Jumatatu, 17 Agosti 2026

JAJI KIREKIANO MWENYEKITI MPYA TMJA TAWI LA DAR ES SALAAM

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Arnold Kirekiano amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Dar es Salaam  baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Jaji, Mhe. David Ngunyale kuhamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ndogo ya Bukoba.

Mhe. Kirekiano alichaguliwa katika Mkutano Mkuu Maalum, uliofanyika tarehe 14  Agosti, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho,  Jaji Kirekiano, ambaye alimuwakilisha Mlezi wa Tawi hilo, ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi aliwasisitiza Majaji na Mahakimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia uadilifu, weledi na uwajibikaji katika utendaji kazi wao.

“Sisi Wanachama wa TMJA ambao ni sehemu ya watumishi wa Mahakama, tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutimiza wajibu wetu katika mambo yote ambayo Mahakama inayafanya katika kuhudumia wananchi. Haitaleta picha nzuri, ikiwa mambo ambayo tulipaswa kuyafanya hatuyafanyi,” alisisitiza Mhe. Kirekiano.

Aidha, aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa, matumaini ya Jaji Mfawidhi ni kwamba, kikao hicho kitakuwa ni mwanzo wa kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Akiendelea kutoa salamu za Mlezi wa Chama hicho, Mhe. Kirekiano pia aliwajulisha wajumbe wa mkutano huo, kuwa Mahakama inaendelea na maboresho mbalimbali na kwa sasa rasimu ya Mpango Mkakati, inaandaliwa na ipo katika hatua ya ushirikishwaji wa ndani kabla haijatoka nje kama nyaraka rasmi.

Jaji Kirekiano aliwataka wanachama hao kuwa mstari wa mbele katika kutoa maoni yao pindi rasimu hiyo itakaposhushwa kwao na kwamba wao kama Maofisa wa Mahakama  ambao wanafanya jukumu la msingi la utoaji haki, wanapaswa kufanya hivyo ili wakati wa utekelezaji wawe wamepata kile ambacho kimekuwa kikitarajiwa.

Mhe. Kirekiano alitumia mkutano huo kutoa mwaliko kwa wajumbe wote kwa niaba ya  Jaji Mfawidhi kushiriki kikamilifu katika Bonanza lililoandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dar es Salaam litakalofanyika Jumamosi tarehe 22 Agosti, 2026 katika Viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Saalam.

Katika mkutano huo pia kulikuwa na uchaguzi wa Mwenyekiti wa Chama hicho, Tawi la Dar es salaam, ambapo wajumbe, walipiga kura na kumchagua Mhe. Jaji Kirekiano kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ndogo ya Dar es Salaam, Mhe. Arnold Kirekiano (aliyesimama) ambaye pia ni Mwenyekiti mpya wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Dar es Salaam akitoa shukrani kwa Wanachanma kwa kumchagua kuwa Mwenyekiti wa TMJA- Dar es Salaam. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa TMJA Tawi la Dar es Salaam, Mhe. Ramadhan Rugemalira na kulia ni Katibu wa TMJA, Mhe. Marko Mochiwa.

Baadhi ya wanachama wa TMJA Tawi la Dar es Salaam wakiwa katika kikao cha chama hicho.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dar es Salaam na Mwenyekiti mpya wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), Mhe. Arnold Kirekiano (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wanachama wa TMJA Tawi la Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Mhe. Ramadhan Rugemalira, Makamu Mwenyekiti wa TMJA Tawi la Dar es Salaam, wa kwanza kulia ni Mhe. Jacqline Rugemalira, Mhazini wa TMJA Tawi la Dar es Salaam, wa kwanza kushoto ni Mhe. Ishaq Kuppa, Mwakilishi wa TMJA Tawi la Dar es Salaam  na wa pili kushoto ni Katibu wa Tawi hilo, Mhe. Marko Mochiwa.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni