Ijumaa, 21 Agosti 2026

DKT. MAMBI AJITAMBULISHA KWA MKUU WA MKOA MANYARA

Na CHRISTOPHER MSAGATI - Mahakama, Manyara

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi amemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga ofisini kwake jana tarehe 20 Agosti, 2026 kwa ajili ya kujitambulisha kwa viongozi na wadau wa Mkoa wa Manyara tangu alipohamia Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara Mwezi Juni, 2026.

Mhe. Dkt. Mambi alimshukuru Mhe. Sendiga kwa kumkaribisha ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo, kufahamiana na kujadiliana juu ya utendaji kazi na ushirikiano unaopaswa kuwepo baina ya Ofisi hizo.

Aidha, Mhe. Dkt. Mambi alimuomba Mkuu wa Mkoa huyo aweze kusaidia katika suala la upatikanaji wa viwanja kila Kata za Mkoa wa Manyara kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo.

“Kwa kuwa huduma za Mahakama zinaendelea kukua kila siku, tunaomba utusaidie katika michakato mzima wa kupata viwanja pamoja na hati za umiliki katika Kata ambazo hamna huduma za Mahakama ili tuweze kujenga Mahakama hizo na kusogeza huduma karibu na wananchi,” alisema Mhe. Dkt. Mambi.

Kwa upande wake, Mhe. Sendiga alimuahidi Mhe. Dkt. Mambi kutekeleza jukumu hilo kwa kuwasiliana na mamlaka zilizopo chini yake ili viwanja hivyo vipatikane ili kukidhi adhima ya Mahakama ya kusogeza huduma za haki karibu na wananchi.

“Ninatambua kuwa Mkoa wetu wa Manyara una changamoto ya uhalifu na hususan mashauri ya kijinsia, na kwa sababu hiyo ni kweli kila mahali panahitaji kufikiwa na huduma hizi za Mahakama. Kwa sababu hiyo Mhe Jaji nitajitahidi kuwasiliana na viongozi wa Mamlaka nyingine ili tufanikiwe katika upatikanaji wa viwanja na hati hizo,” alisema Mhe. Sendiga.

Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Mambi, alikukutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kwa ajili ya kujitambulisha na kufanya nao mazungumzo juu ya ushirikiano wa Taasisi zao katika mnyonyoro wa Utoaji haki. Viongozi hao wa Kamati ya Ulinzi na Usalama walimkaribisha na kumuahidi ushirikiano wa kutosha katika kuhakikisha kazi za Mahakama zinakwenda ipasavyo.

Katika ziara hiyo, Mhe. Dkt. Mambi aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Charles Mnzava na Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Bi. Nyanzobe Hemei.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe. Dkt. Adam Mambi (wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga (katikati), (wa pili kushoto) ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Charles Mnzava, (kulia) ni Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Bi. Nyanzobe Hemed, na (kushoto) ni Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria Mhe. Kuruthumu Mkundawantu.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Manyara Mhe Charles Mnzava (aliyesimama) akichangia jambo wakati wa mazungumzo kati ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe. Dkt. Adam Mambi na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Manyara.

Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Manyara Bi. Nyanzobe Hemed (kushoto) akifuatilia mazungumzo kati ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe. Dkt. Adam Mambi na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga walipomtembelea Mkuu huyo wa Mkoa Ofisini kwake na kulia ni Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria Mhe. Kuruthumu Mkundawantu.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga (katikati) akichangia neno mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe. Dkt. Adam Mambi (kulia) pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Charles Mnzava mara baada ya kumtembelea ofsini kwake.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi akiwa anamsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga (hayupo pichani) mara baada ya kumtembelea ofisini kwake.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga akiwa ofisini kwake akifanya mazungumzo na  Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe. Dkt. Adam Mambi (hayupo pichani) wakati alipomtelea ofisini kwa ajili ya kujitambulisha.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe. Dkt. Adam Mambi (aliyekaa kwenye kiti) akiwa katika picha ya pamoja na timu ya viongozi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Manyara.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni