Na LIGHTNESS KABAJU-Mahakama ya Kazi na WINFRED NZILANO-Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Baadhi ya
viongozi kutoka Mahakama nchini China jana tarehe 20 Agosti, 2026, waitembelea
Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi na katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujifunza na
kubadilishana uzoefu kuhusu uendeshaji wa mashauri ya kazi.
Viongozi hao
ni Shan Guojun, ambaye ni mjumbe wa kudumu wa kamati ya uamuzi wa mashauri Mahakama
Kuu ya Watu Beijing na Wang Fei, ambaye ni Jaji wa Divisheni ya Kwanza ya Mashauri
ya Madai ya Mahakama ya Watu Beijing.
Wengine ni Wu
Bowen, ambaye ni Naibu Mkuu wa Divisheni ya Sita ya Madai Mahakama ya Watu Beijing
pamoja na Li Guodong, ambaye ni Naibu Jaji Mkuu wa Divisheni ya Kwanza ya Madai
ya Changping Beijing.
Wakiwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, wageni hao walipata maelezo kutoka kwa Naibu Msajili Mfawidhi wa
Divisheni ya Kazi, Mhe. Enock Matembele, ambaye aliwaelezea kwa kina namna
uendeshaji na usimamizi wa mashauri ya kazi unavyofanyika, ikiwemo hatua
mbalimbali zinazohusika katika mchakato wa utoaji haki.
Kwa upande
wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Ntemi
Kilekamajenga, aliwashukuru viongozi hao kwa kutenga muda wa kuitembelea
Mahakama na kushiriki katika ziara hiyo ya kubadilishana uzoefu.
Aidha,
aliwakaribisha tena kutembelea Mahakama hiyo wakati mwingine, akieleza kuwa
ushirikiano na kubadilishana uzoefu miongoni mwa Taasisi za Mahakama kutoka
nchi mbalimbali ni muhimu katika kuimarisha utoaji wa haki na ufanisi wa huduma
za Mahakama.
Viongozi hao
wa Mahakama China pia walitembelea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa lengo la
kubadilishana uzoefu kuhusiana na mamalaka ya Mahakama ya Hakimu Mkazi na
Mahakama ya Wilaya na namna mashauri ya kazi yanayohusiana na jinai na madai.
Ziara hiyo imekuwa sehemu muhimu ya kubadilishana uzoefu na maarifa kati ya mifumo ya utoaji haki ya Tanzania na China, hususan katika eneo la utatuzi wa migogoro ya kazi.
Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga akisalimiana
na Mhe. Shan Guojun baada ya kuwasili kwenye Mahakama hiyo kwa ziara ya mafunzo
na kubadilishana uzoefu kuhusu usikilizaji wa mashauri ya kazi.
Naibu Msajili Mfawidhi
wa Divisheni ya Kazi, Mhe. Enock Matembele, akiwaeleza wageni hao namna Mahakama
hiyo inavyoendesha mashauri.
Uongozi wa Mahakama
Kuu Divisheni ya Kazi na Viongozi wengine wa wakiwa katika kikao cha pamoja.
Picha ya
pamoja ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Ntemi
Kilekamajenga (mbele kushoto) na Viongozi wengine kutoka Mahakama nchini China.
Picha ya pamoja
ya Viongozi wa Mahakama nchini China na Mahakama ya Tanzania.
Viongozi wa Mahakama China wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Viongozi wa Mahakama China wakipitishwa kwenye mada mbalimbali.
Viongozi wa Mahakama China na Vingozi Mahakama ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ziara hiyo.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni