Jumatatu, 20 Julai 2026

WATUMISHI MAHAKAMA KUU DIVISHENI YA ARDHI WAMUAGA JAJI MANDIA

  • Wamkaribisha pia Jaji Otaru

Na DHILLON UISSO – Mahakama Ardhi Dar es Salaam

Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, tarehe 17 Julai, 2026 walishiriki katika hafla ya kumuaga aliyekuwa Jaji Nehemia Mandia, Jaji, aliyehamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.

Katika hafla hiyo, Waumishi pia walimkaribisha Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Monica Otaru, ambaye amehamia Divisheni ya Ardhi, maarufu udongoni.

Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi na kuhudhuriwa na Kaimu Jaji Mfawidhi, Mhe. Arafa Msafiri na baadhi ya Majaji na Naibu Wasajili, Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, pamoja na Watumishi.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Msafiri alimpongeza Mhe. Mandi kwa ushirikiano, upendo na mchango mkubwa kipindi chote alichohudumu katika Divisheni ya Ardhi.

“Tunakupongeza sana Mhe. Mandia kwa uchapakazi, upendo na ushirikiano wako na ukawe balozi wetu huko. Wewe bado ni mwana udongoni,” alisema.

Kaimu Jaji Mfawidhi alitumia fursa hiyo kumkaribisha Mhe. Otaru kwa kujiunga na timu ya Divisheni ya Ardhi yenye upendo na ushirikiano mkubwa.

“Najua wewe ni mchapakazi na mwenye upendo mkubwa, karibu sana kwenye familia ya udongoni. Tutakupa ushirikiano na “team work,” Mhe. Msafiri alisema.

Kwa upande wake, Mhe. Mandia alitoa shukrani kwa Majaji, Viongozi wengine na watumishi wote aliobahatika kufanya nao kazi kwa kipindi chote. Alisema ushirikiano, upendo na mshikamano alioupata kutoka kwao ulichangia mafanikio yake katika kazi za kila siku.

Aliwaasa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, bidii na uaminifu, akisisitiza kuwa mafanikio katika utumishi yanatokana na kuipenda kazi na kutimiza wajibu kwa moyo wa kujituma.

Naye Mhe. Otaru alitoa neno la kushukuru kwa kukaribishwa na kuanza kushughulikia majalada kwa kasi na ushirikiano kutoka kwa Majaji, Viongozi na Watumishi kwa ujumla na kufanya kazi yake kuwa rahisi.

Majaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Nehemia Mandi na Mhe. Monica Otaru, wakikata keki.


Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Monica Otaru akitoa neno.

Kaimu Jaji Mfawidhi, Mhe. Arafa Msafiri, akimkabidhi Mhe. Mandia zawadi.

Majaji wa Mahakama Kuu wakifurahia jambo wakati wa hafla hiyo.

 Watumishi wa Divisheni ya Ardhi wakiwa kwenye hafla hiyo.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni