Na. ASHA JUMA-Mahakama Morogoro.
Mahakama
Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Morogoro, imefanya kikao cha menejimenti na uongozi kilicholenga kutathmini utendaji wa Mahakama, kujadili changamoto
mbalimbali pamoja na kuweka mikakati ya kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za
haki kwa wananchi.
Kikao hicho kilifanyika tarehe 17 Julai, 2026 katika ukumbi wa mikutano uliopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji
Haki (IJC) Morogoro, na kuongozwa na Jaji Mfawidhi, Mhe. Rose Ebrahim, ambaye alikuwa Mwenyekiti
wa kikao hicho.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Majaji wa
Mahakama Kuu Morogoro, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Morogoro, Mtendaji wa Mahakama Morogoro,
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mahakimu Wafawidhi
wa Mahakama za Wilaya, pamoja na Viongozi na Maafisa kutoka vitengo mbalimbali,
wakiwemo Maafisa Utumishi, Afisa TEHAMA, Afisa Ugavi na Mkaguzi wa Ndani.
Miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa ni tathmini
ya utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita, hususan kuhusu uboreshaji wa
miundombinu ya Mahakama. Kikao kilibaini kuwa changamoto zilizokuwa zikihusu
upatikanaji wa maji, umeme na huduma za mtandao katika baadhi ya Mahakama
zimefanyiwa kazi kwa kiwango kikubwa.
Aidha, kikao kilijadili namna ya kuboresha
utaratibu wa upokeaji wa taarifa kutoka Taasisi mbalimbali, ikiwemo Jeshi la Magereza,
pamoja na kufanya tathmini ya hali ya miundombinu katika Mahakama mpya ili
kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu kama maji, umeme na mawasiliano ya
mtandao kwa ajili ya kuongeza ufanisi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho,
Jaji Mfawidhi aliwataka Viongozi na Watumishi kuendelea kushirikiana katika kujenga mazingira bora ya kazi na
kuimarisha mawasiliano ndani ya Taasisi.
"Vikao hivi ni kama vikao vya kifamilia
au vya kitaasisi. Morogoro tunaamini katika uwazi na mawasiliano mazuri, hivyo
naomba ushirikiano wa Viongozi na Watumishi wote ili kwa pamoja tuendelee kuijenga Mahakama ya Morogoro
kuwa mfano wa utendaji bora," alisema Mhe. Ebrahim.
Akiwasilisha taarifa ya uongozi na utendaji,
Mtendaji wa Mahakama Morogoro, Bw. Ahmed Ngéni, alieleza hali ya majengo, utekelezaji wa miradi mipya pamoja na hali ya
vyombo vya usafiri katika Mahakama hiyo.
Aidha, alibainisha kuwa miongoni mwa changamoto
zinazoikabili Mahakama hiyo ni upungufu wa watumishi uliotokana na baadhi yao
kubadilishwa kada, hali ambayo imeathiri utekelezaji wa baadhi ya majukumu.
Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu
Morogoro, Mhe. Amiri Msumi, akiwasilisha taarifa ya hali ya mashauri,
alisisitiza matumizi sahihi ya mifumo ya uendeshaji wa mashauri, utunzaji wa
vielelezo na uingizaji wa taarifa sahihi katika mifumo mbalimbali ya uendeshaji
wa mashauri.
Mhe. Msumi alisema kuwa wanaendelea
kufanya vizuri katika kupunguza mashauri ya mlundikano, kwani mengi
yanamalizika kwa wakati na ipo haja ya kuandaa
mipango ya kimkakati ambayo itaweka mfumo wa kujitathmini, kurekebisha maeneo
yanayoonekana kuwa na mapungufu na kuboresha namna na kasi ya utekelezaji wa
majukumu yao.
”Nasisitiza kuwa jukumu
mama la Mahakama ni kusikiliza na kufanya maamuzi mapema iwezekanavyo ili
kuepusha mlundikano wa mashauri mahakamani, matumizi sahihi ya mifumo ya kielektroniki na tukumbuke kuingiza taarifa sahihi katika mifumo hiyo kwani taarifa
zisizo sahihi zinaweza kusababisha wananchi kukosa haki zao," alisema Mhe.
Msumi.
Akihitimisha kikao hicho, Jaji Mfawidhi aliwashukuru
Majaji, Mahakimu na Viongozi wote walioshiriki kikao hicho kwa michango yao. Aliwasisitiza
kuendelea kuzingatia misingi ya uongozi bora, uwajibikaji na kufuata taratibu
za kazi ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wananchi.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kudumisha upendo, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa Watumishi wa Mahakama, huku akiahidi kuandaa ratiba maalumu ya kufanya ukaguzi katika Mahakama zote zilizopo Morogoro ili kutambua na kutatua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim, akizungumza wakati wa kikao.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Morogoro, Mhe. Rose Ibrahim, (aliyekaa katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga (kushoto) na Mhe. Aisha Sinda (kulia).
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Morogoro, Mhe. Amiri Msumi, akisoma taarifa ya mashauri katika kikao hicho.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Janeth Kinyage, akichangia mada katika kikao hicho.
Mtendaji wa Mahakama Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni, akisoma taarifa ya utendaji katika kikao hicho.
Wajumbe wa kikao cha menejimenti ya Mahakama Morogoro wakifuatilia taarifa mbalimbali wakati wa kikao.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni