Na ARAPHA RUSHEKE -Mahakama Kuu Dodoma.
Tawi la Chama cha Wafanyakazi wa
Serikali Kuu na Afya (TUGHE) la Mahakama Kuu Dodoma limefanya mkutano wa
wanachama uliojaa furaha, mshikamano na hamasa, ukiambatana na kujadili masuala
mbalimbali ya ustawi wa wafanyakazi pamoja na kuwaaga wafanyakazi wastaafu na
wanaokaribia kustaafu.
Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi
wa Mahakama uliopo Kituo Jumuishi cha uUoaji Haki (IJC) tarehe 21 Agosti,2026.
Mkutano huo uliongozwa na Mlezi wa TUGHE Tawi la Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, ambaye ni Jaji Mfawidhi, Mhe. Joachim Tiganga. Mhe. Tiganga aliwapongeza wanachama kushiriki katika mkutano huo na kusisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano miongoni mwa wafanyakazi.
Jaji
Tiganga alisema kuwa anaamini kikao hicho kitakuwa na manufaa kwa wanachama,
akieleza kuwa TUGHE ni chama cha hiari kinacholenga kuwaleta pamoja wafanyakazi
na kuwawezesha kushirikiana katika kujenga na kulinda maslahi yao.
Alitoa
wito kwa wafanyakazi ambao bado hawajajiunga na TUGHE kujiunga kwa kadri
watakavyoweza, akisisitiza kuwa nguvu ya wafanyakazi inatokana na kuwa na umoja
na sauti moja.
Aidha,
Jaji Mfawidhi alisisitiza ujumbe wa mshikamano unaosisitizwa kupitia wimbo wa
TUGHE, akieleza kuwa wafanyakazi wanapaswa kuungana kwani kujitenga kunaweza
kudhoofisha uwezo wao wa kusimamia masuala yao kwa pamoja.
Katika
mkutano huo pia kulijadiliwa suala la afya
ya akili, ambapo mada hiyo iliwasilishwa na Daktari kutoka Hospitali ya
Mirembe, kwa lengo la kuongeza uelewa miongoni mwa wafanyakazi kuhusu umuhimu
wa afya ya akili katika maisha na mazingira ya kazi.
Hafla
hiyo ilihitimishwa kwa furaha na bashasha, ambapo wafanyakazi wastaafu pamoja
na wanaokaribia kustaafu walikabidhiwa zawadi kama ishara ya kuthamini mchango
wao katika utumishi wa Mahakama.
Shamrashamra
ziliendelea kwa kukatwa kwa keki na kusherehekea pamoja, huku zawadi maalumu zikitolewa kwa Jaji Mfawidhi
na Mtendaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Bw. Bedson Mariba, hali iliyoongeza
furaha na kuufanya mkutano huo kuwa wa kipekee.
Mkutano huo umeendelea kuonesha umuhimu wa umoja, mshikamano na kujali ustawi wa wafanyakazi ndani ya Mahakama Kuu Dodoma.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma na Mlezi wa TUGHE Tawi la
Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, wakati akiwasilisha hotuba yake wakati
wa kikao hicho.
Sehemu
ya wajumbe wa Tawi la TUGHE Mahakama Kuu Dodoma wakiimba wimbo wa mshikamano
mara baada ya ufunguzi wa kikao.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma na Mlezi wa TUGHE Tawi la
Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga akifurahishwa kwa bashasha na zawadi
aliyopewa na wajumbe wakati wa kikao hicho.
Sehemu
ya wajumbe wa TUGHE Tawi la Mahakama Kuu Dodoma wakifurahia jambo wakati wa
kikao hicho.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma na Mlezi wa TUGHE Tawi la
Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga (wa kwanza kushoto) pamoja na
Mtendaji wa Mahakama Dodoma, Bw. Bedson Mariba wakifurahishwa kwa bashasha na
zawadi waliyopewa na wajumbe wakati wa kikao hicho.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni