Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam
Naibu Msajili ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam Kisutu, Mhe. Franco Kiswaga amesema ubora wa Mahakama unapimwa na Watendaji kazi wake na si majengo pekee.
Mhe. Kiswaga aliyasema hayo tarehe 17 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke alipokuwa akifungua Mafunzo ya siku moja ya namna ya kupokea Ushahidi wa kieletroniki hususan kwa Mahakama za Mwanzo za Wilaya yaliyotolewa kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na Wilaya katika Wilaya za Temeke na Kigamboni.
Mhe. Kiswaga aliwakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa Mahakama haiwezi kuwa bora kuliko uwezo wa watendaji wake ambapo alisema, “ubora wa Mahakama ni namna watumishi wanavyowahudumia wananchi.”
Aliongeza kuwa, Wananchi hawawezi kuhudumiwa hewani
bila kuwa na elimu na maarifa na kadri wanavyojifunza ndio wanaimarisha
uaminifu wa wananchi kwa Mhimili wa Mahakama.
“Tunaishi zama ambazo teknolojia imebadili kila kitu, imebadili namna ya watu wanavyoishi, wanavyowasiliana na hata wanavyofanya biashara,” alisema Mhe. Kiswaga.
Aliongeza zaidi kwa kusema, “leo ushahidi unaoweza kuamua shauri unaweza kupatikana kupitia simu za mikononi, ujumbe mfupi mawasiliano ya WhatsApp, telegram, majukwaa mengine ya kidijitali CCTV rekodi za benki, miamala ya fedha kwa njia ya kielektoniki.”
Aidha, aliwapongeza Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya Temeke na Kigamboni kwa kuona umuhimu wa kuandaa mafunzo hayo ili kuboresha utendaji kazi na kuendana na mabadiliko ya Sheria ya Ushahidi katika Mahakama za Mwanzo (The Magistrates Courts (Rules of Evidence in Primary Courts) (Amendment) Regulation, 2026 GN No. 143 iliyoongeza kanuni ya 8A.
Baada ya kufungua mafunzo hayo Mhe. Kiswaga alitoa mada ya juu wa kaulimbiu ya Mahakama na kuifafanua namna ambavyo kama Maofisa wa Mahakama wanatakiwa kuiishi.
Kadhalika Naibu Msajili huyo alieleza kuwa, Kanuni za Maadili za Maofisa wa Mahakama zinajengwa juu ya misingi sita ambayo ni uhuru wa Mahakama, kutokuwa na upendeleo, uadilifu, mwenendo unaofaa, usawa na umahiri.
Alipokuwa akifafanua maana ya Uadilifu na Uwajibikaji,
Mhe. Kiswaga alieleza kuwa, Maofisa wa Mahakama kama Viongozi wanapaswa kujua
namna bora ya kuaminiana wao kwa wao, watumishi wengine wasio Mahakimu pamoja
na Wananchi.
Aliongeza kwa kusema kuwa, kama kuna mtumishi mwenye maadili yasiyofaa basi Viongozi wajitahidi kumbadili na kuwa naye karibu ili aweze kubadilika na Viongozi wasiathiriwe na matendo yake.
Naye, Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam Kisutu, Mhe. Romuli Mbuya alitoa mada juu ya uchukuaji, upokeaji na tathmini ya ushahidi wa kieletroniki hususan kwa Mahakama za Mwanzo kwa kuzingatia Kanuni ya 8A ya Kanuni za Ushahidi katika Mahakama za Mwanzo.
Mhe. Mbuya aliwasisitiza Mahakimu kusimamia mwenendo wa shauri wakati wa usikilizaji ikiwepo kumtaka Shahidi aweke msingi kwa kueleza chanzo cha ushahidi wake.
Aidha, katika Mafunzo hayo Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Temeke, Mhe. Frank Lukosi alitoa mada juu ya hatua za kuzingatia na namna ya kuendesha shauri la kuidharau Mahakama pale linapoibuka wakati wa usikilizwaji wa shauri.
Katika mafunzo hayo, Ofisa TEHAMA wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Tumaini Malima alipata wasaa wa kuwakumbusha
Mahakimu wa Mahakama za Wilaya juu ya mambo mbalimbali yaliyoboreshwa kwenye Mfumo
wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) ni pamoja kuwa na uwezo wa
kuandaa wito kwa mashahidi (Summons), eneo la kuandika adhabu (sentence),
sehemu ya kuweka vielelezo na kuandaa hati mbalimbali.
Pia katika Mfumo wa Mahakama za Mwanzo umeongeza watumiaji kwa mfano Polisi anaweza kufungua shauri Mahakama ya Mwanzo akiwa Polisi, lakini pia kwa mashauri ya madai mfumo utakuwa na uwezo wa kutengeneza namba za malipo (control number) na mashauri yatapewa namba kwenye mfumo na hii itapunguza matumizi ya rejesta ngumu.
Mfumo huo bado haujaanza kutumika, pindi utakapoanza kutumika matumizi ya karatasi na rejesta ngumu utapungua kwa kiwango kikubwa.
Alipokuwa akitoa neno la ukaribisho Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Temeke, Mhe. Vicky Mwaikambo alisema kuwa, wameandaa mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kuendana na mabadiliko ya Sheria ya Ushahidi yaliyofanyika hivi karibuni.
Akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Naibu Msajili, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kigamboni, Mhe. Mwanakombo Twalib aliishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuziruhusu Mahakama za Mwanzo kuweza kupokea ushahidi wa kielekroniki, kwani kwa sasa matumizi ya ushahidi huo hayakwepeki katika mfumo mzima wa utoaji haki.
Mafunzo hayo pia yaliwahusisha watumishi waliofanyiwa
mabadiliko ya kada na kuwa Mahakimu kutoka Wilaya ya Temeke na Kigamboni ambapo
mafunzo hayo yatawasaidia watakapopangiwa vituo vya kazi.
Sambamba na mafunzo hayo Mahakamu hao walipata wasaa wa kuwapongeza na Mahakimu waliofanyiwa mabadiliko ya kada kuwa Mahakimu kwa kukata keki maalum iliyoandaliwa ikiwa ni ishara ya upendo.
Naibu Msajili ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam Kisutu, Mhe. Franco Kiswaga akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya namna ya kupokea Ushahidi wa kieletroniki hususan kwa Mahakama za Mwanzo za Wilaya yaliyotolewa kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na Wilaya katika Wilaya za Temeke na Kigamboni kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Temeke, Mhe. Vicky Mwaikambo akitoa neno wakati wa mafunzo hayo.
Naibu Msajili kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam-Kisutu, Mhe. Romuli Mbuya akitoa mafunzo ya
namna ya uchukuaji, upokeaji na tathmini ya Ushahidi wa Kielektroniki.
Ofisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaama Bw. Tumain Malima akiwakumbusha Mahakimu namna ya kutumia Mfumo na kuwaeleza baadhi ya maboresho yaliyofanyika katika mfumo wa kusikiliza mashauri.










Hakuna maoni:
Chapisha Maoni