Na HABIBA MBARUKU – Mahakama Dar es Salaam
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, amesema
kuwa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya usuluhishi na upatanishi, unapaswa
kutambuliwa kama sehemu muhimu ya mfumo wa utoaji haki nchini.
Mhe.
Siyani ameyasema hayo leo tarehe 22 Julai, 2026, katika hotuba aliyoisoma kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Nane
wa Mwaka wa Taasisi ya Wasuluhishi Tanzania (TIArb) na Wiki ya Usuluhishi ya
Dar es Salaam (DAR Arbitration Week) ya mwaka 2026 uliofanyika kwenye ukumbi wa
mikutano wa Hoteli ya Delta jijini Dar es Salaam.
Ameeleza
kuwa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaielekeza Mahakama kukuza na
kuimarisha utatuzi wa migogoro miongoni mwa wahusika wa migogoro kama
ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, hivyo usuluhishi na upatanishi unapaswa kutazamwa kama mwendelezo wa
jukumu la Mahakama katika utoaji wa haki ndani ya mfumo wa utawala wa sheria.
"Utoaji
wa haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umepewa Mahakama. Hata hivyo,
mamlaka hiyo haiwazuii wahusika wa mgogoro kutafuta haki kwa njia nyingine
walizokubaliana, kama inavyoainishwa katika Ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inaielekeza Mahakama kukuza na
kuimarisha utatuzi wa migogoro miongoni mwa watu wanaohusika katika migogoro
hiyo,” amesisitiza Mhe. Siyani.
Amesema
mifumo ya jadi ya utatuzi wa migogoro iliyokuwepo kabla ya ukoloni, iliyojengwa
katika misingi ya maridhiano na maelewano, bado ina mchango mkubwa katika
maendeleo ya mifumo ya kisasa ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya Usuluhishi, huku
akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mifumo hiyo inaendana na mazingira ya
Tanzania na inayokidhi viwango vya kimataifa.
"Uhalali
wa mfumo wowote wa utatuzi wa migogoro hautegemei tu uhalali wake wa kisheria,
bali pia kukubalika kwake na jamii pamoja na kuendana kwake na mila na utamaduni
wa wananchi. Kwa hiyo, mustakabali wa mifumo ya Usuluhishi/upatanishi nchini
Tanzania unapaswa kuwa shirikishi, ukichota mema kutoka katika mila na desturi
mbalimbali huku ukizingatia misingi ya haki, kutopendelea upande wowote na
utawala wa sheria,” amesema Jaji Kiongozi.
Aidha,
ameeleza kuwa, usuluhishi na upatanishi havipaswi kuonekana kama njia
zinazotumika pale Mahakama zinapokuwa na mlundikano wa mashauri, bali ni
miongoni mwa njia kamili za utoaji haki zilizoidhinishwa na Katiba na Sheria za
nchi, zenye uwezo wa kusaidia upatikanaji wa haki mapema ipasavyo.
Amebainisha
kuwa, katika kipindi ambacho Tanzania inaendelea kushuhudia ongezeko la
uwekezaji katika miundombinu, Sekta ya Nishati, rasilimali asilia na biashara
za kimataifa, mifumo ya Usuluhishi na Upatanishi ina nafasi muhimu katika
kushughulikia migogoro yenye thamani kubwa na masuala ya kitaalamu kwa ufanisi,
kuongeza uhakika wa mazingira ya biashara na kuimarisha imani ya wawekezaji.
Mhe.
Siyani ameeleza kuwa, pamoja na uhuru wa mchakato wa usuluhishi, Mahakama
inaendelea kuwa na jukumu la kuhakikisha taratibu za usuluhishi zinafuatwa,
tuzo za usuluhishi zinatekelezwa, maslahi ya umma yanalindwa na mfumo wa sheria
unabaki kuwa thabiti kwa kuwa Mahakama na usuluhishi ni mifumo inayokamilishana
katika kufanikisha utoaji haki.
Aidha,
amewataka Wadau wa Sekta ya Sheria kuendelea kuimarisha uwezo wa kitaaluma,
kutumia teknolojia katika uendeshaji wa mashauri ya usuluhishi, kuendeleza
utaalamu katika sekta mbalimbali na kuoanisha mifumo ya ADR na viwango vya
kimataifa ili kuiwezesha Tanzania kujijengea nafasi kama kitovu cha usuluhishi kimataifa.
Pamoja
na hayo, Jaji Kiongozi amewahimiza washiriki kutumia mkutano huo kujifunza,
kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza matumizi ya
Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala nchini.
Katika
hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Hamza Johari, ametaja hatua
mbalimbali zinazofanywa na Ofisi hiyo huku akisisitiza kuwa haki inapaswa
kupatikana mapema ipasavyo.
Pamoja
na hayo, amewataka kuzingatia R4 za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambazo ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na
Kujenga Upya.
Kwa
upande wake Rais wa Taasisi ya Wasuluhishi Tanzania (TIArb) Wakili Aderickson
Njunwa, ameeleza kuwa, Taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1997, imebeba dhima
kubwa ya kuisaidia jamii kutatua migogoro kwa njia ya upatanishi, kadhalika
kukuza uwekezaji na kuimarisha uchumi endelevu.
Wakili Njunwa amefafanua kuwa miongoni mwa majukumu mengine ya (TIArb) ni kuhakikisha kuwa jamii ya Tanzania inapata elimu kuhusu maana ya usuluhishi na umuhimu wake kwa maendeleo endelevu pamoja na kuendeleza uwajibikaji kwa kujengeana uwezo na majukumu ya kitaasisi.
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani,
akifungua Mkutano wa Nane wa Mwaka wa Taasisi ya
Wasuluhishi wa Tanzania (TIArb) na Wiki ya Usuluhishi ya Dar es Salaam (DAR
Arbitration Week) mwaka 2026 kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju uliofanyika leo tarehe 22 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Delta jijini Dar es Salaam.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Hamza Johari akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Nane wa Mwaka wa Taasisi ya Wasuluhishi wa Tanzania (TIArb) na Wiki ya Usuluhishi ya Dar es Salaam (DAR Arbitration Week) mwaka 2026.
Sehemu ya washiriki waliohudhuria katika ufunguzi wa mkutano huo wakifuatilia kinachojiri.
Meza
kuu ikiongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher
Mohamed Siyani (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja. Wa pili kulia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Hamza Johari, wa pili kushoto ni Rais wa Taasisi ya Wasuluhishi Tanzania (TIArb), Wakili Aderickson Njunwa, wa kwanza kushoto ni Makamu wa Rais wa Taasisi ya
Wasuluhishi Tanzania (TIArb), Wakili Usaje Mwambene na wa kwanza kulia ni Meneja
wa Uwekezaji wa Taasisi hiyo, Bw. Daudi Riganda.
Rais
wa Taasisi ya Wasuluhishi Tanzania (TIArb), Wakili Aderickson Njunwa akizungumza
kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, wakati wa
ufunguzi wa Mkutano wa Nane wa Mwaka wa Taasisi ya Wasuluhishi wa Tanzania
(TIArb) na Wiki ya Usuluhishi ya Dar es Salaam (DAR Arbitration Week) mwaka 2026
uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Delta jijini Dar es Salaam.












Hakuna maoni:
Chapisha Maoni