Na. CHRISTOPHER MSAGATI- Mahakama, Manyara
Uongozi
wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara kupitia kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama
hiyo Mhe. Dkt. Adam Mambi umekabidhiwa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya
Mwanzo huku makabidhiano hayo yakifanywa na Viongozi pamoja na Wananchi wa Kata
ya Lengatei iliyopo katika Tarafa ya Kijungu, wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara.
Eneo
hilo lilikabidhiwa rasmi na Viongozi na wananchi wa Kata hiyo, wakati
wakimpokea Mhe. Dkt. Mambi alipofanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama katika
eneo hilo mnamo tarehe 27 Julai, 2026.
Aidha,
wananchi na viongozi hao wameonesha uhitaji wa Mahakama ya Mwanzo katika eneo
lao kwa kuwa, kwa sasa wanapata changamoto kusafiri kwenda mpaka Mahakama ya
Mwanzo Kijungu kupata huduma za kimahakama ambapo kuna umbali wa Kilometa zaidi
ya 12 kutoka kwenye Kata hiyo.
Akizungumza
wakati wa mapokezi ya Kiwanja hicho, Mhe. Dkt. Mambi aliwashukuru viongozi
pamoja na wananchi hao kwa kutoa kiwanja hicho kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama
ya Mwanzo itakayo wasaidia wananchi kurahishisha kutoa huduma za kimahakama
katika Kata hiyo na maeneo ya jirani.
“Tunawashukuru
sana kwa kuwa mmeuona umuhimu wa Mhimili wa Mahakama katika dhima nzima ya utoaji
wa haki mpaka mkaamua kutoa kiwanja hiki. Tunaahidi kushirikiana nanyi bega kwa
bega mpaka tutakapokamilisha ujenzi wa Mahakama hii, naahidi ushirikiano kutoka
kwa Mahakama ili shughuli hii ikamilike mapema,” alisema Mhe. Dkt. Mambi.
Akizungumza
wakati wa kukabidhi kiwanja hicho, Afisa Mtendaji wa Kata ya Lengatei Bw. Julius
Kelato kwa niaba ya viongozi na wananchi wa kata hiyo, alishukuru uongozi wa
Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara kwa kufika katika maeneo hayo na kuahidi
kuanza mchakato wa ujenzi mara baada ya mchakato wa upatikanaji wa hati
utakapokamilika.
“Tukishamaliza
suala la upatikanaji wa hati ya kiwanja hiki, tumekusudia kuanza ujenzi wa
Mahakama hii kwa kutumia nguvu za wananchi wetu kama ambavyo tumekuwa tukifanya
kwa taasisi nyingine za Serikali,” alisema Bw. Kelato,
Katika
hatua nyingine, Mhe. Dkt. Mambi na timu yake ya ukaguzi walitembelea katika
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Wilaya, Mhe.
Fakii Lulandala ambapo Mhe. Dkt. Mambi, alimuomba Mkuu wa Wilaya asaidie katika
zoezi la upatikanaji wa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo ikiwa
ni pamoja na upatikanaji wa hati za umiliki wa viwanja hivyo ili kuepusha
migogoro isiyo ya lazima wakati wa matumizi yake.
Naye,
Mhe. Lulandala aliahidi kufanya hayo. “Siku zote, tumekuwa tukishirikiana na
Mahakama katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo na hususan katika kusaidia
upatikanaji wa haki na amani katika maeneo yetu. Kwa sababu hizo ninakuahidi
Mhe. Jaji kuwa, nitajitahidi kuwasaidia katika suala hili,” alisema Mhe.
Lulandala.
Jaji
Mfawidhi Mhe. Dkt. Mambi akiwa wilayani Kiteto alifanikiwa kukagua Mahakama ya
Wilaya ya Kiteto, pamoja na Mahakama za Mwanzo Kibaya, Dosidosi na Kijungu. Kwa
upande wa Wilaya ya Simanjiro, alikagua Mahakama ya Wilaya Simanjiro, Mahakama
za Mwanzo Engasmet, Shambarai na Msitu wa Tembo.
Aidha,
akiwa wilayani Simanjiro Mhe. Dkt. Mambi alipewa na kupokea ahadi kutoka kwa wananchi
wa Kata ya Msitu wa Tembo kupitia viongozi wao walioahidi kuanza ujenzi wa
Mahakama ya Mwanzo katika eneo lao kama walivyoahidi wananchi wa Kata ya Lengatei
wilayani Kiteto.
Viongozi
wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (wa tano kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja na
Viongozi na wananchi wa Kata ya Lengatei wilayani Kiteto walipotembelea kiwanja
ambacho kimetolewa na wananchi wa Lengatei kwa Uongozi wa Mahakama, Masjala Ndogo
ya Manyara kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo katika eneo hilo.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (aliyesimama)
akiwa anazungumza na viongozi na wananchi wa Kata ya Lengatei alipowatembelea ofisini
kwao wakati wa ziara ya Ukaguzi wa Mahakama wilayani Kiteto. Wengine ni Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe Charles Mnzava (kulia) na
kushoto ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kiteto Mhe. Aron
Losioki.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (kulia)
akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mhe. Fakii Lulandala mara baada ya
kumtembelea Mkuu huyo wa Wilaya katika Ofisi yake.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi akisalimiana
na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Shambarai iliyopo Wilayani Simanjiro mara
baada ya kufika Kituoni hapo kwa ajili ya Ukaguzi.
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Shambarai iliyopo Wilayani Simanjiro
akisoma taarifa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya
Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi na viongozi wengine waliofika kituoni hapo kwa
ajili ya ukaguzi (hawapo pichani)
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (katikati mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya Simanjiro, mbele ya Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro ambalo linaendelea kujengwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi, akisalimiana na sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Kiteto mara baada ya kuwasili kituoni hapo kwa ajili ya Ukaguzi wa Mahakama.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi
(aliyenyoosha mkono) akizungumza na sehemu ya viongozi na wananchi wa Kata ya
Msitu wa Tembo, Wilayani Simanjiro mara baada ya kufika katika Mahakama ya
Mwanzo Msitu wa Tembo kwa ajili ya Ukaguzi.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni