Jumatano, 22 Julai 2026

MAHAKAMA MANYARA YAENDELEA KUTOA MAFUNZO KWA WANAFUNZI TASNIA YA WANYAMAPORI

Na. CHRISTOPHER MSAGATI- Mahakama, Manyara

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Manyara kupitia Mahakama ya Wilaya ya Babati imeendelea kuwapokea Wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya Usimamizi wa Wanyamapori ikiwa ni pamoja na wanafunzi kutoka Chuo cha Wanyamapori Pasiansi cha jijini Mwanza waliofika mahakamani hapo kwa ajili ya mafunzo ya uendeshaji wa mashauri yanayohusu Wanyamapori.

Katika mafunzo hayo, jumla ya wanafunzi 149 kutoka Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi kutoka Mwanza wakiwa wameambatana na walimu wao watatu (3) wamefika kwa lengo la kujifunza taratibu za kisheria na masuala mbalimbali yanayotokea mahakamani kwa njia ya Mahakama mtandao ili njia hizo iweze kuwasaidia katika masomo wanayojifunza chuoni.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe. Charles Mnzava, aliwasihi wanafunzi hao kuzingatia yale yote ambayo watafundishwa na wataalamu wa masuala ya kisheria ili yaweze kuwasaidia katika masomo yao chuoni na hata katika maisha baada ya chuo pale ambapo watakuwa wameajiriwa au kujiajiri katika maeneo mbalimbali.

“Chuoni mnasoma zaidi kwa nadharia, nawapongeza kwa kuja leo na kushuhudia namna mashauri haya yanayohusu wanyamapori na nyara za Serikali yanavyoendeshwa Mahakamani. Mafunzo haya yataongeza tija na uelewa wenu zaidi katika hayo mnayojifunza chuoni na hata baadae mtakapokuwa katika ajira zenu.” alisema Mhe. Mnzava.

“Pamoja na hayo tunawapongeza kwa kuchagua Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara kwa ajili ya kupata mafunzo haya. Kwetu Mahakama ni furaha kubwa sana kuweza kuunganisha Taasisi mbili kama mlivyokuja jana na leo kwa ajili ya mafunzo haya ya kimahakama na hususan namna ya uendeshaji na usikilizaji wa mashauri yanayohusu wanyamapori,” ameongeza Mhe. Mnzava

Katika hatua nyingine, Mhe Mnzava alitumia nafasi hiyo kuwafundisha wanafunzi hao juu ya Muundo wa Mahakama ya Tanzania ulivyo. “Mahakama zetu hapa nchini, kuanzia Mahakama ya Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu Pamoja na Mahakama ya Rufaa zina taratibu zake za usikilizwaji wa mashauri kulingana na uzito wa mashauri husika hivyo ni vema mkafahamu kuwa hata haya mashauri ya Wanyamapori mathalani hayawezi kusikilizwa katika ngazi za Mahakama za Mwanzo”.

Aidha, wanafunzi wa Taasisi hizo waliweza kuhoji na kujibiwa maswali mbalimbali kwa wawezeshaji wa Mafunzo hayo ambao walikuwa ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati Mhe. Victor Joseph Kimaro pamoja na Mahakimu Wakazi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati Mhe. Martin Massao na Mhe. Jumaa Mwambago.

Akishukuru baada ya mafunzo hayo Mwakilishi wa Walimu waliombatana na wanafunzi hao kutoka Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi Mwalimu Hamisi Philimon Matinde, alishukuru uongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara kwa kuwapokea vema na kuwapa Elimu waliyokuwa wakiihitaj.

“Tunashukuru sana Uongozi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara kwa kutupokea na kwa ushirikiano mliotupa, tuaamini kuwa elimu hii itatusaidia sana na tutaendelea kuja hapa kwa ajili ya mafunzo mengine,” alisema Mwalimu Matinde.

Utaratibu wa kutoa Elimu, unaendelea kufanyika kwa kuwawezesha wanafunzi na wanataaluma mbalimbali kutoka Taasisi za Elimu kujifunza masuala mbalimbali kama walivyofanya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka Pamoja na Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi Mwanza.

Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka wakiwa katika picha ya Pamoja na walimu wao na watumishi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara mbele ya jengo la Mahakama Kuu Manyara.

Mahakimu Wakazi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati Mhe. Martin Massao (aliyesimama kushoto) na Mhe. Jumaa Mwambago wakifuatilia mafunzo yaliyokuwa yanatolewa kwa Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka Pamoja na Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi.

Wanafunzi wa Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi wakiwa katika picha ya Pamoja na walimu wao na watumishi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara mbele ya jengo la Mahakama Kuu Manyara.

Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka Pamoja na Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi, Mwanza wakifuatilia mada ambazo zilikuwa zinatolewa katika Ukumbi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati.

Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka Pamoja na Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi, Mwanza wakifuatilia mada ambazo zilikuwa zinatolewa katika Ukumbi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati.




Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Charles Mnzava (wa kwanza kushoto) na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati Mhe. Victo Kimario wakiendelea kutoa Elimu kwa wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka Pamoja na Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi, Mwanza (hawapo pichani) walipofika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara kupata mafunzo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni