Na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama-Dodoma
Chama
cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Dodoma chini ya Mwenyekiti wake,
Mhe. Faisal Kahamba hivi
karibuni walifanya kikao cha wanachama wote kilicholenga kujadili maendeleo ya
tawi hilo, kuimarisha mshikamano wa wanachama pamoja na kujengeana uwezo katika
utekelezaji wa majukumu ya kimahakama
Kikao
hicho kilichohudhuriwa na wanachama wa TMJA kutoka Mahakama mbalimbali za Mkoa
wa Dodoma kilifanyika kwenye Ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo
Dodoma.
Miongoni
mwa ajenda muhimu za kikao hicho ilikuwa ni kuwapokea Wanachama wapya 11 wakiongozwa na Mlezi mpya wa TMJA Dodoma ambae ni Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga
ambaye amehamishiwa katika Kituo hicho hivi karibuni akitokea Mahakama Kuu Masjala
Ndogo Mbeya.
Akizungumza
wakati akitoa salamu zake, Jaji Mfawidhi na Mlezi wa TMJA Dodoma, Mhe. Tiganga alisema,
“ninafurahi kuwa sehemu ya familia hii lakini pia niwashukuru Viongozi kwa
kuandaa kikao hiki muhimu kwangu mimi ni kikao muhimu sana kwani karibia
wanachama wote mmekuja na tumeonana, niwapongeze kwa umoja huu sio kitu rahisi
kupata wajumbe wengi namna hii, wote tunafahamu umuhimu wa kuwa na chama
kilicho hai na chenye malengo yanayotekeleza wanachama wenye utayari wa
kutekeleza malengo hayo.”
Amesisitiza
kuwa, pamoja na mafunzo wanayoyaandaa Wanachama hao wajitahidi kuhudhuria
mafunzo wanapopata nafasi kwa kuwa ni muhimu lakini pia kila mmoja aendelee
kujiongezea elimu na kujifunza kwani elimu haina mwisho.
Vilevile
Mhe. Tiganga aliendelea kusema, “kila mmoja wetu ajitahidi kujibidiisha lengo
ni kwamba pamoja na kuhakikisha kazi za Mwajiri zinakwenda vizuri tujiandae
kukua kitaaluma pia ni vizuri kutambua tunao Mfumo unaotupima JOPRAS, mpimaji
anajaza eneo dogo sana hasa la maadili kwa kiasi kikubwa mfumo wenyewe
unakupima kutokana na utendaji wako wa kazi unachakata zile taarifa za kwenye
mfumo kwahiyo niwakumbushe na tuendelee kufahamu kwamba kujibidiisha ndipo
kutafanya tuonekane kuwa utendaji kazi wetu umebadilika mnatakiwa mfahamu kuwa
hatutakiwi kumuacha mtu yoyote nyuma hivyo tushirikiane kwa muda wote ushauri
na kila kitu kama mlezi na kiongozi wenu wa sasa napenda ushirikiano na
ninapenda kila mmoja wenu asonge mbele.”
Jaji
Mfawidhi huyo amewahakikishia Wana TMJA Tawi la Dodoma kuwa ataendelea kuwa
mlezi na mshauri lakini pia atatekeleza wajibu wake kama Mwanachama kama
ambavyo Katiba inamtaka pamoja na miongozo inavyotaka huku akisisitiza suala la
uhai wa Chama liwe la msingi sana na kuhakikisha chama hicho kinakuwa imara.
Kikao
hicho kiliambatana na mafunzo kuhusu
mbinu za uchukuaji wa ushahidi wakati wa usikilizaji wa mashauri ya jinai,
yaliyowasilishwa na Jaji wa Mahakama
Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Suleiman Hassan.
Katika
Mafunzo hayo Viongozi na Wajumbe mbalimbali walichangia, akiwemo Mhe. Tiganga, Mhe. Biswalo Mganga (Jaji),
Mhe. Irene Msokwa (Jaji).
Washiriki
walieleza kuwa mafunzo hayo yameongeza uelewa na yatachangia kuboresha utoaji
haki kwa kuzingatia misingi ya sheria na weledi.
Mbali
na mafunzo hayo, Wanachama walijadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo
ya Tawi, hususan namna ya kuendelea kuimarisha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa Wanachama.
Akizungumza wakati wa kufunga mjadala huo,
Mwenyekiti wa TMJA Dodoma, Mhe. Faisal
Kahamba, aliwahimiza wanachama kuendelea kutekeleza maazimio ya vikao
vya TMJA na kushiriki kikamilifu katika shughuli zote za Chama kwa lengo la
kuimarisha ushirikiano na mafanikio ya Tawi.
Vilevile,
wanachama walikumbushwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia
kaulimbiu ya Mahakama ya Tanzania isemayo "Uadilifu, Weledi na Uwajibikaji," ambayo ndiyo msingi
wa utoaji wa huduma bora za haki kwa wananchi.
Katika
kikao hicho pia, wajumbe walihimizwa kushiriki kwa wingi katika ziara ya Bagamoyo inayotarajiwa
kufanyika mwezi Septemba, 2026
ambayo itaambatana na Bonanza la kuimarisha afya, ushirikiano na mahusiano
miongoni mwa Wanachama wa TMJA.
Kwa
upande mwingine, Wanachama walitoa pongezi kwa uongozi wa TMJA Dodoma kwa
kuendelea kusimamia matendo ya huruma
katika jamii. Kupitia programu hiyo, tawi limefanikiwa kutoa misaada mbalimbali
ikiwemo vyakula, nguo, magodoro na
vifaa tiba kwa taasisi zenye uhitaji katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wa
Dodoma katika kipindi cha mwaka 2024
hadi 2026.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa wito uliotolewa kwa Wanachama kuendelea kudumisha mshikamano, kuongeza ushirikiano na kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kuendeleza mafanikio ya TMJA Dodoma na Mahakama ya Tanzania kwa ujumla.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Dodoma na Mlezi wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga (aliyesimama katikati mstari wa mbele) na Viongozi na Wajumbe wa TMJA mkoani huo mara baada ya kikao.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Dodoma na Mlezi wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga akiwasilisha hotuba yake kwa wajumbe wa TMJA Dodoma wakati wa kikao chao kilichofanyika hivi karibuni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni