Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile hivi
karibuni aliongoza Viongozi na Wajumbe wa Kikao cha Uongozi wa Mahakama hiyo
kufanya ziara ya kujifunza na kuimarisha ushirikiano na wadau wa Sekta Binafsi
katika Kiwanda cha Chumvi Lishe cha ‘Nyanza Salt Mine’ kilichopo Wilaya ya
Uvinza mkoani Kigoma.
Mara baada ya kumaliza Kikao
chao cha Uongozi kilichofanyika katika Mahakama ya Wilaya Uvinza, Viongozi hao
walitembelea Kiwanda hicho ili kujionea pia uwekezaji mkubwa wa Serikali katika
Sekta ya Madini.
Akiwa kituoni hapo, Mhe.
Rwizile na ujumbe wake walipata fursa ya kipekee ya kujionea kwa vitendo
mchakato mzima wa uzalishaji wa chumvi ya lishe ya mifugo maarufu kama
"Cattle Lick" pamoja na mnyororo mzima wa uzalishaji kuanzia
kuchimbwa kwa madini hayo ardhini hadi kufikia hatua ya mwisho ya bidhaa bora
iliyo tayari kwa matumizi ya walaji na wafugaji.
Aidha, Uongozi wa Mahakama
haukuacha kusifu jitihada zinazofanywa katika uwekezaji huo, huku wakitoa
pongezi za dhati kwa Kampuni ya Chumvi ya Nyanza (Nyanza Salt Mine) kwa kutoa
ajira kwa wananchi wa Kigoma na kuchangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji wa
uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Akitoa taarifa na elimu
kwa Viongozi hao wa Mahakama, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Bw. Mukesh
Mamlani, alieleza kuwa, kiwanda hicho kimekuwa na historia ndefu ya uzalishaji
na kwamba kiliizinduliwa rasmi Agosti, 2025 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony
Mavunde.
Uwekezaji huo ni
utekelezaji halisi wa maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya
kuhakikisha rasilimali na madini ya nchi yanaongezewa thamani hapa nchini na
kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi.
Uvinza sasa inashuhudia
mabadiliko makubwa; kutoka kutegemea machimbo ya jadi yaliyodumu tangu zama za
chuma, eneo hilo limegeuka kuwa kitovu cha viwanda vya kisasa vya kuchakata
chumvi.
“Chumvi lishe ni hitaji
muhimu kwa afya ya mifugo. Kupitia kiwanda hiki, tutahakikisha tunazalisha
bidhaa bora kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, ili wafugaji wa Tanzania
waweze kupata bidhaa salama, bora na kwa bei nafuu. Lengo letu ni kuinua ustawi
wa sekta ya mifugo nchini,” alisema Bw. Mamlani.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji
huyo, alibainisha kuwa, Kampuni hiyo ina mpango kabambe wa kuongeza uwekezaji
hadi kufikia Shilingi bilioni 20, hatua itakayosaidia kuongeza wigo wa
uzalishaji na kuchochea kwa kasi maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa wa Kigoma na
Taifa kwa ujumla.
Kadhlika, Viongozi na Wajumbe wa Kikao cha
Uongozi wa Mahakama Kuu Kigoma walikiri kuridhishwa na uzalishaji wa Kiwanda
hicho pamoja na miundombinu inayotumika na Watanzania wanaojipatia kipato
katika shughuli mbalimbali za kuzalisha chumvi lishe ya wanyama katika kiwanda
hicho cha chumvi wilayani Uvinza.
Wajumbe wa Kikao cha Uongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha ‘Nyanza Salt Mine’, Bw. Mukesh Mamlani (aliyenyoosha mkono) wakati Viongozi hao walipotembelea Kiwanda hicho kilichopo Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (wa pili kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Bw. Mukesh Mamlani mara baada ya Viongozi na Wajumbe wa Mahakama kuwasili katika Kiwanda cha Chumvi Uvinza.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (aliyevaa kofia), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi (wa kwanza kushoto), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masijala ndogo Kigoma Mhe. Fadhili Mbelwa (wa kwanza kulia) wakifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha ‘Nyanza Salt Mine’, Bw. Mukesh Mamlani wakati Viongozi hao walipotembelea Kiwanda hicho hivi karibuni.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya Kasulu, Mhe. Imani Batenzi,(kushoto), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya Uvinza Mhe. Misana Majula (kulia) na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Buhigwe, Mhe. Mwakitalu Venance (katikati) wakisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Bw. Mukesh Mamlani (hayupo katika picha).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (wa tatu kushoto) pamoja na Wajumbe wa Kikao cha Uongozi wa Mahakama Kuu Kigoma wakipata elimu ya uzalishaji wa chumvi kutoka kwa Ofisa Mwandamizi wa Kiwanda hicho (aliyenyoosha mkono).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (wa sita kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi (aliyesimama kushoto kwa Jaji Mfawidhi), akifuatiwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka (wa kwanza kulia) pamoja na Wajumbe wengine wa Kikao cha Uongozi walioambatana na Jaji Mfawidhi katika kutembela kiwanda hicho hivi karibuni.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni