Jumanne, 21 Julai 2026

WANAFUNZI MWEKA WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO MAHAKAMA YA WILAYA YA BABATI

Na. CHRISTOPHER MSAGATI- Mahakama, Manyara

Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro wamefanya ziara ya kujifunza taratibu mbalimbali za kimahakama katika katika uendeshaji wa mashauri yanayohusu uendeshaji wa mashauri yanayohusu wanyamapori.

Mafunzo hayo yanaendeshwa katika ukumbi namba Tatu wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara ambao unatumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Babati katika kuendesha shughuli za Mahakama.

Katika ziara hiyo, jumla ya wanafunzi Hamsini na nane (58) kutoka Chuo hicho waliambatana na walimu wao wanne (4) kwa lengo la kujifunza taratibu na masuala mbalimbali yanayotokea mahakamani kwa njia ya vitendo mtandao ili ziweze kuwasaidia katika elimu yao wanayojifunza chuoni.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Charles Mnzava, aliwasihi wanafunzi hao kuzingatia yale yote ambayo watafundishwa na wataalamu wa masuala ya kisheria ili yaweze kuwasaidia katika masomo yao ya chuoni na hata katika maisha ya baada ya chuo pale ambapo watakuwa wameajiriwa au kujiajiri katika maeneo mbalimbali.

“Chuoni mnasoma zaidi kwa nadharia, nawapongeza kwa kuja leo na kushuhudia namna mashauri haya yanayohusu wanyamapori na nyara za Serikali yanavyoendeshwa mahakamani. Mafunzo haya yatawaongeza tija na uelewa wenu zaidi katika hayo mnayojifunza chuoni na hata baadae mtakapokuwa katika ajira zenu” alisema Mhe. Mnzava.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mnzava alitumia nafasi hiyo kuwafundisha wanafunzi hao juu ya Muundo wa Mahakama Tanzania ulivyo. “Mahakama zetu hapa nchini, kuanzia Mahakama ya Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu Pamoja na Mahakama ya Rufani zina taratibu zake za usikilizwaji wa mashauri kulingana na uzito wa mashauri husika hivyo ni vema mkafahamu kuwa hata haya mashauri ya Wanyamapori mathalani hayawezi kusikilizwa katika ngazi za Mahakama za Mwanzo”.

Aidha, wanafunzi wa chuo hicho cha Mweka waliweza kuhoji na kujibiwa maswali mbalimbali kwa wawezeshaji wa Mafunzo hayo ambao walikuwa ambaye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati, Mhe. Victor Joseph Kimaro pamoja na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Mhe. Martin Massao.

Akishukuru baada ya mafunzo hayo Mwakilishi wa Walimu waliombatana na wanafunzi hao Mwalimu Melckezedeck Tarimo alishukuru uongozi wa Mahakama Kuu Manyara kwa kuwapokea vema na kuwapa Elimu waliyokuwa wakiihitaji.

“Tunashukuru sana Uongozi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara kwa kutupokea na kwa ushirikiano mliotupa, tuaamini kuwa elimu hii itatusaidia sana na tutaendelea kuja hapa kwa ajili ya mafunzo mengine,” alisema Mwalimu Tarimo.

Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara imeendelea na utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi wanaofika mahakamani kila wakati lakini pia kwa kupitia vyombo vya Habari vilivyopo hapa mkoani kwa lengo la kutimiza mahusiano bora kati ya Mahakama na wadau wanaosaidia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Mahakama.

Walimu na wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara walipohudhuria mafunzo katika Mahakama ya Wilaya ya Babati.

Sehemu ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka wakaifuatilia mada zilizokuwa zinafundishwa wakati wa mafunzo yaliyokuwa yakitolewa kwa wanafunzi wao kutoka kwa Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Babati.

Mmoja wa wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka akichangia mada wakati wa mafunzo yaliyokuwa yakitolewa kwa wanafunzi wao kutoka kwa Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Babati.

Walimu wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka (waliosimama) wakifuatilia mafunzo yaliyokuwa yakitolewa kwa wanafunzi wao kutoka kwa Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Babati.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati Mhe. Martin Massao akiendelea na mafunzo kwa Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka waliofika katika Mahakama ya Wilaya ya Babati kwa ajili ya Mafunzo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati Mhe. Victor Kimario (mwenye suti ya rangi ya buluu) akiendelea na mafunzo kwa Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka waliofika katika Mahakama ya Wilaya ya Babati kwa ajili ya Mafunzo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Charles Mnzava (aliyevaa suti nyeusi) akitoa Neno la Ukaribisho kwa Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka waliofika katika Mahakama ya Wilaya ya Babati kwa ajili ya Mafunzo.



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni