Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine
Rwizile hivi karibuni alifanya ziara ya Ukaguzi wa
Mahakama za Wilaya mkoani humo na kuwataka Watumishi wa Mahakama hizo kutumia
vema taaluma na ujuzi walionao ili kutatua changamoto mbalimbali katika maeneo
yao ya kazi.
Mhe. Rwizile alifanya ziara hiyo kwa lengo la kuangalia maendeleo ya
shughuli za Mahakama katika maeneo ya mashauri, miundombinu pamoja na
watumishi.
“Tumieni vema taaluma mbalimbali mlizonazo
kutatua changamoto mbalimbali katika maeneo yenu ya kazi, nafahamu wapo
watumishi wameajiriwa mkiwa na taaluma tofauti na ajira zenu, hivyo ni fursa
kwenu kuonesha uwezo katika kusaidia shughuli zetu pale tunapokwama, hata hivyo
tukishirikiana vema tutaongeza ufanisi na tija katika shughuli za Mahakama,” alisema
Mhe. Rwizile.
Hata hivyo, Jaji Mfawidhi huyo alitoa pongezi
kwa Mtumishi, Mlinzi wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe, Bw. George Kato ambapo alisema,
“nimepokea taarifa yenu imeonesha huyu bwana ametatua tatizo la ki-Tehama kwa kutumia
taaluma yake, ambapo imesaidia shughuli za mashauri kutokwama, anastahili
pongezi kubwa na kutambuliwa, nasi tumeona. Ni rai yangu kuwa, kila mtumishi
mwenye taaluma tofauti na ajira/kada yake aitumie vema kama sehemu ya ubunifu
na weledi wa kusaidia shughuli zetu.”
Vilevile, alitoa wito kwa watumishi wote wa
Mahakama Kanda ya Kigoma kuwasilisha changamoto kwa Viongozi wao ili zitatuliwe
kabla ya kuleta madhara katika mnyororo wa utoaji haki mapema ipasavyo.
Aidha, alisema kuwa, watumishi waendelee
kushirikiana katika mipango wanayopanga na kukubaliana na kuitekeleza kwa
pamoja ili kufikia malengo yenye kiwango kinachokubalika na Mwajiri, sambamba
na utunzaji wa mazingira na miundombinu mbalimbali ya Mahakama.
Kwa upande wake Naibu Msajili wa Mahakama Kuu
ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa alisema kuwa,
atasimamia maelekezo na maono ya Mwajiri ili kuhakikisha shughuli za Mahakama
zinatolewa kwa mapema ipasavyo katika kila kituo.
“Nawapongeza watumishi wa Mahakama zote Kigoma
kwa uchapakazi wenu, hasa katika eneo la mashauri,” alisema Mhe. Mbwelwa na
kukiri kuwa anaridhishwa na usikilizwaji na umalizaji wa mashauri kwa Mahakama
zote, ambapo hakuna mashauri mlundikano.
Hata hivyo, Naibu Msajili huyo aliwataka
Watumishi kuendelea na kasi hiyo ili Mahakama Kigoma iendelee kuwa bora na
tofauti katika maeneo yote ya kiutendaji.
Naye, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka alisema kuwa, atasimamia maagizo yote katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama pamoja na maelekezo yote ya Viongozi wa juu wa Mahakama ya Tanzania ili kufikia lengo na tija katika utoaji haki mapema ipasavyo. Hata hivyo, alimuhakikishia Jaji Mfawidhi kuwa utunzaji wa miundombinu ya Mahakama na vitendea kazi, unakwenda.
Mahakama zilizokaguliwa ni Mahakama za Wilaya za Kigoma, Kasulu, Buhigwe, Kibondo na Uvinza pamoja Mahakama za Mwanzo Kasanda na Manyovu, zilizopo Wilaya ya Buhigwe.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile kikagua Mahakama ya Mwanzo Manyovu alipofanya ziara ya kikazi katika Mahakama hiyo hivi karibuni.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akisalimiana na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe alipofanya ukaguzi hivi karibuni. Anayesalimiana naye ni Bw. George Ilunga Kato, Mlinzi wa Mahakama ya Wilaya hiyo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine K. Rwizile (katikati) akizungumza jambo wakati wa ziara yake Mahakama ya Wilaya Buhigwe. Kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa na kushoto Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe, Mhe. Katoke Mwakitalu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akigusa mti
uliopandwa na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Tabora wa kipindi hicho mwaka 2001, Jaji Mstaafu, Mhe. Edward Rutakangwa, wakati wa ziara ya ukaguzi wa Mahakama Kibondo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akikagua orodha ya mashauri katika ubao wa matangazo, uliopo katika eneo la wateja kusubiria Mahakama ya Wilaya Uvinza. Pamoja naye kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa na katikati ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya uvinza.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (wa pili kulia) akipokea taarifa ya ukarabati wa Mahakama ya Mwanzo Kasanda kutoka kwa Ofisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Kakonko, Bw. Nehemiah Makoko, (kulia) wengine ni Viongozi Waandamizi wa Mahakama Kuu Kigoma walioambatana katika msafara wa Jaji Mfawidhi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Haki Jinai alioambatana nao kukagua Gereza la Mahakama ya Wilaya Kasulu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kibondo mara baada ya ukaguzi wake katika
Mahakama hiyo.
Picha ya pamoja. Katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (katikati), wa pili kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe.
Fadhili Mbelwa, wa kwanza kulia ni Mtendaji
wa Mahakama
Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka, wa pili kushoto ni Kaimu
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kakonko, Mhe. Magreth Rweyemamu wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kasanda Mhe.
Jonas Kilimba.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ni Mtendaji wa Mahakama Kuu
Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka, (kulia) ni Mwendesha Mashtaka
Mfawidhi wa Wilaya Uvinza, Bi. Edina Mkala na waliosimama ni Watumishi wa Ofisi
ya Taifa ya Mashtaka wa Wilaya hiyo mara baada ya kuzulu katika ofisi hiyo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni