Ijumaa, 21 Agosti 2026

WATUMISHI MBEYA WAPITISHWA KWENYE RASIMU YA MPANGO MKAKATI WA MAHAKAMA 2026/27–2030/31

Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya, ameongoza mafunzo ya rasimu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa mwaka 2026/27–2030/31 kwa watumishi wa Mahakama Kuu kwa lengo la kuwajengea uelewa wa pamoja ili kila mtumishi aweze kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi na kuchangia katika kufikia malengo ya Taasisi.

Mafunzo hayo yamefanyika jana Agosti 20, 2026 katika ukumbi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya, yakijumuisha watumishi wa Mahakama kutoka Masjala Ndogo ya Mbeya na sehemu ya watumishi hao walishiriki mafunzo hayo kwa njia ya mkutano mtandao.

Akifungua mafunzo hayo, Mhe. Mtulya, alisisitiza umuhimu wa kila mtumishi kuuelewa kwa kina Mpango Mkakati wa Mahakama, akieleza kuwa, uelewa huo ni msingi muhimu wa utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

“Kila mtumishi wa Mahakama kwa ngazi zote anatakiwa afahamu kwa kina juu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ili kufanikisha malengo ya Taasisi, kwani kwa kufanya hivyo itatujengea ufanisi wa kutekeleza majukumu ili kulifikia lengo mama la Mahakama ya Tanzania la kutoa haki kwa wakati mapema ipasavyo,” alisema Mhe. Mtulya.

Jaji Mtulya ameongeza kuwa, uwasilishaji wa rasimu hiyo kwa watumishi wote unalenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mwelekeo wa Mahakama katika kipindi kijacho, hasa kutokana na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa Mpango Mkakati uliopita wa mwaka 2021/22-2024/25, ambapo watumishi wengi hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu Mpango Mkakati huo.

Watumishi hao walipitishwa kwenye utekelezaji wa Mpango Mkakati uliopita, ikiwa ni pamoja na mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza pamoja na mafunzo yaliyopatikana yanayopaswa kuzingatiwa katika kuandaa na kutekeleza Mpango Mkakati mpya.

Akifafanua umuhimu wa kuweka vipaumbele vinavyotekelezeka na vyenye tija, Mhe. Mtulya alisema: “Tunatakiwa kuwa na vipaumbele muhimu na vyenye tija na kuhakikisha bajeti iliyopo inaendana na vipaumbele vyetu,”

Amesisitiza kuwa, utekelezaji wenye mafanikio wa Mpango Mkakati wa Mahakama hautategemea mpango huo pekee, bali pia utayari, uwajibikaji na ushiriki wa kila mtumishi katika kutekeleza jukumu lake kwa kuzingatia mwelekeo na vipaumbele vya Taasisi.

Aidha, Jaji Mtulya alieleza kwa kina nguzo za kimkakati na maeneo ya msingi ya matokeo yaliyoainishwa katika rasimu hiyo, akifafanua namna malengo ya Taasisi yanavyoweza kufikiwa kupitia utekelezaji madhubuti wa majukumu ya kila mtumishi.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Festo Chonya, alisisitiza umuhimu wa kuwa na Mpango Mkakati ambao siyo kwa Taasisi pekee bali hata katika maisha ya mtu mmoja mmoja, akihusianisha umuhimu wa kupanga, kuweka malengo kuyafanyia kazi na utekelezaji wake.

Naye, Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mhe. Zawadi Laizer, alitoa shukrani kwa Jaji Mfawidhi kwa uwezeshaji wa mafunzo hayo, huku akisisitiza umuhimu wa kila mtumishi kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia nguzo za kimkakati za Mahakama.

“Wote tunahusika katika kuhakikisha kuwa, nguzo hizo za kimkakati zinakuwa msingi wa utekelezaji wa majukumu yetu,” alisema Mhe. Laizer.

Katika hatua nyingine, watumishi walipata fursa ya kutoa maoni, ushauri na mapendekezo kuhusu maboresho ya vipengele mbalimbali vya rasimu hiyo, hatua iliyolenga kuhakikisha kuwa maoni ya watumishi yanazingatiwa katika kuboresha rasimu kabla ya kukamilishwa.

Jaji Mfawidhi, aliwashukuru watumishi kwa kushiriki katika mafunzo hayo na kuwataka kutambua thamani ya nafasi waliyonayo kama watumishi wa umma. Aidha, amewasisitiza kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kuzingatia misingi ya utumishi wa umma katika kutekeleza majukumu yao.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (Katikati), akiwasilisha rasimu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania kwa watumishi ya mwaka 2026/27–2030/31, Kulia ni Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mhe. Zawadi Laizer na (kushoto) ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Festo Chonya.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Festo Chonya (aliyesimama) akizungumzia rasimu pendekezwa ya Mpango Mkakati wa Mahakama katika kikao hicho.

Sehemu ya Watumishi kutoka Mahakama mbalimbali Masjala Ndogo ya Mbeya walioshiriki na kupata mafunzo juu ya rasimu mpya ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ya Mwaka 2026/27–2030/31 katika mafunzo hayo.

Sehemu ya Watumishi kutoka Mahakama mbalimbali Masjala Ndogo ya Mbeya walioshiriki na kupata mafunzo juu ya rasimu mpya ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ya Mwaka 2026/27–2030/31 katika mafunzo hayo.

Sehemu ya Watumishi kutoka Mahakama mbalimbali Masjala Ndogo ya Mbeya walioshiriki na kupata mafunzo juu ya rasimu mpya ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ya Mwaka 2026/27–2030/31 katika mafunzo hayo.

Sehemu ya Watumishi kutoka Mahakama mbalimbali Masjala Ndogo ya Mbeya walioshiriki na kupata mafunzo juu ya rasimu mpya ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ya Mwaka 2026/27–2030/31 katika mafunzo hayo.

Sehemu ya Watumishi kutoka Mahakama mbalimbali Masjala Ndogo ya Mbeya walioshiriki na kupata mafunzo juu ya rasimu mpya ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ya Mwaka 2026/27–2030/31 katika mafunzo hayo.

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Paul Dandi Ntumo akitoa maoni yake ya kuboresha katika rasimu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ya Mwaka 2026/27–2030/31.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Mbeya Mhe. Tedy Mlimba (katikati) akichangia jambo katika Mafunzo hayo ya watumishi wa Masjala Ndogo ya Mbeya. 

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni