Jumanne, 18 Agosti 2026

IDARA YA MIPANGO, URATIBU YAENDESHA MAFUNZO KUSHUGHULIKIA VIHATARISHI NYANDA ZA JUU KUSINI

Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Idara ya Mipango na Uratibu ya Mahakama ya Tanzania inaendesha Mafunzo kuhusu matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Uratibu wa Vihatarishi kwa watendaji wa Mahakama Kuu pamoja na Maafisa Vihatarishi kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo Songwe, Iringa, Njombe, Songea, Sumbawanga na Mbeya.

Mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 17 Agosti, 2026 katika Masjala Ndogo ya Mbeya, yanalengo la kuwajengea uwezo watendaji na Maafisa bajeti wa Mahakama ya Tanzania katika kubaini, kutathmini na kukabiliana na vihatarishi vinavyoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu na malengo ya Mahakama katika suala zima la utoaji wa haki kwa wananchi.

Akifungua mafunzo hayo ya mfumo mpya unaotambulika kama GERMIS (Government Enterprise Risk Management Information System), Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti, Uendelezaji na Ubunifu kutoka Idara ya Mipango na Uratibu Mahakama ya Tanzania, Bw. Kisingi Salehe Mhando, amesema kuwa, mafunzo yanalenga kuimarisha uelewa na uwezo wa washiriki katika matumizi ya mfumo mpya wa kielektroniki wa kubaini na kuratibu vihatarishi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Mahakama katika kuhakikisha malengo yake yanafikiwa kwa ufanisi.

Bw. Mhando amesema kwamba, mfumo huo utasaidia Mahakama kubaini vihatarishi kwa wakati, kuvifanyia tathmini na kuweka mikakati stahiki ya kukabiliana navyo kabla havijaathiri utekelezaji wa mipango na shughuli za Mahakama.

Aliongeza kuwa mfumo mpya unaleta maboresho katika namna ya kuratibu vihatarishi ikilinganishwa na mfumo wa awali, hususan katika kurahisisha mchakato wa kutambua, kurekodi, kufuatilia na kuchukua hatua dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kujitokeza katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali.

Katika siku ya kwanza ya mafunzo, washiriki wamejifunza kuhusu asili ya vihatarishi, matokeo hasi na chanya ya vihatarishi, pamoja na tofauti kati ya kihatarishi (risk) na tatizo (problem). Aidha, wamepata uelewa kuhusu aina na mgawanyo wa vihatarishi pamoja na misingi ya namna ya kukabiliana navyo kupitia dhana ya Usimamizi wa Vihatarishi (Risk Management).

Akifafanua zaidi kuhusu tofauti kati ya kihatarishi na tatizo, Bw. Mhando amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua mapema ili kuzuia kihatarishi kisifikie hatua ya kuwa tatizo linalohitaji rasilimali kubwa zaidi katika kulitatua.

“Rasilimali zinazotumika kutatua kihatarishi ni chache na gharama ndogo ukilinganisha na rasilimali na gharama zinazotumika kutatua tatizo. Hivyo, tuweke nguvu kubwa katika kuthibiti vihatarishi kabla haijafikia hatua ya kuwa tatizo,” alisema Bw. Mhando

Kwa upande wake, Mtakwimu kutoka Idara ya Mipango na Uratibu ya Mahakama ya Tanzania Bw. Mussa Wigute, ameongeza kwa kusema kuwa, usimamizi wa vihatarishi haukusudii kuondoa vihatarishi vyote, bali ni kuweka mikakati inayowezesha taasisi kuendelea kufikia malengo yake licha ya uwepo wa vihatarishi.

Mafunzo hayo yanaendeshwa na timu ya wakufunzi kutoka Idara ya Mipango na Uratibu ya Mahakama ya Tanzania, inayoongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti, Uendelezaji na Ubunifu Bw. Kisingi Salehe Mhando, akisaidiwa na Mtakwimu, Bw. Mussa Wigute, pamoja na Mchumi Bi. Reine Kissae.

Mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kupata ujuzi na maarifa ili kwenda kuwa mabalozi kwa watumishi wengine wanaoshughulikia vihatarishi kuhusu matumizi ya mfumo huo mpya wa kielektroniki na namna utakavyotumika katika kuimarisha usimamizi wa vihatarishi, utekelezaji wa mipango na matumizi bora ya rasilimali za Mahakama.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa (wa kwanza kushoto), Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songea Bw. Allan Mwela (Katikati), na Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Njombe, Bw. Richard Mbambe (wa kwanza kulia) wakiwa katika mafunzo hayo.

Afisa Utumishi kutoka Masjala Ndogo ya Mbeya Bi. Sarah Rossi akichangia jambo kama sehemu ya washiriki katika mafunzo hayo.

Sehemu ya washiriki katika mafunzo hayo.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Festo Chonya (kulia) na Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe, Bw. Sostenes Mayoka (kushoto) wakifuatilia kwa karibu mafunzo hayo.

Sehemu ya watendaji wa Mahakama ambao ni washiriki katika mafunzo hayo.

Mchumi kutoka Idara ya Mipango na Uratibu Mahakama ya Tanzania, Bi. Reine Kissae. (aliyesimama) akitoa elimu juu ya mfumo mpya wa GERMIS unavyofanya kazi.

Mtakwimu kutoka Idara ya Mipango na Uratibu Mahakama ya Tanzania, Bw. Mussa Wigute akitoa ufafanuzi juu ya kukabiliana na vihatarishi katika mafunzo hayo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti, Uendelezaji na Ubunifu kutoka Idara ya Mipango na Uratibu Mahakama ya Tanzania, Bw. Kisingi Salehe Mhando akiendesha mafunzo hayo kwa washiriki (hawapo pichani)

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni