Jumapili, 19 Julai 2026

MAHAKAMA YA KAZI, WADAU WAMUAGA JAJI MLYAMBINA

  • Wampongeza kwa uongozi uliotukuka
  • Wamzawadia tuzo, zawadi mbalimbali
  • Yeye asema haki kazi haiwezi kujengwa na Mahakama peke yake

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina, ameagwa na Watumishi wa Mahakama hiyo pamoja na Wadau wa Haki Kazi baada ya kuapishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hafla ya kumuaga Mhe. Dkt. Mlyambina ilifanyika usiku wa kuamkia jana tarehe 18 Julai, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (PSSSF) Mwenge jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali, akiwemo Majaji wa Mahakama Kuu.

Wengine ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Mahusiano), Bi. Zuhura Yunus Abdallah, Kamishna wa Kazi Bara na Wawakilishi kutoka Wadau mbalimbali wa Haki Kazi, wakiwemo Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA),

Walikuwepo pia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mamlaka ya Usalama Kazini (OSHA), Mashirika ya Hifadhi ya Jamii ya PSSF na NSSF, Vyama vya Wafanyakazi, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wawakilishi Binafsi na Watumishi wa Mahakama ya Kazi.

Hafla hiyo ilipambwa na shamra shamra za utoaji Tuzo na Zawadi mbalimbali pamoja na muziki uliotumbuizwa na bendi na vijana kutoka Mahakama ya Kazi uliobeba ujumbe murua wa kumtakia heri Mhe. Dkt. Mlyambina kwenye majukumu yake mapya.

Salamu mbalimbali ziliwasilishwa na washiriki kwenye hafla hiyo, akiwemo Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo pamoja na Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano.

Katika salamu zake, Mhe. Dkt. Opiyo, pamoja na mambo mengne, alimwelezea Jaji Mlyambina kama Kiongozi asiyependa makuu na asiye mbinabinafsi, bali ni mtu anayependa kuwamshirikisha kila mtu kwenye majukumu mbalimbali ya kiutendaji, hivyo kuwa mfano bora katika uongozi.

“Tunakushukuru sana kwa uongozi uliotukuka, ni vigumu sana kukuelezea kutokana na makubwa uliyofanya, sisi tuliokuwa Mahakama ya Kazi tumejifunza (mengi), umekuwa mama, siyo baba katika uongozi...

“…Tumejifunza sana kwako kwa uongozi shirikishi. Hatukujisikia unyonge kuwa pamoja nawe, ulitushirikisha kwenye mambo mbalimbali. Hatutasahau kamati mbalimbali ulizozianzisha na kutojilimbikizia majukumu,” alisema.

Jaji Opiyo alimwelezea pia Mhe. Dkt. Mlyambina kama Kiongozi mfuatiliaji anayependa ndoto aliyonayo itimie na kile anachokiamini na kupanga kitokee, hivyo ni mtu anayefanikisha matokeo.

Aidha, Mhe. Dkt. Opiyo alimwelezea Jaji Mlyambina kama Kiongozi aliyejaa upendo anayetamani kila mtumishi apate kile kidogo kinachopatikana, kwani anaamini ufanizi kazini huongezeka pale Mtumishi anapofurahi.

Kwa upande wake, Bi. Zuhura alimpongeza Jaji Mlyambina kwa uimarisha uhusiano mzuri kati ya Mahakama, Serikali, Waajiri na Wafanyakazi na kwa kusimamia haki na usawa kwa wafanyakazi kwa Waajiri kwa weledi wa hali ya juu.

Aliemwelezea kuwa Ofisi yake haikuwa tu kwa ajili ya kutoa maamuzi ya kisheria bali pia ilikuwa chamichemi ya ushauri na hekima kwa Wadau wote wa sekta ya haki nchini.

Alieleza kuwa kuteuliwa kwake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani halikuwa jambo la bahati mbaya, bali ni matokeo ya utendaji uliotukuka, uadilifu na uwezo wake.

Naibu Katibu Mkuu alitumia fursa hiyo kumkaribisha Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi mpya, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga, na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliokuwa wakati akitekeleza majukumu yake.

Akihitimisha hafla hiyo, Mhe. Dkt. Mlyambina alieleza kuwa Ofisi ya Kamishna wa Kazi imeendelea kuwa msimamizi muhimu wa utekelezaji wa sheria za kazi, upatanishi wa migogoro na kukuza mazungumzo ya kijamii, hivyo kusaidia migogoro mingi kutatuliwa kabla haijafika mahakamani.

Alisema kuwa WCF imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha wafanyakazi wanaopata madhara wanapata fidia stahiki kwa mujibu wa sheria, jambo linaloimarisha haki na ustawi wa wafanyakazi na kupunguza migogoro Mahakamani.

Mhe. Dkt. Mlyambina alieleza pia kuwa OSHA imechangia kwa kiasi kikubwa kujenga utamaduni wa usalama na afya mahali pa kazi, hivyo kupunguza ajali na magonjwa yatokanayo na kazi na kuimarisha heshima kwa utu wa mfanyakazi.

Alisema kuwa CMA nayo amekuwa mdau muhimu wa huduma za upatanishi na usuluhishi wa migogoro ya kikazi, na kwa kufanya hivyo imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro inayofika Mahakama na kuhimiza utatuzi wa migogoro kwa njia za amani.

Kwa mjibu wa Mhe. Dkt. Mlyambina, PSSF na NSSF zimeendelea kutoa mchango mkubwa katika kuhakikisha wafanyakazi wanapata hifadhi ya jamii, jambo ambalo si tu linawapa usalama wa kiuchumi, bali pia linachangia ustawi wa jamii na uthabiti wa mahusiano ya kazi.

Alielezea pia upande wa vyama vya wafanyakazi TUCTA, TUGHE, TUICO na vingine ambavyo vimeendelea kuwa sauti muhimu ya wafanyakazi kwa kutetea haki zao, kukuza mazungumzo ya pamoja na kuhamasisha uhusiano wa kazi unaozingatia sheria, usawa na heshima.

“Kwa pamoja, kila mmoja wenu amekuwa mshirika wa karibu wa Mahakama ya Kazi katika kuhakikisha kuwa mfumo wa haki za kazi unafanya kazi kwa ufanisi,” alisema na kuongeza…

“Ingawa wakati mwingine tumekutana katika nafasi tofauti kutokana na majukumu yetu ya kisheria, tumekuwa tukiongozwa na lengo moja kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa sheria, migogoro inatatuliwa kwa haki na kwa wakati, na mazingira ya kazi nchini yanaendelea kuwa ya amani, tija na yenye kuheshimu utu wa binadamu.”

Jaji Mlyambina alibainisha pia kuwa katika kipindi chake cha uongozi kama Jaji Mfawidhi, amejifunza kuwa haki kazi haiwezi kujengwa na Mahakama peke yake, bali inahitaji waajiri wanaoheshimu sheria na wafanyakazi wanaotekeleza wajibu wao kwa uaminifu.

Alieleza pia kuwa inahitaji vyama vya wafanyakazi na waajiri vinavyotanguliza mazungumzo ya kijamii, pamoja na taasisi za Serikali zinazotekeleza majukumu yao kwa weledi.

Mhe. Dkt. Mlyambina alisema pia kuwa Mahakama imekuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha kuwa tofauti zinapotokea zinatatuliwa kwa haki, kwa mujibu wa sheria na bila upendeleo.

Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akipokea tuzo kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Mahusiano), Bi. Zuhura Yunus Abdallah, kwenye hafla ya kumuaga iliyofanyika Mwenge jijini Dar es Salaam.

Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akipokea zawadi kutoka kwa Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo.

Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (kulia) akipongezwa na Majaji na Watumishi wa Mahakama.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga (kushoto) akizungumza wakati wa hafla hiyo. Kulia ni sehemu ya watumishi wa Mahakama hiyo.

Meza Kuu inayoongozwa na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (katikati).

Meza Kuu inayoongozwa na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (katikati) ikiwa kwenye picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu na Wadau mbalimbali (juu na picha mbili chini).




Sehemu ya Wageni mbalimbali wakiwa kwenye hafla hiyo.


Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Mahusiano), Bi. Zuhura Yunus Abdallah akizungumza wakati wa hafla hiyo.


Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Vijana kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi (juu) na  Bendi ya Muziki (chini) wakitumbuiza wakati wa hafla hiyo.


Picha na Bakari Mtaullah-Dar es Salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni