Jumatano, 19 Agosti 2026

JAJI MFAWIDHI MAHAKAMA YA KAZI ATEMBELEA TUME YA USULUHISHI NA UAMUZI

Na MWANDISHI WETU-Mahakama ya Kazi, Dar es Salaam

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga, jana tarehe 18 Agosti, 2026 alitembelea Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).

Lengo la ziara hiyo ni kujionea utendaji, kufahamu kwa undani namna inavyotekeleza majukumu yake na kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama ya Kazi na Tume katika kuhakikisha migogoro ya kikazi inatatuliwa kwa ufanisi na kwa wakati.

Ziara hiyo imekuwa ya kwanza kwa Mhe. Dkt. Kilekamajenga  katika Tume hiyo tangu alipoteuliwa kuwa Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuendelea kujenga uelewa na ushirikiano wa kiutendaji kati ya Taasisi zinazohusika katika mnyororo wa utoaji wa haki kazi nchini.

Jaji Mfawidhi alipokelewa na uongozi wa Tume na kupata fursa ya kutembelea baadhi ya ofisi, ambapo alijionea mazingira ya kazi na namna watumishi wanavyotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Uongozi wa Tume ulimweleza Jaji Mfawidhi na wajumbe aliokuwa ameambatana nao kuhusu majukumu mbalimbali ya CMA, muundo wa utendaji kazi pamoja na nafasi ya Tume katika utatuzi wa migogoro ya kikazi nchini.

Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ni Taasisi huru ya utatuzi wa migogoro ya kikazi iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Kazi. Miongoni mwa majukumu yake ni kufanya usuluhishi wa migogoro ya kikazi inayowasilishwa mbele yake na, kwa mujibu wa sheria, kuamua migogoro kupitia mchakato wa uamuzi.

Akizungumza katika kikao cha pamoja, Mkurugenzi Mkuu wa CMA, Mhe. Usekelege Mpulla, alimweleza Jaji Mfawidhi kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri ya Usuluhishi na Uamuzi unaojulikana kama e-Utatuzi.

Mfumo huo ulianza kutumika rasmi Januari 21, 2026, ukiwa na lengo la kuboresha usimamizi na uendeshaji wa mashauri ya migogoro ya kikazi kwa kutumia teknolojia ya kidijitali.

Mfumo huo unamwezesha mdau kusajili na kufuatilia shauri lake kwa njia ya mtandao, bila kulazimika kufika ofisi za Tume kwa kila hatua.

Mpaka sasa, zaidi ya mashauri 1,678 yamewasilishwa kwa njia ya mfumo  ambapo mashauri 622 yameisha kwa njia ya usuluhishi na mashauri 277 yameisha kwa njia ya uamuzi.

Hata hivyo, Kiongozi huyo alieleza kwamba jitihada za kufanya mfumo huo usomane na mfumo wa usimamizi wa mashauri unaotumiwa na Mahakama ya Tanzania.

Akielezea umuhimu wa mfumo huo, Mkurugenzi wa CMA alisema matumizi ya e-Utatuzi yanalenga kuongeza ufanisi katika utendaji wa Tume, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza gharama ambazo wadaawa wanaweza kuzitumia katika kufuatilia mashauri yao.

Mfumo huo umesaidia kupunguza utegemezi wa majalada ya nakala ngumu, kuimarisha usimamizi wa nyaraka za mashauri na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika hatua mbalimbali za mchakato wa utatuzi wa migogoro.

Aidha, matumizi ya mfumo huo yanaongeza uwezekano wa huduma za utatuzi wa migogoro kufikiwa kwa urahisi zaidi na wananchi walioko maeneo mbalimbali nchini.

Mhusika anaweza kusajili na kufuatilia mwenendo wa shauri lake akiwa mahali alipo, kwa kutumia kifaa chenye mtandao, jambo linalosaidia kupunguza ulazima wa kusafiri mara kwa mara kwenda katika ofisi za Tume.

Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Kilekamajenga aliipongeza Tume kwa namna inavyotekeleza majukumu yake katika kusaidia kutatua migogoro ya kikazi na kwa hatua zinazochukuliwa katika kuboresha huduma kwa wananchi.

Jaji Mfawidhi alieleza kuwa ziara hiyo imempa fursa ya kupata uelewa mpana zaidi kuhusu utendaji wa CMA, changamoto zinazokabili Tume pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kuboresha huduma za usuluhishi na uamuzi.

Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama ya Kazi na CMA, akieleza kuwa Taasisi hizo zina nafasi muhimu katika mfumo wa utoaji wa haki za kazi nchini.

Jaji Mfawidhi aliwataka viongozi na watumishi wa Taasisi hizo kuendelea kushirikiana katika kubaini maeneo yanayohitaji maboresho, kubadilishana uzoefu na kutafuta njia bora za kuongeza ufanisi katika utatuzi wa migogoro ya kikazi.

Aidha, aliwasihi viongozi wa CMA kuendelea kufanya jitihada ili kuhakikisha mifumo hiyo inasomana na kurahisisha uendeshaji wa mashauri katika utoaji haki kazi.

Ziara hiyo imeonesha umuhimu wa mawasiliano na ushirikiano wa mara kwa mara kati ya Taasisi zinazohusika katika utoaji wa haki za kazi. Kwa kuwa CMA na Mahakama ya Kazi zina majukumu yanayogusana katika mnyororo wa utatuzi wa migogoro ya kikazi, ushirikiano wao unaweza kusaidia kubaini changamoto za kiutendaji na kutafuta suluhisho kwa pamoja.










Hakuna maoni:

Chapisha Maoni