Na AMINA SAID - Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Dar es Salaam
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu, amewataka watumishi wa Mahakama Kuu-Divisheni
ya Biashara kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi huku
akisisitiza umuhimu wa kila mtumishi kutambua nafasi yake katika kuimarisha utendaji
kazi na kufanikisha malengo ya Taasisi.
Dkt. Jingu aliyasema hayo
tarehe 17 Agosti, 2026 wakati wa ziara yake katika Divisheni hiyo, iliyolenga
zaidi kuimarisha mahusiano, kufahamiana na kujenga mawasiliano ya karibu kati
ya uongozi na watumishi, pamoja na kupata fursa ya kusikiliza maoni na hoja
mbalimbali zinazohusu utekelezaji wa majukumu na mazingira ya kazi.
Akizungumza na watumishi
hao, Dkt. Jingu amesisitiza kuwa, Mahakama ni Mhimili wa kutenda haki na kwamba
uimara wake una umuhimu mkubwa kwa ustawi wa nchi.
“Mahakama ni Mhimili wa
kutenda haki, ukikaa vizuri, Nchi inakaa vizuri; ikiyumba, Nchi inayumba. Kwa
hiyo tuna jukumu la kuilinda Mahakama yetu,” alisema Mtendaji Mkuu.
Kadhalika, amesema jukumu
la kuilinda Mahakama linaanzia kwa kila mtumishi kutekeleza wajibu wake kwa
uadilifu, weledi na kujituma, akieleza kuwa utendaji mzuri wa watumishi ni
sehemu muhimu ya kuimarisha Taasisi na kujenga hoja zenye msingi kuhusu
maboresho na maslahi mbalimbali ya watumishi.
Dkt. Jingu pia amewataka
watumishi kuwa wabunifu katika nafasi zao za kazi kwa kutumia rasilimali
zilizopo na kutafuta njia bora za kutekeleza majukumu yao.
Amesisitiza kuwa, ubunifu
hauhitaji rasilimali nyingi kila wakati, bali unahitaji utayari wa kutumia
fursa zilizopo na kuboresha namna ya kufanya kazi.
Aidha, Mtendaji amewataka
watumishi kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na kujenga utamaduni wa
kusaidiana, kuthaminiana na kuheshimiana, huku akisisitiza kuwa kila mtumishi
ana mchango katika kufanikisha majukumu ya Mahakama.
Katika ziara hiyo,
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara, Bw. Anathory
Kagaruki aliwasilisha taarifa ya kiutawala kuhusu hali ya Divisheni hiyo.
Taarifa hiyo ilihusu
maeneo mbalimbali ya uendeshaji, ikiwemo hali ya watumishi, hali ya kifedha,
vyombo vya usafiri na maslahi ya watumishi pamoja na masuala mengine yanayohusu
utekelezaji wa majukumu ya Mahakama hiyo.
Baada ya taarifa hiyo,
watumishi walipata fursa ya kuwasilisha hoja, maoni na changamoto mbalimbali
kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
Hoja hizo zilihusu
masuala mbalimbali yanayowagusa watumishi katika utekelezaji wa majukumu yao na
mazingira ya kazi, huku wakitoa mapendekezo yenye lengo la kuboresha utendaji
na ustawi wa watumishi.
Katika ziara hiyo, Dkt.
Jingu amewataka watumishi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kujituma na kwa
kuzingatia wajibu wao wa kulinda heshima, uadilifu na hadhi ya Mahakama ya
Tanzania.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu (aliyesimama) akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara alipotembelea Mahakama hiyo jana tarehe 17 Agosti, 2026. Aliyeketi kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni Maalum, Bi. Mary Shirima na kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Bw. Anatory Kagaruki.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara wakisikiliza kwa makini maelekezo ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu (hayupo katika picha) alipokuwa akizungumza nao.
Mwandishi Mwendesha Ofisi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Bi. Tausi Mwambujule akiwasilisha hoja mbele ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu (hayupo katika picha).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Kevin Mhina (kulia) akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu (kushoto) alipowasili katika Mahakama hiyo jana tarehe 17 Agosti, 2026.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara, Mhe. Kevin Mhina (aliyeketi mbele) akiwa katika kikao na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu (aliyeketi wa kwanza kulia kwa Jaji Mfawidhi) pamoja na sehemy ya Viongozi walioambatana na Mtendaji Mkuu (kushoto). Kulia ni Majaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni Maalum, Bi. Mary Shirima (aliyesimama) akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara wakati wa ziara ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama katika Mahakama hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu (kushoto) akisalimiwa na kukaribishwa na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara, Bw. Anatory Kagaruki (kulia) wakati Mtendaji Mkuu alipowasilisha katika Divisheni hiyo tarehe 17 Agosti, 2026. Wa pili kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni Maalum, Bi. Mary Shirima na wa kwanza kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara, Mhe. Suzan Kihawa.
Picha ya pamoja kati ya Viongozi wa meza kuu na Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara. Aliyeketi katikati ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu, kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni Maalum, Bi. Mary Shirima na kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara, Bw. Anatory Kagaruki.
(Picha na IMAN KASSIAN, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara)
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni