduni za kijamii, kiuchumi zilizopo katika jamii ambazo sio rafiki na wanabaguliwa au wamekuwa waathirika wa muda mrefu wa ukiukwaji wa
haki.
Kadhalika, amewataka kutenda kwa umakini na kuendelea kuwajibika vema na
kwamba ikiwa hawatafanya hivyo basi watawajibishwa na Mahakama endapo Mungu
atachelewa kuwaadhibu hapa duniani.
“Mimi nataka kila
mmoja wetu anaposhughulika na mashauri
haya awe makini. Sisi hatutamfuata mmoja
mmoja huko na kuanza kumchapa viboko lakini tukimjua kwamba anacheza na haki za watu hawa, kama Mwenyezi Mungu
atachelewa kumuwajibisha, sisi hapa tutamuwajibisha,” amesema Mhe. Masaju.
Amefafanua
kuwa, kanuni zinaeleza wazi kuwa, mashauri yoyote ya Haki Jinai au Haki Madai
yanayohusu watu kutoka katika makundi maalum yanapaswa kuhitimishwa ndani ya
miezi sita kuanzia tarehe ya kuanza kwa usikilizaji wake isipokuwa kama
Mahakama inaweza katika hali ya kipekee kuongeza muda huo kwa kipindi
kisichozidi miezi mitatu.
“Jaji
au Hakimu anayesikiliza kesi inayohusu mtu kutoka katika kundi maalum atatakiwa
kuzipa kipaumbele kesi hizo kuliko kesi nyingine zote katika hatua zote ikiwemo
usajili, usikilizaji na utoaji wa maamuzi na ninyi mtawakumbusha wanaozembea
kwamba kuna maelekezo ya Mheshimiwa Jaji Mkuu, mzipe kipaumbele kesi hizi,”
amesisitiza Jaji Mkuu.
Ameeleza
kuwa, ni wajibu wa Mahakama kuteua Afisa Dawati ili kusimamia kesi za makundi
maalum huku akirejelea kitabu cha Zaburi 41: 1-3, inayosisitiza kumkumbuka
mnyonge…. Heri amkumbukaye mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu, Bwana
atamlinda na kumhifadhi hai, naye atafanikiwa katika nchi, wala usimtie katika
hali wamtakiayo adui zake…… akaongeza kuwa “msipowahudumia kwa haki wanyonge
mnakaribisha laana katika familia zenu kuanzia kizazi cha kwanza hadi cha nne,
hatuwezi kufanikiwa katika nchi kama tutakuwa tunawadharau wanyonge.”
Amezitaja
kazi za Afisa Dawati kuwa ni pamoja na kutambua kesi na wahusika na kuwasilisha
taarifa hizo kwa Jaji au Hakimu aliyepangiwa kesi hiyo, kuwatambua watu wenye
uhitaji maalum, kuanzisha na kutunza kanzidata ya kesi zinazohusu makundi
maalumu, kutoa elimu na kuwaongoza wafanyakazi wengine kuhusu masuala ya
makundi maalumu na kutekeleza majukumu mengine yote kama yatakavyoelekezwa na
Jaji au Hakimu Mfawidhi, huku mahakamani hilo litekelezeni kwa ufanisi
ipasavyo.
Aidha,
amewataka Mawakili kushirikiana na Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama
katika utekelezaji wa majukumu yao na yenu huku wakizingatia uadilifu, faraja
kwa wanyonge, staha, uaminifu, uwezo wa kumudu majikumu na ushirikiano.
Katika
hatua nyingine, ameitaka TLS kulinda na kusimamia sheria na utekelezaji wa
kanuni zinazogusa makundi maalum huku wakiwa sauti kwa wasio na sauti, wakitoa
mchango wao wa usaidizi wa sheria kwa makundi hayo wakitekeleza majukumu yao
kwa uadilifu, akili weledi na busara.
Amewataka
Mawakili hao kutimiza wajibu wao wa kuwa mstari wa mbele kuwakumbusha Majaji na
Mahakimu katika mashauri ya Haki Jinai na Haki Madai kwa heshima na si kulaumu,
pia wajiulize wanatekeleza wajibu gani kama inavyoelekezwa katika kifungu cha
75 cha Sheria ya Mawakili (Sura ya 341 Marejeo ya 2023), hivyo ni vema kwa
pamoja kutekeleza ipasavyo sheria na kanuni zilizowekwa.
Pia,
amewaasa Mawakili hao kuendelea kuwaenzi wazazi, wenza wao, ndugu, jamaa na
marafiki ambao walikuwa pamoja nao kwa kipindi chote hadi walipofika walipo……
amesema, “muwaenzi wazazi wenu na ninyi mliooa na mlioolewa muwaheshimu wenzi
wenu kwa kuheshimu mchango wao kwani ni kuenzi utu na heshima kama inavyoelezwa
katika amri ya 4 inayosema waheshimu baba yako na mama yako, upate miaka mingi
na heri duniani…… nendeni mkatekeleze majukumu yenu kwa haki, usawa na uadilifu
Mahakama itaendelea kufuatilia utendaji wenu.”
Ameuhakikishia
Umma wa Watanzania kwamba, Mahakama itaendelea jukumu lake la msingi la kutoa
haki mapema ipasavyo kwa mujibu wa sheria.
Hii
ni sherehe ya 74 ya kuwapokea Mawakili, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1986 kupokelewa
na kukubaliwa waombaji hao 655 kunafanya idadi ya Mawakili walioandikishwa
kufikia 14,875.




















Hakuna maoni:
Chapisha Maoni