Jumapili, 19 Julai 2026

JAJI MLYAMBINA AHIMIZA WATUMISHI WA MAHAKAMA YA KAZI KULINDA UHURU WA MAHAKAMA

  • Awataka pia kuheshimu utawala wa sheria, kuendeleza ushirikiano na Wadau

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina, amewahimiza Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kuendelea kulinda uhuru wa Mahakama, kuheshimu utawala wa sheria na kuendeleza ushirikiano baina ya Mahakama, Taasisi na Wadau wa Haki Kazi nchini.

Mhe. Dkt. Mlyambina alitoa wito huo usiku wa kuamkia Jana tarehe 18 Juylai, 2026 kwenye hafla ya kumuaga iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirika la Hifadhi ya Jamii PSSSF Mwenge jijini Dar es Salaam baada ya kuteuliwa na kuapishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani  hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Haki inapotekelezwa kwa wakati na kwa usawa, hujenga amani mahali pa kazi, huongeza imani ya wananchi kwa Taasisi za umma na huimarisha maendeleo ya Taifa,” alisema huku akinukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alisema, “Haki ndiyo msingi wa amani, na amani ndiyo msingi wa maendeleo.”

Mhe. Dkt. Mlyambina alimshukuru kila mmoja kwa ushirikiano, heshima, urafiki na msaada waliompa katika kipindi chote alichohudumu kama Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Kazi na kwamba ataendelea kuyathamini mahusiano hayo na popote atakapokuwa ataendelea kuwa balozi mwema wa Mahakama ya Kazi.

Jaji Mlyambina alieleza kuwa anajivunia kuwa sehemu ya safari ya kuendelea kuimarisha Mahakama ya Kazi, kwani ameshuhudia maendeleo katika usimamizi wa mashauri, matumizi ya teknolojia, uboreshaji wa huduma kwa wananchi, na kuimarika kwa ushirikiano na wadau mbalimbali.

“Mafanikio haya hayakuwa ya mtu mmoja, ni matokeo ya kazi ya pamoja. Tulifanya kazi kama timu moja. Timu yetu haikuwa kikundi cha watu wanaofanya kazi pamoja, ilikuwa kikundi cha wau wanaoaminiana kila mmoja. Nimebahatika kufanya kazi na timu yenye uwezo mkubwa, inayojali haki na inayoweka mbele maslahi ya wananchi. Kila mmoja wenu amechangia mafanikio yaliyopatikana,” alisema na kuwashukuru kwa dhati Majaji wenzake, Wasajili, Mahakimu na watumishi wote wa Mahakama ya Kazi.

Aidha, Mhe. Dkt. Mlyambina alieleza kuwa akiwa Jaji Mfawidhi alipata nafasi ya kujifunza, kufundishwa na kushirikiana na watu wenye weledi mkubwa na kujifunza kuwa uongozi si mamlaka bali ni dhamana; si nafasi ya kutawala bali ni wajibu wa kutumikia wengine kwa haki, busara na unyenyekevu.

Alimnukuu Mwandishi Simon Sinek katika kitabu chake ‘Find your why’ uk. 157, ambaye anasema, “The greatest contribution of a leader is to make other leaders” kwa tafsiri isiyorasmi kwa Kiswahili anasema, “Mchango mkubwa wa Kiongozi ni kuwafanya wengine kuwa Viongozi.”

“Naamini nimetekeleza hili kwa kadri nilivyoweza. Zaidi ya yote kila iitwayo leo kwa ushirikiano tulioujenga niliona kila mtumishi anatamani kuendelea kufanya kazi Mahakama ya Kazi” Mhe. Dkt. Mlyambina alisema.

Halikadhalika, aliwapitisha washiriki wa hafla hiyo kwenye nukuu nyingine ya Mwandishi Simon Sinek katika utangulizi wa kitabu chake cha Find your why anaposema:

“Fulfilment is a right and not a privilege. Every single one of us is entitled to feel fulfilled by the work we do, to wake up feeling inspired to go to work, to feel safe when we’re there and to return home with a sense that we contributed to something larger than ourselves. Fulfilment is not a lottery. It is not a feeling reserved for lucky few who get to say, ‘‘I love what I do’’

Kwa Kiswahili kisicho rasmi anasema, “Kuridhika ni haki, si upendeleo. Kila mmoja wetu ana haki ya kupata utoshevu kutokana na kazi anayoifanya; kuamka kila siku akiwa na hamasa ya kwenda kazini; kujisikia salama akiwa mahali pa kazi; na kurejea nyumbani akiwa na hisia kwamba ametoa mchango katika jambo kubwa zaidi kuliko maslahi yake binafsi. kuridhika si bahati nasibu inayowakuta wachache, bali ni haki inayomstahili kila mfanyakazi.”

Jaji Mlyambina ana imani kuwa Mahakama ya Kazi itaendelea kuwa nguzo muhimu katika kulinda haki za wafanyakazi na waajiri, kuimarisha mazingira bora ya kazi na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa kupitia utoaji wa haki wenye ufanisi na unaoaminika.

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina, akizungumza kwenye hafla ya kumuaga iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirika la Hifadhi ya Jamii PSSSF Mwenge jijini Dar es Salaam.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga, akizungumza kwenye hafla hiyo.

Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Enock Matembele, akitoa utambulisho wa wageni mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo. Picha chini ni matukio ya picha za Wadau na Watumishi wa Mahakama kwenye hafla hiyo.












Picha na Bakari Mtaullah-Dar es Salaam.


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni