Ijumaa, 17 Julai 2026

MAHAKAMA GEITA, SONGWE WABADILISHANA UZOEFU KWENYE MATUMIZI YA TEHAMA

Na MWANDISHI WETU-Mahakama, Geita

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Geita, Mhe. Projestus Kahyoza, tarehe 15 Julai, 2026 alipokea ugeni kutoka Mahakama Kuu Songwe, kwa lengo la kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji wa huduma za Mahakama.

Ziara ya Viongozi kutoka Mahakama Songwe iliongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Songwe, Mhe. Joyce Minde, akiwa ameambatana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Afisa Utumishi pamoja na watumishi wengine wa Mahakama hiyo.

Akifungua kikao hicho, Mhe. Kahyoza alisema kuwa kubadilishana uzoefu ni fursa muhimu ya kujifunza mbinu bora zinazoweza kuboresha utendaji kazi na kuimarisha utoaji wa huduma za haki kwa ufanisi, kwa wakati na kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia.

Aliwahimiza watumishi wa Mahakama Kuu Geita kuitumia kikamilifu fursa hiyo kwa kujifunza kutoka kwa wenzao wa Songwe na kushiriki kikamilifu katika mijadala.

"Kama una jambo la kuchangia au kuuliza, usisite kulisema. Lengo letu ni kujifunza kutoka kwa kila mmoja ili kuboresha huduma zetu," alisema Jaji Kahyoza.

Akizungumzia Mkoa wa Geita, Mhe. Kahyoza alisema kuwa licha ya kuwa ni Mkoa mchanga, una mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa kupitia shughuli za uchimbaji madini, kilimo, uvuvi na ufugaji. Aidha, alisema Mkoa huo umejaliwa vivutio mbalimbali vya utalii, ikiwemo Ziwa Victoria, Hifadhi ya Kigosi pamoja na urithi wa utamaduni.

Kuhusu matumizi ya TEHAMA mahakamani, Jaji Mfawidhi alieleza kuwa ni takwa la kisheria na kwamba Mahakama Kuu Geita ilianza rasmi kutekeleza mfumo wa Mahakama kidijiti tangu ilipoanzishwa tarehe 23 Desemba, 2023, kufuatia maelekezo ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wakati wa uzinduzi wa masjala hiyo.

Alisema Jaji Mkuu alielekeza Mahakama Kuu Geita kuanza shughuli zake kama Mahakama ya kidijiti (purely digital), bila kutumia karatasi. Aliongeza kuwa kufuatia maelekezo hayo, Masjala iliweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha matumizi ya TEHAMA yanatekelezwa kikamilifu.

Mikakati hiyo ilijumuisha kuendesha mafunzo ya ndani kwa watumishi, kufanya mikutano na wadau wa Mahakama, Viongozi wa Serikali pamoja na wananchi ili kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa kuondokana na matumizi ya karatasi katika utoaji wa huduma za Mahakama.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, Mhe. Fredrick Lukuna, aliwasilisha mada kuhusu matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (ECMS), akieleza namna mfumo huo unavyowezesha uendeshaji wa mashauri bila matumizi ya karatasi.

Alisema mfumo huo umeongeza ufanisi katika usimamizi wa mashauri kwa kuwezesha ufuatiliaji wa mwenendo wa kesi, kupunguza mlundikano wa mashauri, kuharakisha utoaji wa haki na kuimarisha uwazi katika shughuli za Mahakama.

Aidha, alieleza kuwa matumizi ya TEHAMA yameboresha utunzaji wa kumbukumbu za mashauri kwa kuondoa changamoto ya upotevu wa mafaili, kurahisisha upatikanaji wa hukumu na maamuzi kupitia hifadhidata, kuboresha usahihi wa takwimu za Mahakama pamoja na kupunguza muda na gharama za uendeshaji kupitia matumizi ya Mahakama pepe.

Akizungumza kuhusu mafanikio ya Taasisi, Mhe. Lukuna alisema kuwa ni muhimu kuwa na malengo yaliyo wazi na yanayopimika, kujenga timu yenye nidhamu, kusimamia muda kwa ufanisi na kuendelea kuwajengea uwezo watumishi kupitia mafunzo endelevu.

"Ni muhimu kudumisha mahusiano mazuri kazini, kujifunza kutokana na makosa yaliyopita, kubaini changamoto zinazochelewesha utendaji, kuhakikisha rasilimali muhimu zinapatikana na kuwa tayari kufanya maamuzi yatakayochochea mafanikio ya pamoja," alisema.

Naye Mtendaji wa Mahakama Geita, Bi. Masalu Kisasila, alieleza namna masjala hiyo ilivyoondokana na matumizi ya karatasi kwa kutumia mifumo ya kidijitali katika mawasiliano na utunzaji wa nyaraka.

Alisema hatua hiyo imeongeza ufanisi wa kazi, kupunguza gharama za ununuzi wa mafaili na vifaa vya kuhifadhia nyaraka, kuimarisha usalama wa taarifa kwa kupunguza hatari ya uvujaji wa taarifa, kurahisisha utoaji wa huduma kwa wateja na kuongeza ubunifu katika utendaji kazi.

Bi. Kisasila aliwashauri washiriki kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mifumo ya TEHAMA, kutoa motisha kwa watumishi na kuendelea kuendesha mafunzo ya ndani ili kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma.

Kwa niaba ya ujumbe kutoka Songwe, Mhe. Minde, alitoa shukrani kwa uongozi wa Mahakama Kuu ya Geita kwa mapokezi mazuri na mafunzo yenye tija yaliyotolewa wakati wa ziara hiyo.

Alimshukuru Jaji Mfawidhi, Naibu Msajili, Mtendaji pamoja na watumishi wote wa Mahakama Kuu ya Geita kwa ushirikiano waliouonyesha licha ya taarifa ya ujio wa ujumbe huo kutolewa kwa muda mfupi. Aidha, aliahidi kuwa maarifa na uzoefu walioupata vitatekelezwa na kusambazwa katika vituo vyao vya kazi ili kuboresha utoaji wa huduma za Mahakama.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, Mhe. Projestus Kahyoza, akiwakaribisha watumishi kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Songwe.


Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi (wa katikati) akihimiza kushiriki kikamirifu katika mafunzo ya kubadilishana uzoefu, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Geita, Mhe. Fredrick Lukuna, wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Songwe, Mhe. Joyce Minde.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, Mhe. Fredrick Lukuna, akitoa mada kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (ECMS) bila matumizi ya karatasi.

Mtendaji wa Mahakama Geita, Bi. Masalu Kisasila, akieleza mafanikio ya matumizi ya TEHAMA katika eneo la utawala.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Geita, Mhe. Mujuni Muchunguzi, akiwezesha mafunzo juu ya matumizi ya TEHAMA kwa upande mashauri na utawala katika ngazi ya Wilaya pasipo kutumia karatasi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu, Mhe. Ally Mgomba, akiwezesha mafunzo juu ya mfumo wa Mahakama ya Mwanzo unaotumika Geita.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, Mhe. Projestus Kahyoza (wa pili kushoto) akiwa na Naibu Msajili wa Mahakama Songwe, Mhe. Joyce Minde na watumishi wa Mahakama Songwe.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam.


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni