Jumatano, 19 Agosti 2026

AMANI NA USALAMA NDIO MSINGI WA UWEKEZAJI: JAJI MRISHA

Na HABIBA MBARUKU, Mahakama

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe, Mhe. Abubakar Mrisha amesema amani na usalama ndio msingi mkuu wa kuvutia uwekezaji nchini na kusisitiza kuwa, utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050 haiwezi kufanikiwa bila mambo hayo mawili kuwepo.

Mhe. Mrisha ameyasema hayo leo tarehe 19 Agosti, 2026 kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Songwe, Mhe. Gabriel Malata wakati akitoa salamu za Mahakama katika Jukwaa la Dira 2050 na Uwekezaji lililofanyika mkoani Songwe.

“Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kwa upande wa Mahakama ndio msingi mkuu katika kutekeleza yote yanayotakiwa kutekelezwa kutokana na Dira kwanini nalisema hili, ni kwa sababu ili Dira iweze kutekelezwa lazima kuwepo na amani, kuwepo na usalama na haya yote ndiyo yatakayokuwa ni kivutio cha wawekezaji na wafanyabiashara katika nchi yetu,” amesema Mhe. Mrisha.

Mhe. Mrisha ameeleza kuwa, jukumu kubwa la Mahakama ni kutafsiri sheria zinazotungwa na Bunge pamoja na sheria ndogo (by-laws) zinazotungwa na Madiwani pale msuguano unapotokea, ili kuhakikisha sheria hizo zinaleta amani na usalama kwa jamii.

Akitoa mfano wa usogezwaji wa huduma karibu na wananchi, Jaji Mrisha amebainisha kuwa kuanzishwa kwa Mahakama Kuu ndani ya Mkoa wa Songwe kumesaidia kupunguza kero na gharama za wananchi waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kwenda Mbeya ili kupata huduma za rufaa, hatua ambayo imesaidia kuongeza muda wa kusikiliza mashauri na kuharakisha utoaji haki.

Amebainisha kwamba, haki ikichelewa inahesabika kuwa imekosekana, ndio maana Mahakama inaendelea na ujenzi wa Mahakama za Mwanzo na za Wilaya zikiwa zimeunganishwa na mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) itakayowezesha kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao, pamoja na matumizi ya Mahakama Inayotembea (Mobile Courts) ili kwenda na kasi ya utekelezaji wa Dira hiyo.

“Lakini kwa maendeleo ya TEHAMA Mahakama ina lengo la kufanya maendeleo na kuweka mfumo ambao kesi zitasikilizwa kwa njia ya mtandao, kwa hiyo utaona ni kwa kiasi gani tutakuwa tumepunguza gharama,” ameongeza Mhe. Mrisha.

Aidha, amewasihi wananchi na wadau mkoani Songwe kutumia fursa ya elimu na wataalam walioshiriki kwenye jukwaa hilo ili kuelewa fursa zilizopo na kuzitumia kuwekeza katika rasilimali za Mkoa huo kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Jukwaa la Dira 2050 na Uwekezaji limehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo kama Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mkuu wa Wilaya wa Songwe pamoja na viongozi vingine wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Songwe.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe, Mhe. Abubakar Mrisha akitoa salamu za Mahakama kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Songwe, Mhe. Gabriel Malata katika Jukwaa la Dira 2050 na Uwekezaji lililofanyika leo tarehe 19 Agosti, 2026 mkoani Songwe. 

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni