Alhamisi, 30 Julai 2026

MWANASHERIA WA SERIKALI MFAWIDHI KIGOMA AJITAMBULISHA RASMI KWA JAJI MFAWIDHI, MHE. RWIZILE

  • Aahidi kudumisha ushirikiano na Mahakama mkoani humo

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Mwanasheria wa Serikali Mfawidhi wa Mkoa wa Kigoma, Bw. Said Seni amefanya ziara ya heshima ya kumtembelea Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile lengo likiwa ni kujitambulisha rasmi na kuimarisha ushirikiano wa kikazi katika utoaji haki mkoani humo.

Ziara hiyo imefanyika leo tarehe 29 Julai, 2026 katika Ofisi za Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma ambapo Mwanasheria huyo aliambatana na Wakili  wa Serikali Mfawidhi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Mkoa wa Kigoma, Bw. George Kalenda pamoja na Mfawidhi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mfawidhi Mkoa wa Kigoma, Bw. Waziri Magumbo.

Aidha, wakati wa mazungumzo ya Viongozi hao walijadili masuala mbalimbali yanayohusu upatikanaji haki, ikiwemo kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri na kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani.

Vilevile, walisisitiza juu ya umuhimu wa kuendelea kudumisha nidhamu, weledi na uwajibikaji katika mnyororo mzima wautoaji haki mapema ipasavyo.

Aidha, Mhe. Rwizile amewakaribisha Viongozi hao na kuwapongeza kwa hatua ya kufanya ziara hiyo ya kumtambulisha Mwanasheria Mkuu Mfawidhi Mkoa wa Kigoma, huku akisisitiza kuwa na ushirikiano wa karibu baina ya Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) ni nguzo kuu katika kuhakikisha haki inatendeka mapema ipasavyo na kwa haki kwa kila mwananchi.

“Mahakama Kigoma itakupa ushirikiano ili utimize wajibu wako katika mnyororo wa haki, hivyo utakapobaini changamoto yoyote inayohitajika kutatuliwa na Mahakama basi usisite kuileta kwa ajili ya kutatuliwa kabla haijaathiri mnyororo wa kutoa haki mapema ipasavyo kwa kila mwananchi,” amesema,  Jaji Rwizile.

Kwa upande wake, Mwanasheria huyo Mfawidhi  wa Mkoa Kigoma, Bw. Said Seni amesema, anaishukuru mamlaka yake kumpangia kazi mkoani Kigoma, kwani amekutana na watu wema, wakarimu na wenye ari ya kufanya kazi kwa weledi na kujituma.

Amesema kuwa, anayo imani kwamba atapata ushirikiano wa kutosha katika kutimiza wajibu wake katika kipindi chote atakachokuwa katika ofisi hiyo Mkoani Kigoma.

Kadhalika, Mwanasheria huyo amemuahidi Jaji Mfawidhi kuwa, atafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na kuhakikisha amri za Mahakama zinatekelezwa kwa wakati na kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Ameongeza kwamba, Ofisi hiyo ni mpya katika Mkoa wa Kigoma imeanzishwa kwa lengo la kuongeza nguvu ili kuisaidia Mahakama kutenda haki mapema ipasavyo, kupitia kutimiza wajibu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa, Mtendaji wa Mahakama, Bw. Yusuph Kasuka. 

Ziara hiyo imelenga kuimarisha mahusiano ya kikazi na ushirikiano baina ya Mhimili wa Mahakama na Taasisi za usimamizi wa sheria na uendeshaji wa mashtaka mkoani Kigoma, ili kuhakikisha mashauri yanashughulikiwa kwa ufanisi na mapema ipasavyo kwa maslahi ya wananchi kwa ujumla.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (aliyeketi mbele) akifanya mazungumzo na Ujumbe wa Mwanasheria wa Serikali Mfawidhi wa Mkoa wa Kigoma ulipomtembelea  ofisini kwake Mahakama Kuu Kigoma leo tarehe 30 Julai, 2026.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akitoa neno kwa wageni wake katika maongezi yaliyofanyika katika ofisi yake iliyopo katika jengo la Mahakama Kuu Kigoma.

Mwanasheria wa Serikali Mfawidhi wa Mkoa wa Kigoma, Bw. Said Seni akitoa neno la shukrani kwa Jaji Mfawidhi na Viongozi wengine wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma kwa mapokezi mazuri.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akitoa utambulisho wa Viongozi waliofika katika Ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile leo tarehe 30 Julai, 2026.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi akifurahia jambo alipokuwa akizungumza na Viongozi na Wadau wa Haki Jinai waliofika ofisini kwake kumsabahi na wakimtambulisha Mwanasheria wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Kigoma, Bw. Said Seni.


Wakili wa Serikali Mfawidhi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Mkoa wa Kigoma,  Bw. George Kalenda akisikiliza kwa makini wakati Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile, alipokuwa akitoa neno wakati wa mazungumzo yao leo tarehe 30 Julai, 2026.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile  (wa tatu kulia) akiwa pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa (wa tatu kushoto), Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka (wa kwanza kushoto), Mwanasheria wa Serikali Mfawidhi wa Mkoa wa Kigoma, Bw. Said Seni, (wa wa pili kulia), Mfawidhi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) Mkoa wa Kigoma, Bw. Waziri Magumbo (wa kwanza kulia) na Wakili wa Serikali Mfawidhi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Mkoa wa Kigoma, Bw. George Kalenda.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi (aliyeketi mbele) akitoa neno kwa Viongozi waliofika ofisini kwake kwa ajili ya utambulisho wa Mwanasheria wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Kigoma, Bw. Said Seni.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni