Jumanne, 18 Agosti 2026

MAOFISA MAGEREZA SINGIDA WANOLEWA KUHUSU MIFUMO YA KIELEKTRONI YA MAHAKAMA

EVA LESHANGE & AMIRI BAKARI, Mahakama – Singida

Maofisa Magereza wanaohusika na Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mkoani Singida wamepatiwa mafunzo ya Mifumbo mbalimbali ya Kielektroni ya Mahakama lengo likiwa ni kuwajengea uelewa Maofisa hao juu ya mifumo mbalimbali ya kimahakama ikiwemo Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-Case Management System), Mahakama Mtandao (Virtual Court) na Mfumo wa Taarifa za Maamuzi, Sheria na Kanuni za Tanzania (TanzLII).

Akifungua mafunzo hayo jana tarehe 17 Agosti, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Singida, Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Mhe. Jasmin Abdul aliwasisitiza washiriki kuongeza ufanisi katika kutoa huduma na kuwa wabunifu ili kutoa Haki kwa wakati.Aidha mafunzo haya yalihusisha maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Magereza Mkoa wa Singida,Maafisa kutoka Magereza ya Wilaya Singida, Iramba,Ushora na Manyoni.

“Watumishi wenzangu napenda kuwajulisha kuwa Mahakama ya Tanzania kwa sasa inatumia mifumo ya TEHAMA katika kuendesha shughuli zake za kila siku hususan za utoaji haki na Magereza ni miongoni mwa Wadau muhimu wa Mahakama, ni matarajio yangu kuwa katika mafunzo haya mtajifunza kwa vitendo, mtabadilishana uzoefu na mwisho kubaini changamoto na kuzitafutia suluhu hivyo muwe wazi na tayari kujifunza,” alisema Naibu Msajili huyo.

Aidha, aliwasisitiza kufanya kazi kwa ushirikiano wanapopata changamoto za kimfumo kuziwasilisha kwa haraka na kwamba mafunzo hayo yatakuwa endelevu kwa kadri mabadiliko kimifumo yanayotokea.

Mada za mafunzo hayo ya TEHAMA ziliwasilishwa na Ofisa TEHAMA Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida, Bi.Valentina Nkullanga ambapo katika uwasilishaji wake aliwaeleza Maofisa Magereza kuwa matumizi ya mifumo hiyo katika uendeshaji wa shughuli za Mahakama umeleta manufaa makubwa kwa Mahakama na Wadau kwani imeongeza ufanisi katika usimamizi wa mashauri, imepunguza matumizi ya karatasi.

Manufaa mengine ni kupunguza ucheleweshwaji wa mashauri, kuimarika kwa usalama, kupunguza gharama za usafirishwaji wa Mahabusu na kuongezeka kwa upatikanaji wa haki mapema ipasavyo.

Katika mafunzo, walijifunza pia kwa vitendo hatua zote kuanzia shauri linavyosajiliwa hadi kukatiwa rufaa na waliona maandalizi ya awali katika kuandaa mashauri yanayosikilizwa kwa njia ya mtandao namna ya kuandaa vitendea kazi, kuviunganisha na mtandao.

Kadhalika, walielekezwa namna ya kuingia katika mfumo wa TanzLII kwa ajili ya kupata nakala za hukumu za wafungwa wao na kupata rejea mbalimbali kwa ajili ya kujifunza.

Akihitimisha mafunzo hayo Naibu Msajili wa Mahakama, Mhe. Allu Nzowa aliwasisitiza washiriki kufanya kazi kama timu na kuyachukulia mabadiliko hayo katika mtazamo chanya ili kuleta ufanisi zaidi.

  Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Mhe. Jasmin Abdul akizungumza jambo na Washiriki wa Mafunzo ya Mifumo ya Kielektroni ya Mahakama (hawapo katika picha) wakati wa ufunguzi wa Mafunzo kwa Maofisa Magereza tarehe 17 Agosti, 2026.

  Ofisa TEHAMA wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Bi Valentina Nkullanga (aliyesimama) akitoa mada kwa washiriki wa Mafunzo hao (hawapo katika picha) wakati wa mafunzo na  Maofisa Magereza.

 CPL Yondani Kibuti kutoka Gereza la Wilaya Singida akichangia jambo wakati wa mafunzo hayo.

  Meza Kuu ikiongozwa na Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Allu Nzowa (aliyeketi katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa Mafunzo kutoka Gereza la Wilaya Manyoni. Aliyeketi kulia ni Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya Wilaya Singida na Mwenyekiti Kamati ya Elimu Kanda, Mhe. Aloyce Masua na kushoto ni Afisa Utumishi Mahakama Kuu Singida, Bi.Eva Leshange.

 Meza Kuu ikiongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Allu Nzowa (aliyeketi katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na Washiriki kutoka Gereza la Wilaya Iramba. Aliyeketi kulia ni Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya Wilaya Singida na Mwenyekiti Kamati ya Elimu Kanda, Mhe. Aloyce Masua na kushoto ni Afisa Utumishi Mahakama Kuu Singida, Bi.Eva Leshange.

  Meza Kuu ikiongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Allu Nzowa (aliyeketi katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki kutoka Gereza la Wilaya Singida. Aliyeketi kulia ni Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya Wilaya Singida na Mwenyekiti Kamati ya Elimu Kanda, Mhe. Aloyce Masua na kushoto ni Afisa Utumishi Mahakama Kuu Singida, Bi.Eva Leshange.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni